Alfred Tibaigana alipokuwa kazini siku chache kabla ya kustaafu.
Katika mahojiano maalumu na gazeti hili nyumbani kwake Buganguzi wilayani Muleba, Kamishna Tibaigana alisema suala la maandamano halikumsumbua kwa kuwa alielewa kuwa sheria inayaruhusu, hivyo alichokuwa akifanya ni kuwaita viongozi wa vyama vinavyotaka kuandamana na kufanya nao makubaliano ya namna maandamano hayo yanavyopaswa yafanywe kabla ya kuyaruhusu.
“Pengine hiyo ndiyo sababu sikuwahi kushambuliwa kwa maneno ya kejeli au matusi na wanasiasa kwa kuwa sikuwahi kuzuia maandamano yao bila sababu na hata kama kulikuwa na sababu niliwaita na kuwaeleza na tulikubaliana.
“Kikubwa ni kujenga tabia ya kuwaita viongozi wa waandamanaji na kujadiliana nao, vinginevyo wanaweza pia hata kukufikisha mahakamani wakipinga kuzuiwa maandamano yao,” alisema Tibaigana ambaye alikumbana na sakata la kudai maandamano wakati akiwa Kamanda kwenye mikoa ya Tanga, Arusha na Dar es Salaam.
“Nilikuwa nawaita viongozi nakaa nao tunakubaliana. Hata kama ningeambiwa na kiongozi gani nisitoe kibali, kama hakuna sababu za kweli, nilikataa kwa kuwa kisheria mimi ndiye nawajibika kama vyama vikishtaki. Ili uzuie maandamano unapaswa kuwa na sababu za msingi ambazo ukiwaeleza waandamanaji wanakuelewa.”
Tibaigana anakumbuka jinsi CUF kilivyoandaa maandamano makubwa kushinikiza kuundwa kwa serikali ya mseto visiwani Zanzibar baada ya kutoridhishwa na matokeo ya Uchaguzi Mkuu mwaka 2005, lakini anasema kutokana na msimamo wake, haikuwa vigumu kwake kuruhusu jambo hilo.
“Wakati wa uongozi wangu CUF ilikuwa na nguvu sana, lakini mimi sikuwa na tatizo nao. Walipotaka kibali cha kuandamana niliwapa bila woga na tuliishi vizuri,” anaeleza Tibaigana.
Vuguvugu la maandamano pia lilitanda wakati wa maandalizi ya ziara ya Rais wa zamani wa Marekani, George Bush nchini kutokana na wasomi na baadhi ya wanaharakati kutaka kufanya maandamano kupinga vitendo vya taifa hilo kubwa dhidi ya raia wa Palestina na sehemu nyingine ambako wananchi wasio na hatia walikuwa wakiuawa.
“Nilichofanya ni kukutana nao na kuwaeleza njia ambazo wangeweza kutumia katika maandamano hayo na hali ilikuwa shwari,” alisema Kamanda Tibaigana.
Katika kipindi chake cha uongozi wa Polisi Dar es Salaam, Kamanda Tibaigana pia alikumbana na vurugu za kidini ambazo zilisababisha askari mmoja kupoteza maisha, lakini anasema kwa kushirikiana na wadau wengine, walijipanga na hali ikawa shwari.
Alivyomng’ang’ania Ditopile
Moja ya matukio makubwa wakati akiwa Kamanda wa Kanda ya Dar es Salaam ni tukio la mkuu wa zamani wa Mkoa wa Tabora, Ditopile kumuua dereva wa daladala baada ya kutokea kutoelewana barabarani, hali iliyolazimu sheria kufuata mkondo wake. Jeshi la Polisi lilitakiwa limkamate mkuu huyo na kumfikisha mahakamani.
Ditopile alituhumiwa kufanya mauaji hayo Novemba 5, 2006. Akidaiwa kumuua kwa kumpiga risasi dereva wa daladala, Hassan Mbonde. Alikamatwa na kufikishwa mahakamani, lakini alifariki dunia Aprili 20, 2008 wakati kesi yake ikiendelea.
Kamishna Tibaigana anasema tukio hilo lilimtia katika msukosuko mkubwa kutokana na kupata shinikizo kutoka kwa viongozi mbalimbali waliokuwa wakitaka asitekeleze wajibu wake wa kumkamata na kumfikisha mahakamani.
“Nilihojiwa na baadhi ya viongozi baada ya kuamuru Ditopile akamatwe, lakini nikasisitiza kuwa amevunja sheria kama walivyo wahalifu wengine,” alisema.
Kamanda Tibaigana alisema kuwa alifanya uchunguzi wa tukio hilo hatua kwa hatua, tangu Ditopile alipokuwa akifukuzana na gari hilo hadi alipompiga risasi dereva wake, akajiridhisha kuwa alivunja sheria.
“Baada ya hapo niliamuru Ditopile akamatwe kama watu wengine. Sasa tatizo ni kwamba watu wengine walichukulia suala hilo kisiasa na baadhi walikuwa wakinitisha kwamba nikimkamata nitafukuzwa kazi. Lakini mimi niliamini sheria iko palepale. Kwangu halikuwa tukio kubwa,” anasema.
Tibaigana ambaye ni mwanasheria kitaaluma, alisema katika masuala ya sheria, uwezo au hali ya mtuhumiwa haina nafasi katika uamuzi wa mashtaka yanayomkabili.
‘Niliulizwaulizwa na viongozi sababu ya kumkamata Ditopile na kumweka ndani. Niliwajibu ushahidi tulioukusanya unatosha kumpeleka mahakamani, hilo suala halikunishtua sana,’’ anasema Tibaigana.
Ziara ya Clinton
Kamanda Tibaigana pia anajivunia jinsi alivyoweza kuimarisha ulinzi wa Taifa wakati wa ziara ya marais wawili wa zamani wa Marekani, akiwa na majukumu ya kipolisi mkoani Arusha na Dar es Salaam.
Akiwa Kamanda wa Polisi wa Arusha, Tibaigana alihusika na ulinzi wakati wa ziara ya Rais wa zamani wa Marekani, Bill Clinton. Pia anasema alifanikiwa kuimarisha ulinzi wakati wa ziara ya Rais Bush nchini wakati akiwa Kamanda wa Kanda Maalumu ya Dar es Salaam.
Anasema ziara hizo za marais wa nchi hiyo, ziliwatia woga viongozi wa hapa nchini na wa Marekani.
Baada ya kuondoka salama nchini, Tibaigana anasema viongozi hao wa Marekani walimwandikia barua maalumu ya kumshukuru kutokana na kazi kubwa ya ulinzi waliyoiona, jambo ambalo alisema lilikuwa sifa kubwa kwa Taifa.
Matukio mengine makubwa
Tibaigana pia anajivunia kulipaisha jina la Jeshi la Polisi la Tanzania kimataifa baada ya kufanikiwa kumkamata mtuhumiwa wa ugaidi aliyekuwa akisakwa na Serikali ya Marekani.
Anasema mwaka 1995 wakati huo akiwa Mkuu wa Upelelezi wa Makosa ya Jinai wa Arusha, Marekani ilitangaza donge nono kwa mtu ambaye angefanikisha kukamatwa kwa mtuhumiwa huyo ambaye alidai kwamba alikuwa anatega mabomu na kulipua kumbi za starehe katika nchi mbalimbali duniani.
Anasema baada ya kupitia nyaraka mbalimbali zilizohusiana na taarifa za awali za mhalifu huyo, ilibainika kuwa alikuwa amejificha nchini na kuwa alipewa maelekezo na Inspekta Jenerali wa Polisi wakati huo, Omary Mahita kumtafuta mtuhumiwa huyo.
Alisema aliomba wiki moja, lakini akafanikiwa kumtia nguvuni ndani ya siku moja.
Anasema pamoja na kauli yake kutoaminika kwa viongozi wake, aliishangaza dunia kwa kumkamata mhalifu huyo ambaye hakumtaja jina ndani ya siku moja akiwa na dereva wake pamoja na msaidizi mmoja.
Baada ya kumkamata, Ubalozi wa Marekani ulijulishwa na baadaye nchi hiyo kutuma wapelelezi wake ambao walimtambua kuwa ndiye mhalifu aliyekuwa akitafutwa.
Anasema suala hilo liliweka jina la Jeshi la Polisi katika sura ya Kimataifa na nchi ikapata pongezi nyingi kutoka Marekani kwa kufanikisha kumkamata mhalifu wa kimataifa aliyekuwa anasakwa na dunia nzima na kwamba walipewa donge lililoahidiwa na wakagawana kwa utaratibu waliojiwekea.
