ANGALIA LIVE NEWS

Tuesday, September 23, 2014

NDOA YENYE MZOZO KILA SIKU MKE ANA KASORO - 2

Wiki iliyopita katika mada yetu tuliishia pale ambapo dada Mary alikuwa akizungumzia nafasi ya mke katika ndoa ambapo alisema ‘yeye kama yeye’ haamini kama anaweza kufanya jambo ambalo likamfanya mumewe achukue hatua ya kumpiga au kuzozana naye kwa vile anaijua nafasi yake katika ndoa.

Alisema: “Kujibizana na mume ndani ya nyumba ni kukosa heshima kwani mume ni kiongozi, huwezi kijibizana na kiongozi wako ndiyo maana Mungu alisema mke mwema hutoka kwake lakini hajasema popote kuhusu mume mwema anakotokea.”

NI KWELI WANAWAKE WAKO KATIKA MPANGO MWINGINE WA KUPINGA MAAGIZO YA MUNGU?
Wiki hii tunaendelea hapa. Kumekuwa na hoja mbalimbali katika mitandao ya kijamii na mada za wazi kwamba, eti wanawake wapo katika mpango mwingine wa kupinga maagizo ya Mungu.
Hoja hii inazungumzwa na wachambuzi wakirejea katika uumbaji kwamba, mwanamke ndiye wa kwanza kupinga agizo la Mungu (Eva au Hawa) pale bustanini kwa kula lile tunda kisha kumpa Adamu naye kula.

Wachambuzi wanayasema hayo wakiamini kuwa, wimbi la kutaka usawa kati ya mwanamke na mwanaume kwa sasa duniani kote ni njia ya ‘kishetani’ katika kuelekea kwenye utimilifu wa mpango huo.

Wachambuzi wanasema shabaha ‘njema’ lakini isiyo njema ya mataifa ya dunia kunia mpango wa usawa wa kijinsia ndiyo msukumo wa ndoa nyingi kufa au kuvunjika kwa kigezo cha kila mmoja ndani ya nyumba kushika madaraka na hivyo ndoa kukosa mwenye uelekezi kama ilivyokuwa kwa mababu.

KUNA USAWA KATI YA MWANAMKE NA MWANAUME?
Kusema ukweli hakuna usawa hata kidogo. Ndiyo maana kuna mwanaume na kuna mwanamke. Usawa ungekuwepo kama wote wangeitwa kwa jina moja! Mwanamke akiota ndevu anakuwa si wa kawaida kama vile mwanaume akiingia kwenye mzunguko wa mwezi. Uumbaji huu pekee unafuta usawa.

Ila kuna haki katika ya mwanamke na mwanaume. Haki za kimsingi kabisa katika kuishi, kula, kulala na katika kutoa mawazo ya ushauri, hata kuongoza nje ya ndoa. Kinyume cha hapo ni upotoshaji unaofanywa kwa kigezo cha maendeleo.

Hivi karibuni, ndani ya mjadala wa Bunge Malaam la Katiba mjini Dodoma, mbunge mmoja wa jimbo lililopo kwenye moja ya mikoa ya kanda ya ziwa alisema hakuna haja ya wanaume kuomba kujulikana au kuunda chama cha kutetea wanaume kwa vile wao walishapewa nafasi ya mbele tangu kuumbwa kwa ulimwengu huu.

Naongezea kwa kusema kuwa, ndiyo maana hata katika vita ua maafa mengine, jamii za kimataifa huweka wazi kwamba, wanaoathirika ni wanawake na watoto bila kutaja wanaume kwa vile ndilo kundi lisilojiweza.

WANAWAKE NA KAULI ZAO
Kumekuwa na kauli au matamko ya wanawake siku hizi wakisema; tukiwezeshwa tunaweza. Tamko hili linamaanisha kweli kuna tofauti kubwa kati ya jinsi hizi, lakini pia siku hizi kuna kauli nyingine; wanawake wanaweza bila kuwezeshwa! Ni sahihi lakini katika matamko hayo ndipo tofauti inapozidi kujulikana.

HITIMISHO

Nasisitiza kwamba, wanandoa kama kila mmoja atashika nafasi yake na kuitambua hakuna mzozo na mara zote mzozo hutokea pale mmoja anaposhindwa kutii kwa mwenzake ambaye ndiye anayemwongoza.

Tukutane wiki ijayo. GPL

1 comment:

Anonymous said...

Asante sana mtoa MADA hii, God bless you. Mimi naongeza hivi:- mke na mme wana haki za msingi na kiutu wote wako sawa sababu ni binadamu. Yaani mke au mume si wanyama wala mawe, hivyo wanathamani sawa mbele za Mungu.

Lakini ktk eneo la nafasi zao kama wanandoa head prifect na mwingine asistant prifect wa mwenzake na siyo makamu bali ni msaidizi. Na ndiyo maana Mungu aliwaagiza wanaume wote duniani waishi na wake zao kwa AKILI. Hili neno "akili" siyo ubongo, bali ni understanding and knowledge from God... II Timothy 2:7, thanks all.