Advertisements

Tuesday, September 23, 2014

TANZANIA YATAKA VIPAUMBELE VYA KITAIFA VIPEWE UMUHIMU

Mhe. Waziri Fatma Fereji kutoka Ofisi ya Makamu wa Kwanza wa Rais, Serikali ya Mapinduzi Zanzibar akizungumza kwa niaba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania wakati wa Kikao Maalum cha Baraza kuu la Umoja wa Mataifa kilichofanyika Jumatatu ambapo wakuu wa nchi na wawakilishi wa serikali kutoka nchi 193 walikutana kutathimini Mpango wa Utekelezaji walioupitisha miaka 20 iliyopita huko Cairo, Misri kuhusu uboreshaji wa maisha ya watu na masuala yahusuyo Idadi ya Watu. Mhe. Fereji ni sehemu ya Ujumbe wa Mhe. Rais Jakaya Mrisho Kikwete katika Mkutano wa 69 wa Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa.
Mhe. Waziri Fatma Fereji akiwa na Muwakilishi wa Kudumu wa Tanzania katika Umoja wa Mataifa, Balozi Tuvako Manongi na Naibu wake, Balozi Ramadhan Mwinyi wakati wa ufunguzi wa Kikao Maalum wa ICPD ambapo Waziri Fereji aliongoza ujumbe wa Tanzania katika Mkutano huo.
Kutoka kushoto ni Balozi Ramadhan Mwinyi, Waziri Fatma Fereji wakiwa na Mwakilishi kutoka Ofisi za UNFPA ambaye aliwahi pia kufanya kazi nchini Tanzania akimpongeza Waziri baada ya kutoa mchango wa Tanzania na kulia kabisa ni Dkt. Joyceline Kaganda

Na Mwandishi Maalum,  New York
Kikao Maalum  kilichowakutanisha  Viongozi wakuu wa  Nchi  na wawaskilishi  wa serikali kwa lengo la kutathmini hatua  ambazo zimechukiliwa na  serikali  katika kuboresha maisha ya watu na masuala ya idadi ya watu  kwa kipindi cha miaka 20 iliyopita kimefanyika siku ya Jumatatu hapa Umoja wa Mataifa.
Ujumbe wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania katika Mkutano huo, umeongozwa na  Mhe. Fatma Fereji  Waziri wa Nchi Ofisi ya Makamu wa Rais wa kwanza, Serikali ya Mapinduzi Zanzibar. Mhe. Fereji ni sehemu ya Ujumbe wa Mhe. Rais  Jakaya  Mrisho Kikwete katika Mkutano wa 69 wa Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa.
Mwaka  1994 nchi wanachama wa 179 wa Umoja wa Mataifa walikutana  katika Mkutano wa Kimataifa wa Idadi ya Watu na Maendeleo  ( ICPD)uliofanyika mjini Cairo ambapo walithibisha ahadi zao ambazo pamoja na mambo mengine zilikuwa za kuhakikisha kuwa  haki na ustawi wa watu unakuwa  msingi mkuu  katika suala zima la  maendeleo.

Mkutano huo  ( 1994)ulitoa Mpango wa Utekelezaji uliosisitiza umuhimu wa kulinda haki za binadamu, hasa haki za wanawake na vijana, kuwekeza katika afya na elimu, kuendeleza usawa wa kijinsia na kuwawezesha wanawake, pamoja na kuhakikisha upatikanaji wa huduma za afya na haki za uzazi.
Miaka 20 baadaye nchi wanachama ambazo sasa ni 193 wamekutana  katika Mkutano huo wa jumatatu na  ambao  ulikwenda hadi usiku  kutathimini mpango huo wa utekelezaji,  kupima matokeo yake , changamoto zake na kurejea ahadi walizotoa mwaka 1994.
Karibu  kila   mjumbe aliyepanda jukwaani kuzungumza  alielezea kile  ambacho serikali yake imetekeleza katika kuboresha  afya ya wanawake, watoto,   upatikanaji wa  huduma zote za msingi   zinazohusu  afya, elimu, uboreshwaji wa haki za msingi  za makundi mbalimbali ya   jamii, fursa  sawa za kijinsia na kupunguza idadi ya watu maskini.
Pamoja na kuelezea mafanikio  wajumbe hao pia walielezea changamoto mbalimbali zikiwamo za uhaba wa raslimali fedha, wataalamu wa kutosha,  kuendelea kuwapo kwa watu maskini, vifo  vitokanavyo na uzazi , vifo vya watoto wachanga, ndoa na mimba za utotoni na magonjwa kama vile malaria,  kifua kikuu, ukimwi na sasa Ebola.
Akizungumza kwa niba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Waziri Fatma Fereji, pamoja na kuelezea maeneo ambayo Tanzania imefanikiwa  kuyatekeleza vema katika kipindi hicho cha miaka 20 amesema, umaskini  bado ni tatizo  kubwa na ambalo  limeendelea kuchangia  pamoja na mambo mengine ndoa za utotoni.
Akayataja baadhi ya  maeneo ambayo Tanzania imefanya vizuri kuwa  katika Malengo ya Maendeleo ya Millenia  namba mbili, tatu  na nne   ambayo yamepata mafanikio ya kuridhisha  hata kabla   ya  mwaka 2015.
Akaeleza kuwa,  Tanzania bado inakabiliwa na  vifo vya watoto vinavyotokana na magonjwa yanayoweza kuzuilika kama vile,  malaria,  kuharisha na kifua kikuu.  Hata hivyo amesisitiza kuwa serikali  inaendelea na  juhudi mbalimbali  zinazolenga kuzitafutia ufumbuzi wa kudumu changamoto zilizobakia.
Akaitaka Jumuiya ya Kimataifa kuhakikisha kwamba  vipaumbele vya kitaifa katika eneo zima la  ustawi wa watu na maendeleo vinapewa umuhimu  na hususani katika kipindi  hiki ambacho jumuiya hiyo ya kimataifa imejikita katika maandalizi ya  malengo mapya ya maendeleo endelevu baada ya 2015.
Akasisitiza kuwa  ni vema  pia Jumuiya ya Kimataifa  ikaendelea kuyafanyia kazi maeneo ambayo bado  ama  yatakuwa hayajakamilika ifikiapo mwaka 2015 lakini vile vile  yasiachwe njiani bali yawe sehemu  ya  maeneo yatakayoshughulikwa  baada ya 2015.
Pamoja na  wakuu wa nchi na wawakilishi wa serikali kuzungumza katika mkutano huo,   Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa, Ban Ki Moon,  Rais wa Baraza Kuu la 69 la Umoja wa Mataifa,Bw. Sam Kutesa na  Mkurugenzi Mtendaji wa  Mfuko wa  Idadi ya Watu wa Umoja wa Mataifa  ( UNFPA) Babatunde Osotimehin nao walizungumza  mwanzoni mwa mkutano huo.

No comments: