Wananchi hawaoni kama wanao uwezo
wa kuishawishi Serikali
Wengi wanafuata njia zisizo rasmi za
kufanikisha mambo yao wenyewe
wa kuishawishi Serikali
Wengi wanafuata njia zisizo rasmi za
kufanikisha mambo yao wenyewe
2 Septemba, 2014, Dar es Salaam: Wananchi walio wengi (70%) wanaripoti kuwa sauti zao hazisikiki katika maamuzi ya Serikali. Pamoja na haya, wananchi saba kati ya kumi (71%) wanaripoti kuwa, kwa maoni yao, upigaji kura ndio njia pekee ya kuleta ushawishi kwa Serikali. Kimsingi, haya yanaonesha hisia zilizofanana – kwamba mbali na uchaguzi unaofanywa wakati wa kupiga kura – wananchi wengi hawana ushawishi kwenye maamuzi ya Serikali au shughuli zake. Wananchi pia wanaonekana kuwa na imani ndogo na taasisi rasmi au maafisa wa Serikali za mitaa katika kushughulikia masuala yao: wananchi tisa kati ya kumi wakiwa wameripoti kuwa hawajawahi kuzungumza au kuwasiliana na mbunge wao ndani ya kipindi cha mwaka mmoja na nusu uliopita. Pia, wananchi (47%) waliripoti kutowahi kuzungumza na mwenyekiti wao wa mtaa/kijiji ili kujadili masuala yanayowahusu. Ni mwananchi mmoja tu kati ya saba (16%) aliye mwanachama wa chama cha siasa.
Matokeo haya yametolewa na Twaweza kwenye muhtasari wa utafiti wenye jina la Wananchi wana uchu wa mabadiliko: Je, wananchi wanashiriki na wanaweza kuiwajibisha serikali? Muhtasari umetokana na takwimu ya Sauti za Wananchi, utafiti wa kwanza Afrika wenye uwakilishi wa kitaifa unaofanyika kwa njia ya simu za mkononi kote Tanzania Bara.
Licha ya mwingiliano mdogo ulio wazi kati ya wananchi na mifumo rasmi ya serikali, wananchi 6 kati ya 10 (58%) wanaripoti kuwa wamewahi kushuhudia wananchi wakipeleka malalamiko kwa viongozi ndani ya kipindi cha miezi 12 iliyopita. Malalamiko haya kwa kawaida huandaliwa ili kudai maboresho kwenye huduma za umma katika ngazi za mitaa. Masuala yaliyoonekana kulalamikiwa sana yalikuwa ni pamoja na utoro wa walimu na upatikanaji haba wa maji safi na salama.
Linapokuja suala la kuibua na kuzungumzia masuala yanayoihusu jamii, Sauti za Wananchi ilibaini kuwa watu walijitahidi kuzungumzia matatizo yaliyowakabili. Wananchi nane kati ya kumi (84%) walizungumzia masuala yao walipokutana katika makundi. Wananchi wengine watatu kati ya kumi walipiga simu kwenye vipindi vya redio 32% na 31% walilalamika kwa marafiki zao. Katika kuchukua hatua za kuungana pamoja na kusimamia jambo, wananchi walionekana kuwa wenye uwezo mdogo wa kususia mijadala. Ni 9% tu walioripoti kuwa wameshawahi kususia mijadala ndani ya kipindi cha mwaka uliopita, 8% walishiriki maandamano, 6% waliokataa kulipa kodi na waliotumia nguvu kufanikisha suala la kisiasa walikuwa (1%).
Kwa kawaida, vikundi vya kijamii hufanya kazi kubwa kusaidia maisha ya watu. Watanzania saba kati ya kumi waliripoti kuwa wamejiunga na moja ya makundi la kijamii. Makundi ya kidini pia yalionekana kuwa maarufu sana: mwananchi mmoja kati ya watatu (36%) alionekana kuwa amejiunga na kundi la kidini na wananchi wa tatu kati ya kumi (30%) walishiriki katika karibu nusu ya mikutano yote iliyoandaliwa na kundi lake. Mbali na makundi ya kidini, vyama vya kuweka na kukopa vilishika nafasi ya pili, ikiwa wananchi wawili kati ya kumi (22%) walikuwa ni wanachama wa vyama/vikundi hivyo. Wengi wao (20% ya wananchi) walihudhuria angalau nusu ya mikutano ya vikundi.
Mshikamano miongoni mwa jamii ulionekana kuwa mkubwa: karibu wananchi wote (98%) waliamini kuwa kama lingetokea tukio lisilotarajiwa, kwa mfano nyumba kuungua moto, jamii yao bila shaka ingekusanyika kusaidia. Kwa upande mwingine, wananchi walipoulizwa kama waliwaamini watu kwa ujumla, tisa kati ya kumi (87%) walionekana kuwa makini sana walipokuwa wakishirikiana na watu wengine.
Wananchi saba kati ya kumi (68%) wameripoti kuchangia moja kwa moja katika ujenzi au ukarabati wa vituo/majengo ya umma. Kati ya hawa, wananchi walio wengi (88%) walichangia fedha na (12%) waliobaki walichangia muda wao. Hii haikulingana na viwango vya ukusanyaji wa kodi, lakini ilionesha kuwa wananchi kwa njia moja au nyingine huchangia uendeshaji wa serikali. Hata hivyo, makusanyo hayaratibiwa vizuri kisheria, michango haikusanywi kwa haki wala kutumika kwa tija chanzo kikiwa uwazi mdogo na mfumo dhaifu wa kudhibitiana. Wananchi wanne kati ya kumi (39%) waliochangia vituo vya umma walisema walilazimishwa kufanya hivyo, na hii iliondoa imani ya wananchi.
Walipoulizwa, wananchi walihisi kuwa na uwezo wa kuzitegemea jitihada zao wenyewe ili kufanikisha mambo yao. Watanzania saba kati ya kumi (70%) waliitetea kauli hii na kusema kuwa wanao uwezo wa kujisimamia mambo yao wenyewe na kukabiliana na changamoto zinazowakabili. Pia wanaweza kutafuta ufumbuzi wa matatizo yao na kutimiza malengo yao wenyewe.
Rakesh Rajani, Mkuu wa Twaweza, alitoa maoni juu ya matokeo haya akisema. "Watanzania ni wanajamii hupeleka malalamiko yao kwa viongozi. Pia Watanzania wanaamini wana uwezo wa kukabiliana na vikwazo maishani mwao, lakini hawaamini wana uwezo wa kuishawishi Serikali. Wananchi wengi wanakwepa kujihusisha na vitendo vya kufanya jambo kwa hisia hasi au kali kama vile kukataa kulipa kodi, maandamano au matembezi ya kupinga jambo fulani. Lakini changamoto muhimu za utoaji huduma bado zipo kwenye sekta zote kuu. Kama serikali haitakuwa sikivu zaidi kwa hatua hizi, tunaweza kushudia wananchi wakiwa wakali zaidi katik siku zijazo."
No comments:
Post a Comment