“Kwa wakati huu huyo mhalifu angeweza kufananishwa na (kiongozi wa kundi la Al Qaeda, marehemu) Osama bin Laden kwa jinsi alivyokuwa anasakwa na dunia.”
Kamanda Tibaigana alibainisha kuwa kukamatwa kwa mtuhumiwa huyo kuliondoa hisia zilizokuwa zimeanza kujengeka kuwa nchi imeshindwa kumtafuta na kumkamata. Anasema taarifa za mitandao ya Marekani zilionyesha kuwa mtuhumiwa huyo alikuwa amejificha hapa nchini.
Uhalifu wa mtandao
Akizungumzia tatizo la uhalifu wa kutumia mtandao ulioanza kushika kasi nchini, Kamanda Tibaigana anasema wakati wa uongozi wake suala hilo halikuwa kubwa na kuwa polisi haina budi kubadilika ili kwenda na mazingira ya sasa.
Anasema Serikali inawapeleka askari wake nje ya nchi kupata mafunzo mbalimbali ya kukabiliana na uhalifu, lakini hilo pekee halitasaidia katika utendaji kwa kuwa hakuna vifaa vya kisasa vinavyohitajika kwa kazi hiyo.
“Mimi nimekwenda kozi mbalimbali dunia nzima, lakini ukirudi hapa nyumbani vifaa vya kufaya kazi hiyo havipo kwa sababu ya ufinyu wa bajeti. Matokeo yake tunabaki kujivunia takwimu kuwa tuna askari waliopata mafunzo nje ya nchi,” anasema Tibaigana.
Anasema hata baadhi ya vifaa huchukua muda mrefu kununuliwa na hivyo huwakuta wale waliopata mafunzo ya jinsi ya kuvitumia wakiwa tayari wamestaafu kazi, hali inayofanya kukosekana kwa wataalamu wa kuvitumia.
Anaishauri Serikali iache kusuasua katika ununuzi wa vifaa vya kisasa kuwezesha utendaji wa ufanisi wa jeshi hilo katika kukabiliana na uhalifu.
Polisi kushirikiana na wahalifu
Pia alizungumzia tuhuma za polisi kushirikiana na wahalifu. Katika hilo, Kamanda Tibaigana anasema tuhuma hizo ni kweli akisema tatizo hilo ni sawa na msafara wa mamba kujumuisha kenge pia.
Alisema polisi ni sehemu ya jamii na kwamba wapo askari wachache wanaochafua taswira ya jeshi hilo, lakini suala hilo linakuzwa sana.
“Matatizo hayo yapo tangu kuanzishwa kwa Jeshi la Polisi na viongozi wengi wa jeshi wanayashughulikia,” alisema.
Alisema polisi wengi wanaotuhumiwa kuhusika katika uhalifu, hufikishwa kwenye mahakama za kijeshi ambako uamuzi hufanyika haraka, lakini kumekuwapo na malalamiko kutoka kwa baadhi ya askari kuwa kupelekwa kwenye mahakama hizo ni kukiuka haki za binadamu.
Kuhusu ubunge
Tibaigana aligombea ubunge wa Jimbo la Muleba Kusini baada ya kustaafu, lakini akashindwa katika kura za maoni ndani ya CCM na Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi, Profesa Anna Tibaijuka, lakini hana mpango wa kurudi tena ulingoni kugombea nafasi hiyo.
“Wakati naomba kura ili niteuliwe na chama changu cha CCM kugombea ubunge, niliwaambia wananchi kuwa wanipe miaka mitano tu. Sasa, kwa kuwa muda huo umeshapita, nawaachia wengine,” anasema Tibaigana.
Alisema kuwa kama angetaka angeweza kugombea kama mgomea binafsi bila kupitia chama chochote kama suala hilo lingepitishwa katika Katiba Mpya, lakini ameamua kupumzika.
Mchakato wa Katiba Mpya
Kuhusu mchakato wa Katiba Mpya, Tibaigana anasema awali, alikuwa muumini wa Muungano wenye wa serikali tatu, lakini amebadilisha msimamo wake baada ya kuridhika na hoja za wanaotetea muundo wa serikali mbili.
Mwananchi
No comments:
Post a Comment