Advertisements

Sunday, September 21, 2014

Tunu: Pinda kutajwa urais kulinishtua

Dodoma. Mke wa Waziri Mkuu, Mizengo Pinda, mama Tunu Pinda amesema kuwa alishtuka kusikia habari kwamba mumewe ametangaza nia ya kuwania urais mwaka 2015.
Magazeti mbalimbali (siyo Mwananchi), yaliandika habari zilizodai kuwa Pinda ametangaza nia kutaka kuwania urais mwaka 2015. Hata hivyo, katika mahojiano na gazeti hili juma lililopita, Waziri Mkuu Pinda alisema kuwa kutajwa kutaka kuwania nafasi hiyo ni jambo jema na kutangaza nia pia ni jambo jema.
Lakini katika mahojiano na gazeti hili yaliyofanyika nyumbani kwake mjini Dodoma, Tunu Pinda alisema:
“…Niliposikia kwanza nilishtuka kwa sababu bahati mbaya hatukuwa pamoja nikajiuliza imekuwaje. Ukweli nilishtuka na alipokuja nikamuuliza, naye akasema; “mimi sijatangaza, wala sijaita vyombo vya habari au labda kuzungumza kwamba nautaka urais, lakini muda utakapofika nitasema.”
Tunu ambaye mwezi uliopita aliteuliwa kuwa Balozi wa Amani Duniani na mkutano wa dunia (World Summit 2014), ulioandaliwa na Taasisi ya Universal Peace Federation(UPF), nchini Korea Kusini aliongeza:
“Kwa hiyo kama walivyosema na iwe hivyo kama Bwana Mungu aishivyo, nasema amina. Kwa sababu muda bado haujafika, utakapofika tutajua.”
Uwaziri Mkuu wa Pinda
Akizungumzia nafasi ya uwaziri mkuu kwa Pinda aliyodumu nayo tangu mwaka 2008, mke huyo wa Waziri Mkuu alisema, mumewe ameweza kudumu na kuwa salama hadi sasa kwa nguvu na uwezo wa Mungu.
“Yaani unamwona huyu bwana (Pinda), mpaka leo kwenye nafasi hii ni kwa ajili ya nguvu na neema za Mungu. Kwa akili za kibinadamu huwezi. Bila kumtarajia Mungu afanye, hutaweza. Kwa hiyo tuna ratiba ya kusali kifamilia kila siku na kushiriki kusali kanisani na kujitolea kama watu wengine,” alisema Tunu.
Majukumu yake kama mama
Akizungumzia majukumu yake kama mama awapo nyumbani, mke huyo wa Waziri Mkuu alieleza kuwa maisha yake ni ya kawaida kama mama mwingine wa Kitanzania aliye na majukumu ya kifamilia.
“Maisha yangu ni ya kawaida sana si kwamba kwa nafasi niliyonayo niishi maisha ya ajabu, hapana. Kinachoongezeka kwangu ni kule kuwa mke wa kiongozi, labda na taratibu zinazoendana na nafasi hiyo,”alisema Tunu.
Katiba Mpya
Kuhusu mchakato wa Katiba na muundo wa Serikali, alisema:
“Mimi mtazamo wangu haupo hata kwenye mapendekezo ya Rasimu. Mtazamo wangu kama Tunu nilitamani sana iwe Serikali moja. Kwa kuwa moja haipo, hata kwenye rasimu, tuendelee hivi tulivyo sasa hivi.
Tuendelee kuishi kindugu, yale matatizo yaliyo kwenye Muungano yaendelee kurekebishwa. Tuhakikishe tunaendelea kudumisha undugu wetu kwa miaka mingine hamsini ijayo.”
Balozi wa Amani Duniani
Agosti 12,2014 Mama Pinda alitunukiwa tuzo na kuteuliwa kuwa Balozi wa Amani Duniani katika mkutano uliojadili amani, usalama na maendeleo ya dunia ulioandaliwa na UPF, inayotoa ushauri kwenye Baraza la Umoja wa Mataifa linaloshughulikia Uchumi na Jamii ambapo pia alikuwa mmoja watoa mada.
Akinukuu alichosema katika mkutano huo uliokuwa wa siku tano na kujumuisha wajumbe nchi 68 duniani kote na aliwasilisha mada iliyohusu amani, maendeleo kwa binadamu barani Afrika alisema:
“Naiomba jamii ya kimataifa duniani tusimamie amani na usalama, kinyume na hapo ni kuleta machafuko. Wanawake hatupendi vita, wala machafuko.
“Nawasihi tuendeleze maono ua Muumba wetu, Tuweke utu mbele kwa kuwajali wengine, tuache kutanguliza masilahi binafsi,” alisema mama Pinda na kuongeza:
“Nilitaka washiriki wote tusimame kwenye nafasi zetu kama baba, mama, kaka na dada kuhakikisha dunia inakuwa mahali pazuri pa kuishi.”
Alisema kuwa katika mkutano huo mwasilishaji kutoka Afrika alikuwa pekee yake ambapo alizungumzia usalama na amani Afrika Mashariki, ukanda wa Sadc, Bara la Afrika na dunia.
“Kama hakuna amani, hakuna maendeleo na hamwezi kupanga maendeleo kwa sababu muda wote hakuna uhakika na usalama wenu. Kwa hiyo usalama na amani ni vitu muhimu kwa mustakabali wa maendeleo ya nchi na binadamu. Binadamu anastahili vitu hivyo ndipo ataweza kufikiria maendeleo.
Binadamu ana haki ya kuishi kwa amani na wanaothirika amani inapokosekana ni kinamama, watoto na wazee wao hukosa uwezo wa kukimbia. Natamani dunia izungukwe na amani ili tuweze kuleta maendeleo kwani Mungu hakutuumba ili tuteseke,”alisema.
Mwananchi

No comments: