Hii picha ni mtoto Mary Rappyson Ishabakaki mwenye umri wa miaka 4 aliyepotea July 15, 2014. Picha hii haiusiani na habari hapo chini.
Mwanamke mmoja mkazi wa Mchikichini, Mbagala jijini Dar es Salaam, Tatu Nyambwela (30) anashikiliwa na polisi baada ya kutuhumiwa kumuiba mtoto mchanga wa miezi mitatu.
Polisi pia inachunguza mtoto wake mwingine wa miaka sita anayeishi naye baada ya kudaiwa kuwa alimpata kwa njia ya udanganyifu.
Taarifa kutoka eneo hilo zinasema mwanamke huyo alikamatwa wiki iliyopita na kufikishwa katika Kituo cha Polisi Mbagala Maturubai, baada ya majirani kumtilia shaka.
Akizungumzia tukio hilo, Mwenyekiti wa mtaa huo, Said Pazi, alisema alipata taarifa hizo kupitia kwa majirani wanaoishi eneo hilo, ambapo baada ya kujiridhisha aliamua kutoa taarifa polisi.
MTOTO AGUNDULIKA
Akielelezea tukio hilo, alisema walikwenda nyumbani kwa mwanamke huyo akiwa pamoja na polisi wawili kwa ajili ya kubaini ukweli wa jambo hilo.
Alisema, walipofika katika nyumba anayoishi mwanamke huyo, walimkuta akiwa amekaa pamoja na mumewe aliyetajwa kwa jina la Adinan Mkanilo (45), na mama mkwe wake Asha Limbanga (80) wakizungumza.
Mwenyekiti huyo alisema walipomuhoji uhusiano wa mama huyo na mtoto mchanga, Tatu alionekana kuwa mkali na kueleza mtoto ni wake amemzaa Septemba 9, mwaka huu.
Alipotakiwa kuthibitisha kauli yake kwa kuonyesha kadi ya kliniki, hakuweza kuitoa badala yake alisema alimzaa nyumbani, hivyo hakuweza kupata kadi kama ilivyo kwa watoto wengine.
"Mashaka yetu yalizidi baada ya kuona yule mama hana kadi ya kliniki na hata tulipomshauri atuletee mtoto tumuone, alikataa jambo ambalo ilibidi polisi kutumia nguvu kuingia ndani kumuona mtoto," alisema mwenyekiti huyo.
"Baada ya kufanikiwa kumpata mtoto tulibaini amedanganya umri kwani kwa mujibu wake mtoto alikuwa wa mwezi mmoja, kitu ambacho siyo kweli, tulipomuangalia tulibaini alikuwa na umri wa zaidi ya miezi mitatu," alisema.
Baada ya kushuhudia hali hiyo, polisi walimkamata mwanamke huyo pamoja na mume wake na kuwapeleka katika kituo cha Mbagala kwa ajili ya mahojiano.
Wakiwa kituoni hapo, mama huyo alikiri kwamba mtoto huyo hakumzaa kama alivyoeleza awali bali alimuiba nyumbani kwao Mkuranga kwa nia ya kumdanganya mume wake kwamba amejifungua ili kulinda ndoa yake.
MAJIRANI WASIMULIA
Baadhi ya majirani wa eneo hilo walisema waliamua kutoa taarifa hizo ngazi ya serikali, baada ya kuwa na mashaka juu ya mwanamke huyo, hasa kutoeleweka vizuri mwenendo wake wakati wa ujauzito na anapojifungua.
Wakizungumza kwa masharti ya kutotajwa majina yao, walisema kwa miaka mingi, wanamshuhudia mwenzao huyo akiwa anabeba ujauzito na kujifungua watoto watatu katika hali ya kutatanisha, jambo lilowapa wasiwasi kwamba hazai kwa njia ya kawaida.
Walisema kila mara wanamuona anakuwa na hali ya ujauzito lakini inapofikia hatua ya mwisho, anatoweka na anaporejea anarudi akiwa na mtoto mwenye umri mkubwa.
Walisema jambo lingine lilowatia wasiwasi ni tabia ya mama huyo kutowanyonyesha watoto wake kama ilivyo kwa akinamama wengine, badala yake anatumia maziwa ya chupa mpaka mtoto anapokua.
"Unajua hali hii tumeshuhudia kwa mtoto wake wa kwanza, wa pili ambaye alifariki na huyu wa tatu, ndipo tukaona tujaribu kushirikiana na viongozi wetu tujue ukweli," alisema mwanamke mmoja.
Alisema safari hii mwanamke huyo kama kawaida yake alipokwenda nyumbani kwao akiwa mjamzito, alirejea akiwa na mtoto mchanga, lakini kilichowashangaza wengi ni pale mtoto huyo kuonekana ana umri mkubwa tofauti na maelezo ya mama yake.
MAMA MKWE: NILIAMINI ANA UJAUZITO
Akizungumzia suala hilo, Asha Limbanga, ambaye mtoto wake ndiye aliyemuoa tatu, alisema tangu aishi na mkwe wake kwa muda wa miezi sita, aliamini ujauzito alionao ni halisi.
Alisema, hajaweza kuona kwa uwazi tumbo la mkwe wake, lakini kutokana na maisha waliyokuwa wakiishi hakuwa na wasiwasi kwamba ipo siku ataletewa mtoto wa wizi.
Alisema, ilipofikia muda wa kijifunga, aliaga kwamba anakwenda nyumbani kwao na baada ya kukaa muda wa miezi miwili alirudi akiwa na mtoto huyo wa kiume.
Hata hivyo, Mkanilo hakupatikana kuzungumzia jambo hilo baada ya kuelezwa kwamba amekwenda Mkuranga kumpelekea chakula mke wake ambaye amewekwa mahabusu.
POLISI: TUNAMCHUNGUZA ZAIDI
Akizungumza kwa njia ya simu, Mkuu wa upelelezi Wilaya ya kipolisi ya Mbagala, aliyejitambulisha kwa jina la Afande Walelo, alikiri kutokea kwa tukio hilo na kwamba mtuhumiwa amekabidhiwa kwa wenzao wa Mkuranga kwa ajili ya kumfungulia kesi.
CHANZO: NIPASHE JUMAPILI
No comments:
Post a Comment