Advertisements

Tuesday, September 23, 2014

Wasira: Urais si mama mkwe

Dodoma. Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais (Uhusiano na Uratibu), Steven Wasira amesema hana sababu ya kuona haya kutangaza kuutaka urais kwa kuwa urais si ukwe ila anasubiri wakati mwafaka.
Wasira alitoa kauli hiyo hivi karibuni alipokuwa akizungumza katika mahojiano maalumu na gazeti hili mjini Dodoma.
“Watakaposema ruksa, nitasema na wala kugombea urais si suala la kuonea haya. Ni kutoa huduma kwa Watanzania. Unalionea haya la nini? Kwani kugombea urais ni ukwe?” alihoji Wasira na kuendelea;
“Urais ni mama mkwe wako, hapana. Wakati ukifika nitasema tu. Na mradi kuna wananchi wanasemasema na wananitia moyo, ukifika wakati nitasema.”
Hata hivyo, waziri huyo ameonya kuwa endapo urais utachezewa kwa kuingia mtu ambaye si mwadilifu, biashara atakayoifanya Ikulu itakuwa ni kuuza haki za watu.
Alisema hawezi kufahamu nani atashinda katika kinyang’anyiro cha urais katika uchaguzi mkuu wa mwakani, lakini lazima rais awe mtu mwenye sifa za kushika nafasi hiyo.
“Mimi siwezi kufahamu ni nani ataongoza Tanzania, lakini ninaweza kusema sifa.” Alisema Wassira na kutaja sifa hizo kuwa ni pamoja na kuwa Mtanzania kwa sababu haiwezekani kuagiza mtu kutoka nje ya nchi kuja kuwania nafasi hiyo.
Aliongeza; “Rais pia anatakiwa kuwa mzalendo anayeipenda nchi yake na adhihirishe mapenzi yake, awe na uwezo wa kuongoza na pia ame-prove (amedhihirisha) uwezo wake huo wa kuongoza.”
Sifa nyingine ya urais, aliitaja kuwa ni mgombea kuwa mtu aliyewahi kuongoza taasisi nyingine na kuwaridhisha Watanzania kuwa aliongoza vizuri.
“Lakini pia rais lazima awe mwadilifu maana unalinda haki za watu. Baba wa Taifa aliwahi kusema Ikulu kuna biashara gani, lakini kuna biashara ya nguvu tu. Unaweza kuuza haki za hao watu,” alisema na kuongeza;
“Maana chakuuza pale hakuna. Mimi nafanya pale. Mimi naona watu wanamwagilia maua tu lakini kuna power (nguvu), kama wewe unapenda hela zaidi kuliko watu waliokuweka pale basi wewe utakuwa kazi yako ni kuuza haki zao.”
Alisema sifa hizo ni za msingi na wala si ngumu na kama mtu hana, hana tu.
Alipoulizwa katika sifa hizo anazozielewa yeye anajipimaje, alijibu, “Mimi siwezi kujipima. Nitajipimaje? Mimi nitapimwa na watu wengine”.
“Lakini kama wananitaja habari ya urais, wananisema na mimi nawashukuru wanaonisema. Kumbe na mimi ninaweza kupimwa na Watanzania,” alisema.
Waziri huyo ambaye pia ni mbunge wa Bunda alisema kwa sababu Watanzania wanasema na yeye ni miongoni mwa watu wenye nia ya kuwania urais, labda wanapima kwa sifa hizo.
Alisema chama chake kina utaratibu wa kufuata endapo mwanachama anataka kuwania nafasi ya uongozi.
Umri wa urais
Wasira mwenye umri wa miaka 69, alisema ujana au uzee siyo sifa za uongozi.
“Sifa zipo, akiwa anazo kijana anaongoza, akiwa nazo mzee anaongoza. Huwezi kusema ujana ni sifa. Mbona ni wengi. Tungekuwa hatuna tatizo la kupata rais maana wako wengi, asilimia 60 ni vijana, sasa tungepata shida gani kama ni ujana tu,” alisema.
Alisema uzee ni idadi ya miaka tu na wala si sifa ya uongozi kwa sababu hata hao wanaojiita vijana leo, kesho watakuwa wazee na wanaweza kuwa wazee bila ya kuwa na sifa za uongozi.
Rushwa katika uchaguzi
Wassira alisema rushwa ndani ya siasa ina madhara makubwa kwa sababu watapatikana watu waliochaguliwa ambao kimsingi hawana cha kuwafanyia wananchi zaidi ya kurudisha mali zao.
“Lakini unawachagua ili waende kupambana na rushwa, halafu wanachaguliwa kwa rushwa, sasa hii ni problem (ni tatizo), rushwa si kitu kizuri sana cha kujivunia,” alisema Wasira na kuongeza;
“Lakini unaisemaje rushwa, siipendi. Na ninachoweza kusema mimi sipendi hayo mambo. Mimi ningependa mtu anayechaguliwa achaguliwe na Watanzania hawa kwa imani.”
Alisema angependa Watanzania wachague rais na viongozi wengine kwa imani baada ya kuwapima sifa zao za uongozi na siyo kwa rushwa.
“Unaweza kuchaguliwa ubunge kwa rushwa lakini uchague mpaka rais kwa rushwa Mungu wangu mbona nchi itakuwa imekufa!”
Mwananchi

No comments: