ANGALIA LIVE NEWS
Saturday, October 4, 2014
ABUNUWASI NA HUKUMU YA KIJANA
Hapo zamani za kale katika nchi moja Afrika, paliishi mama mmoja ambaye alikuwa mjane. Muda mfupi tu kabla ya mumewe kufariki walijaliwa mtoto mmoja wa kiume ambaye huyo mama alimlea kwa shida na taabu nyingi. Hata hivyo mama na mtoto wake walipendana ipasavyo. Hapo katika kijiji chao kulikuwa pia na tajiri mmoja ambaye alikuwa bahili na katili kweli. Yule kijana maskini alikwenda kwa tajiri kuomba kazi. Tajiri alimwambia kwamba alikuwa na kazi kwake na angemlipa vizuri sana.
Kijana alifurahi kusikia hivyo na akamwuliza tajiri kwa furaha.
"Kazi gani hiyo utanipa mheshimiwa? Mimi nitaifanya vizuri mpaka hata wewe utafurahia."
Tajiri akamwambia, "Ukilala katika maji baridi sana usiku mzima, nitakupa shillingi laki moja." Ulikuwa wakati wa baridi sana kwamba maji ya ziwa karibu yagandamane kuwa theluji kwa baridi.
Lo! Kijana hakufikiria angeweza kuwa na pesa nyingi hivyo katika maisha yake. Tamaa ya kutaka kumsaidia mama yake ambaye wakati huo alikuwa mgonjwa na mzee, ilikuwa kubwa sana kwa hivyo akakubali bila kufikiria. Mama aliposikia habari hizo karibu azimie kwa wasiwasi na huzuni.
"Mwanangu sitaki uhatarishe maisha yako kwa sababu ya pesa. Mungu yuko nasi na hajatuacha hata siku moja tukalala njaa. Atazidi kufanya hivyo hivyo. Je, ukifa nitabaki na nani mwanangu? Mimi mzee sasa wala sijiwezi!" Kijana alimjibu,
"Mama usiwe na wasiwasi wala woga wo wote! Nitaweza kabisa kulala kwenye maji baridi mpaka asubuhi na siwezi kufa" Mama bado alizidi kubisha, lakini kijana alisisitiza kabisa kwamba lazima afanye hiyo kazi ambayo itawaondolea shida zote za kifedha, kama alivyoona yeye.
Kwa huruma ya mama na wasiwasi juu ya mtoto wake, alikwenda karibu na ziwa pale alimotumbukizwa mtoto wake kwenye maji baridi kama barafu, Alimwona kichwa tu kimelea juu ya maji. Mama aliwasha moto mkubwa karibu na ziwa lile kwenye ufa, ili aweze kumwangazia angalao mwangaza na kumwona. Usiku kucha mama mtu hakufunguka jicho hata dakika moja. Alimlilia Mungu amtunze mwanae asife kwa baridi.
Kwa huruma ya Mwenyezi Mungu, kijana alistahimili baridi yote ile mpaka alfajiri siku ya pili.
Alikwenda kwa tajiri kupokea malipo yake lakini tajiri akamwambia.
"Hupati hata ndururu ng'o!"
"Kijana alishangaa akamwuliza, "Kwa nini mheshimiwa? Uliniahidi kunipa shillingi laki moja nikilala katika maji yabaridi usiku mzima. Usiku mzima nilikuwa ndani ya maji hayo na shahidi wako wameshuhudia na pia mama yangu."
"Ehe, hapo sasa umenena. Mamako aliyekuwashia moto ili upate joto usiku mzima. Hayo ndiyo yalikuwa maagano yetu? Sikumbuki tukiagana kwamba mama yako atakuja na kuwasha moto mkubwa wa kukupa joto kisha unidanganye umelala kwenye maji ya baridi. Unaniona mimi bwege sio? Nenda zako, sikulipi cho chote."
Kijana alikasirika kweli na akamweleza jirani yake mzee Abunuasi. Kama kuna watu Abunuasi aliowazira, ni matajiri waliopenda kuwaangamiza maskini badala ya kuwasaidia. Abunuasi akamwambia kijana asiwe na wasiwasi kwamba rafiki yake Sultan atamsaidia. Akamwambia aende kwake na kumweleza habari zote. Kijana alifuata ushauri wa Abunuasi, lakini Sultani aliposikia kisa chote kutoka pande zote mbili aliamua kwamba kijana asipate malipo kamwe. Abunuasi alishangaa na uamuzi huo wa Sultani mzima wa nchi akamwambia kijana bado asiwe na wasiwasi atapata hela zake. Kijana alimwahidi Abunuasi kumpa shillingi elfu ishirini akimsaidia.
Abunuasi aliandaa karamu kubwa na akawaalika watu wengi pamoja na Sultani na yule tajiri pia. Alichinja mbuzi akatayarisha vitu vyote, mchele, mboga zikakatwakatwa na kuwekwa kando. Moto mkubwa uliwahswa na kila kitu kikawekwa kando ya moto, nyama ya mbuzi katika sufuria pamoja na vitunguu na viungo. Mboga, mchele, zote zikawekwa kando ya moto na Abunuasi akaenda kuwakaribisha wageni wake. Wageni walingojea chakula siku kutwa hawakuona hata maji ya kunywa. Abunuasi aliwaambia kwamba chakula bado kinapikwa jikoni na wala hakijawa tayari. Itabidi wangojee. Mwisho walikasirika na kuingia wote katika jiko. Walikuta moto unawaka vizuri na kando ya huo moto chakula chote walichokuwa wakikingojea kiko kando ya moto huo mkubwa. Sultani akiwa mmoja wa wale waliokuwa na njaa alisema.
"Abunuasi wewe akili zako zinafanya kazi? Hiki chakula ulisema kinapikwa? Mbona moto uko kando na chakula kando? Hakitaiva hata baada ya miaka elfu. Wewe mwehu kweli kama watu wanavyokusema. Unatulisha njaa siku nzima?"
"Usiwe na wasiwasi Sultan, chakula kitaiva tu! Subira huvuta kheri mheshimiwa."
"Acha upuzi na ubwege. Hiki chakula hakitaiva kamwe. Hakipati hata joto la moto huo hata kama mkali kiasi gani"
"Kwa nini kisiive mheshimiwa? Wewe uliamua kesi ya kijana maskini asilipwe na huyu tajiri nduli alipomlazimisha kulala kwenye maji baridi usiku mzima. Kwa njaa na umaskini wake, alikubali. Naye mama yake kwa upendo wa mwanae, alilala kando ya ziwa akimumlikia mwanae ili apate kumwona tu kama angali hai. Wewe uliamua asilipwe kwa sababu ya huo mwangaza aliyemlikiwa na mamake. Basi na hiki chakula kutokana na uamuzi wako lazima kiive hivyo hivyo moto ukiwa kando." Sultani aliona aibu kweli mbele ya watu hao wote, na akaamuru tajiri amlipe kijana pesa zake mara moja na Sultani akampa Abunuasi zawadi kubwa kwa sababu ya ubusara wake. Baada ya hayo yote kukamilika, chakula kiliwekwa juu ya moto, kikaiva na wote wakala.
Wote walimshukuru Abunuasi sana!
Subscribe to:
Post Comments (Atom)
No comments:
Post a Comment