ANGALIA LIVE NEWS

Sunday, September 28, 2014

ZLS: Katiba ya wananchi imeporwa na watawala

Zanzibar. Rais wa Chama cha Wanasheria Zanzibar (ZLS), Awadh Ali Said amesema Rasimu ya Katiba inayopendekezwa na Bunge Maalumu la Katiba imepora mamlaka ya wananchi kutokana na kitendo cha kubadilisha vifungu muhimu ikiwamo mfumo wa Muungano wa Tanganyika na Zanzibar.
Akizungumza jana na gazeti hili mjini Zanzibar, Awadh alisema kitendo cha kubadilisha mfumo wa Muungano wa serikali tatu kama ilivyokuwa imependekezwa na rasimu ya awali ya Jaji Joseph Warioba ni kuvunja msingi wa nyumbani na kinakwenda kinyume na maoni ya wananchi.
Alisema kwamba mfumo wa Muungano wa Serikali mbili na marekebisho yake yaliyofanyika umekuwepo katika miaka ya nyuma na katika kipindi cha miaka 50, lakini umeshindwa kuondoa kero za Muungano.
“Bahati mbaya mchakato wa katiba umeporwa kutoka kwa wananchi na kumilikiwa na watawala kinyume na matakwa ya wananchi, hatuwezi kupata katiba bora kwa kuweka masilahi binafsi ya vyama.” alisema Awadh.
Awadh ambaye alikuwa Kamishna wa Tume ya Mabadiliko ya Katiba alisema kitendo cha kubadilisha vifungu vilivyokuwa vimependekezwa katika Katiba ya awali ni sawa na kuondoa maoni ya wananchi kwa vile rasimu ya Warioba ilitokana na maoni ya wananchi wa pande mbili za Muungano kabla kuwasilishwa bungeni Febuari mwaka huu.
Aidha, alisema kwamba wabunge wa Bunge la Katiba kupitia vyama vya siasa wamezingatia masilahi yao binafsi badala ya masilahi ya Taifa na wananchi wake, ndiyo maana wamefuta vifungu muhimu kama kuwapo kwa ukomo wa kugombea ubunge, kiwango maalumu cha taaluma, wananchi kuwa na mamlaka ya kikatiba ya kumwondoa mbunge asiyewajibika kwa madhumuni ya kuimarisha uwajibikaji na misingi ya utawala bora nchini.
“Jambo la msingi Bunge la Katiba livunjwe, liundwe bunge jipya lisiloshirikisha wabunge wanaotokana na vyama vya siasa ili tupate katiba bora na yenye manufaa kwa wananchi wa pande mbili za Muungano wetu,” alisema Awadh.
Akifafanua, alisema hatua ya wabunge kuingiza mambo ya bahari na ardhi katika orodha ya mambo ya Muungano kutaibua kero nyingine mpya, kwa sababu haiwezekani kuondoa mambo ya mafuta na gesi katika orodha ya mambo ya Muungano wakati rasilimali hizo zinapatikana chini ya ardhi katika mwambao wa bahari.
Hata hivyo, upande wake Mwanasheria Mkuu wa zamani, Hamid Mbwezeleni alisema kwamba rasimu ya mwisho ya Katiba ya Jamhuri ya Muungano siyo mbaya baada ya kufanyiwa marekebisho mbalimbali na kutaka wabunge wa Bunge la Katiba kupewa nafasi ya kukamilisha majukumu yao.
Alisema kwamba, iliyokuwa Tume ya Mabadiliko ya Katiba wakati ikitekeleza majukumu yake hakuna mhimili ambao uliingilia majukumu yake na kushangazwa na kitendo cha aliyekuwa Mwenyekiti wa Tume hiyo kugeuka msemaji mkuu wa Watanzania.
MWANANCHI

No comments: