Hii picha hausiani na stori hapo chini
Mganga Mfawidhi wa hospitali hiyo, Dk. Fredrick Mlekwa, jana alisema tukio hilo lilitokea juzi saa 12 jioni wakati binti huyo alipofikishwa hospitali hapo akitokea katika Kituo cha Afya cha Kambarage, mjini Shinyanga.
“Tulimfanyia uchunguzi na kugundua alikuwa na mimba ya mapacha lakini wakiwa tayari wamefia tumboni, hivyo muuguzi wa zamu katika wodi ya wazazi alianza kumhudumia ili kuwatoa watoto hao tumboni” alisema.
Alisema wakati muuguzi wa zamu akiendelea na zoezi hilo, mama mzazi wa binti huyo aliingia chumba cha kuzalishia na kumkuta mwanae ametolewa viumbe mfu na kuanza kupiga kelele na kumfokea muuguzi huyo kwa matusi hali iliyosababisha vurugu na wananchi kujaa kutaka kumshambulia muuguzi huyo kwa madai amesababisha vifo vya mapacha hao.
Mlekwa alisema watoto hao walikuwa na uzito wa gramu 200 na 500 na ujauzito huo wa miezi sita uliharibika mapema na kulazimika kuwatoa watoto hao kwa upasuaji mdogo ili kuokoa maisha ya binti huyo.
Mama mzazi wa binti huyo, Mwanahamisi Juma, mkazi wa mtaa wa Mshikamano mjini Shinyanga, alisema mwanaye ambaye ni mwanafunzi wa kidato cha pili katika Shule ya Sekondari Mwasele, mjini humo, alishindwa kuhudumiwa kutokana na muuguzi huyo kuonekana bize akichati na simu.
“Nilipoingia katika chumba cha kuzalishia nilimkuta mwanangu anajifungua watoto hao huku muuguzi akichati na simu na kutompa msaada wowote unaohitajika, hivyo kuamua kumfokea kwa hasira,” alisema Mwanahamisi.
Hata hivyo, muuguzi huyo, Yasinta, alisema wakati binti huyo anajifungua watoto walikuwa tayari wamekufa hivyo aliamua kuwapigia wenzake simu ili wamsaidie na ghafla alivamiwa na mama huyo na kuanza kuporomoshewa matusi hadi Mganga Mfawidhi wa hospitali hiyo alipoingilia kati na kuokoa.
CHANZO: NIPASHE
1 comment:
wauguzi wa bongo wanaruhusiwa kutumia simu wakiwa kazini!
Post a Comment