Kamishna Mkuu wa TRA, Rished Bade
Mgomo wa wafanyabiashara wa maduka umetikisa katika maeneo ya Soko Kuu la Kariakoo, jijini Dar es Salaam kutokana na wafanyabiashara kutoka ndani na nje ya nchi kushindwa kununua bidhaa mbalimbali.
Kufungwa kwa maduka hayo jana kulishuhudiwa pia katika maeneo ya Mbagala, Tandika na katikati ya jiji eneo la Posta.
Hali hiyo ilishuhudiwa majira ya saa 4:30 asubuhi wakati maduka ya eneo hilo kwa asilimia kubwa yalikuwa yamefungwa katika mitaa ya Msimbazi, Kongo, Uhuru na maeneo ya jirani, huku watu mbalimbali ambao ni wanunuzi na wamiliki wa maduka wakiwa wamejikusanya katika vikundi na kujadili suala hilo.
Baadhi ya wamiliki wa maduka, ambao hawakuwa tayari kutaja majina yao walipozungumza na NIPASHE, walisema mgomo huo umetokana na Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) kwa kushirikiana na askari wa Jeshi la Polisi kuwakamata na kuwafungia maduka baadhi ya wafanyabiashara wenzao kutokana na kutokuwa na mashine za kieletroniki za kutolea risiti (EFD’s) za TRA.
Walisema hatua ya kuwafungia baadhi ya wenzao wanaomiliki maduka ilisababisha umoja wa wafanyabiashara kuchukua uamuzi wa kufunga maduka yao jana kwa kuwaunga mkono na kushinikiza wenzao,ambao wanashikiliwa kuachiwa huru na kisha kufunguliwa maduka yao.
Said Hassan, ambaye alifika katika eneo la Kariakoo kwa ajili ya kununua vitu mbalimbali na kisha kwenda kuviuza, alisema hali hiyo imekwamisha biashara zake kwa jana.
“Hii hali ya mgomo imetuathiri sisi wafanyabiashara wadogo au wamachinga, kwani tunakuja kununua kila siku bidhaa ili na sisi tukawauzie wateja wetu. Na hapa Kariakoo wanapategemea hata wafanyabiashara kutoka nje ya nchi, kama Malawi, Zambia, Zimbabwe na Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo,” alisema Hassan.
Naye Selestine Shayo, ambaye ni mfanyabiashara mdogo, alisema mgomo huo unatokana na kutokuwa na mashine za EFD’s, ambao haumhusu, kwani wanaotumia mashine hizo ni wafanyabiashara wa maduka makubwa.
“Wanapofunga maduka hawa wafanyabiashara wakubwa kwangu mimi mfanyabiashara mdogo napata faida kwa kuwa nauza sasa, kwani katika siku za kawaida kama hakuna mgomo, sisi tunafukuzwa na wafanyabiashara wakubwa, ” alisema Shayo.
Muuzaji wa duka dogo la ‘Supermarket’, ambalo linatumia mashine hizo katika eneo la Kariakoo, ambaye hakuwa tayari kutaja jina lake, alisema hawajafunga duka lao kutokana na kuwa na mashine katika duka lao.
“Sisi hatuwezi kushiriki mgomo huo, kwani mashine ipo. Tunaendelea na biashara kama kawaida,” alisema.
Akizungumza na NIPASHE, Katibu wa Soko Kuu la Mbagala, Frank Mapuli, alisema soko hilo kwa siku ya jana halikuwa na wafanyabiashara wakubwa, ambao walifungua maduka yao kutokana na wengi wao kutokuwa na mashine hizo.
“Mgomo huu umewaathiri wafanyabiashara wadogo, ambao ni wanunuzi wa rejareja katika maduka makubwa, hivyo wameshindwa kununua bidhaa katika biashara zao. Wao ni wachuuzi, ” alisema Mapuli.
Alisema Soko la Mbagala lina wafanyabiashara zaidi ya 1,000 kutoka maeneo tofouti ndani na nje ya mkoa wa Dar es Salaam, ambao hufanya shughuli zao katika soko hilo.
Msemaji wa Jumuiya ya Wafanyabiashara nchini (JWT), Johnson Minja, alipotafutwa kwa njia ya simu na NIPASHE ili kuzungumzia mgomo huo, alijibu: “Mimi sikuwapo. Nimerudi kutoka safarini nimepata taarifa za maduka kufungwa. Lakini kuna baadhi ya viongozi wemeenda kukutana na Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam kuzungumzia suala hili.”
Wafanyabiashara Kariakoo waligoma kwa kufunga maduka yao Novemba, mwaka jana kwa madai ya kulazimishwa kutumia mashine hizo.
Waligoma tena katika maeneo mbalimbali katika mikoa ya Arusha, Ruvuma, Mbeya, Mwanza, Dar es Salaam na Dodoma kwa kuishinikiza serikali kuondoa mashine hizo.
MOROGORO
Nao baadhi ya wafanyabiashara wa kati mjini Morogoro jana walifunga maduka yao kwa hofu ya kufungiwa na TRA na kutozwa mamilioni ya shilingi kama faini kutokana na kutokuwa na mashine hizo.
Walidai hatua hizo zimeanza kuchukuliwa jijini Dar es Salaam, huku mazungumzo kati ya TRA na wafanyabiashara yakiwa hayajakamilika.
NIPASHE ilipita maeneo mbalimbali ya mji wa Morogoro na kushuhudia maduka mengi yakiwa yamefungwa, huku wafanyabiashara wakikwepa kuzungumzia hali hiyo na wengine wakionekana mbele ya maeneo yao ya biashara bila kufanya shughuli zozote.
Mwenyekiti wa Wafanyabiashara wa Kati mjini Morogoro, Ali Mamba, alisema mgomo huo hauhusiani na matumizi ya mashine hizo, bali mfumo wa ulipaji wa kodi kwa wafanyabiashara.
Alisema wafanyabiashara pamoja na kushawishiwa kuachana na mgomo, walidai kuchukua uamuzi huo kwa kutowaamini viongozi wao katika mazungumzo yaliyokuwa yakiendelea baina yao na TRA, baada ya kushuhudia mamlaka hiyo ikianza kuwafungia wafanyabiashara jijini Dar es Salaam, ikiwa ni pamoja na kuwapa masharti magumu baada ya kufungiwa.
Alitaja masharti yaliyowatisha wafanyabiashara kuwa ni pamoja na kutakiwa kulipa faini ya Sh. milioni tatu, kununua mashine kwa 680,000 ya kufuli linalotumika kufungia eneo linalofungiwa.
Wakizungumzia mgomo huo, wafanyabiashara wanaosambaza bidhaa katika maduka mbalimbali, walieleza kuathiriwa na mgomo huo.
Walisema pamoja na kutumia mashine hizo, bado mtandao wake ni wa tabu, hivyo TRA badala ya kutaka wafanyabiashara watumie mashine ni vyema ikaangalia pia na changamoto zilizopo kwenye mfumo huo kabla ya kuhimiza matumizi.
“Kama hivi sisi tuna mashine, lakini hatufanyi biashara, kwa sababu wafanyabiashara wakifunga na sisi hatuna pa kuuzia, inabidi tuzunguke tu,” alisema Onesmo Christian aliyekuwa akisambaza maji ya jumla.
Meneja wa TRA mkoa wa Morogoro, Kilomba Kanse, alikataa kuzungumzia hali hiyo kwa madai tayari Kamishna Mkuu wa Mamlaka hiyo, Risherd Bade, alishazungumza na vyombo vya habari kuhusiana na mashine hizo.
Akinukuliwa na vyombo vya habari, Bade mbali na kuzungumzia umuhimu wa uanzishwaji wa mashine za EFD na kuwahimiza wananchi kudai stakabadhi sahihi kwa kiwango cha fedha wanachotoa wanaponunua bidhaa.
Aliwaonya wanaohamasisha kutishia au kutumia njia yoyote kuwarubuni wengine wasitumie mashine hizo ama kufunga biashara zao waache mara moja, vinginevyo sheria itachukua mkondo wake.
Alisema nia ya uanzishwaji wa mashine hizo ni kurahisisha utunzaji wa kumbukumbu za kibiashara na hivyo kupunguza au kuondoa kabisa misuguano wakati wa ukokotoaji wa kodi na kuleta uwazi kwa mfanyabiashara bila kuonewa au mapato ya serikali kupotea hatimaye kuleta maendeleo ya taifa.
TRA WALONGA
TRA imesema haiko tayari kuyumbishwa na wafanyabiashara wasiopenda kutumia mashine hizo, bali wanaendelea na zoezi la uhakiki wa matumizi yake sahihi.
Akizungumza na NIPASHE jijini Dar es Salaam jana, Mkurugenzi wa Huduma ya Kodi na Elimu wa TRA, Richard Kayombo, alisema sheria ya kufanya uhakiki ilitungwa na Bunge, hivyo ni wajibu wao kutekeleza.
Alisema baada ya Bunge kupitisha sheria hiyo, wajibu wa TRA ni kutekeleza, huku Wizara ya Fedha na Jeshi la Polisi likisimamia utakelezaji huo kisheria.
Alisema ikiwa wafanyabiashara watafunga maduka bila kushawishi wengine, hilo litawasaidia TRA kuendesha zoezi la uhakiki kirahisi kwa kuwa tayari watakuwa wamejitoa kufanya biashara.
“Hatuwezi kugombana na mtu aliyeamua kufunga biashara yake. Lakini kwa wale watakaohamasisha, kutishia au kushawishi wengi wafunge biashara zao, wanatakiwa kuacha tabia hiyo, vinginevyo hatua za kisheria zitachukuliwa,” alisema.
Alisema wafanyabiashara walianza kwa kulalamika elimu itolewe ya matumizi ya EFD, baadaye wakasema mashine hizo hazitunzi umeme, vyote hivyo vilikuwa ni visingizio vya kugoma kuzitumia.
Kayombo, alisema pia walilalamikia mtandao kuwa chini wakati wa kutuma ripoti zao za mauzo na mwisho walisema mfumo wa kodi uangaliwe upya na kusema kubadilisha malalamiko kila wakati ni kukosa hoja ya kusimamia.
Alisema wakati wote TRA imekuwa ikishirikiana na wafanyabiashara kutoa taarifa na kufanya maboresho, ikiwamo kutoa elimu ya matumizi ya biashara na kuongeza saa 72 ya kutuma taarifa zao.
Kayombo alisema wanashangaa kuona wafanyabiashara wakiendelea kulalamikia mashine hizo ili wasilipe kodi kutokana na mapato yao, serikali ilinunua mashine hizo ili kuleta uwazi na kurahisisha ukusanyaji wa mapato yake.
Ufuatiliaji uliofanywa na TRA hivi karibuni umebaini baadhi ya wafanyabiashara walengwa hawajanunua mashine na wengine wamenunua lakini hawazitumii.
Imeandikwa na Christina Mwakangale; Efracia Massawe; Enles Mbegalo; Leonce Zimbandu (Dar) na Idda Mushi (Morogoro).
CHANZO: NIPASHE
1 comment:
Uzalendo(patriotism) uko wapi kwa hawa wabongo kama hata kodi hawataki kulipa! au uzalendo unaoongelewa ni tofauti na ule ambao diaspora walionekana hawana?
Post a Comment