ANGALIA LIVE NEWS

Tuesday, October 14, 2014

Bwana harusi asimulia walivyonusa kifo ajali ya mtumbwi

Bwana harusi, Ramadhani Hamisi (30), aliyenusurika kifo baada ya mtumbwi kuzama katika Ziwa Tanganyika na kusababisha vifo vya watu 10 na wengine 11 kujeruhiwa, ameibuka na kusimulia jinsi alivyochungulia kaburi.

Akizungumza na NIPASHE katika mahojiano maalum jana, Hamis alisema baada ya kuona mtumbwi ukizama, alimrukia mkewe na kumshika mkono na kisha kuanza kuogelea naye hadi nchi kavu na hivyo kunusurika kifo.

Kutokana na hali hiyo, anasema anamshukuru Mungu kwa yeye na mkewe, Mariamu (24), kunusurika katika ajali hiyo iliyohusisha mitubwi miwili ambayo ilitokea Jumamosi iliyopita.

Hata hivyo, anasema ana wasiwasi huenda ajali hiyo ni ya kutengenezwa kwa kuwa kabla yake, zilitangulia ajali za magari mawili kati ya matatu waliyokuwa wamekodi kwa ajili ya kubeba watu waliohudhuria shughuli ya harusi yao.


Hamisi (30), ambaye yeye na mkewe, Mariamu walikuwa wamepanda katika moja ya mtumbwi hiyo, alisema hayo alipozungumza katika mahojiano na NIPASHE jana.

Akisimulia mkasa huo, Hamisi, ambaye ni mkazi wa Kijiji cha Kigalye, mkoani Kigoma, alisema Oktoba 11, mwaka huu, majira ya saa 3:00 asubuhi, alifika kwa shangazi ya mkewe, katika Kijiji cha Mwandiga, kwa ajili ya kufunga ndoa.

Alisema ilipofika saa 6 mchana, ndoa yao ilifungwa na kisha akakodi mabasi madogo matatu aina ya Toyota Hiace kwa ajili ya kuwapeleka watu katika Kijiji cha Kalalangabo tayari kwa safari ya kwenda nyumbani, kijijini Kigalye.

Hamisi alisema walifika katika Kijiji cha Kilalangabo majira ya saa 8:00 mchana na kisha yeye, mkewe na watu wengine waliohudhuria shughuli hiyo wakapanda mitumbwi miwili tofauti iliyounganishwa kwa miti miwili nyuma na mbele.

Alisema walianza safari ya kwenda kijijini Kigalye, lakini walipofika mita 70 kutoka nchi kavu, mashine ya mtumbwi mmoja ilizimika.

Hata hivyo, alisema muda mfupi baadaye, mashine ya mtumbwi huo iliwaka na safari ikaendelea.

Hata hivyo, alisema walipofika katikati ya maji, mashine hiyo ilizimika tena na mawimbi yalikuwa makubwa, hali iliyosababisha mti uliokuwa umeunganishwa mbele ya mtumbwi kukatika.

Alisema baadaye, mti wa nyuma nao ulikatika na mtumbwi mmoja ukazama.

Hamisi alisema watu waliokuwamo kwenye mtumbwi uliozama, waliingia kwenye mtumbwi wa pili, ambao nao pia ukazama.

“Baada ya kuzama mitumbwi yote, mimi nikamrukia mke wangu, nikamshika mkono na kuanza kuogelea naye. Nilipofika karibu na nchi kavu, mke wangu aliishiwa nguvu na mimi nikaishiwa nguvu. Nikapiga kelele, jamani tunakufa! Tunaomba mtusaidie!” alisema Hamisi.

Aliongeza: “Ndipo ikaja mitumbwi ya ‘kachinga’ (mitumbwi inayotumiwa kuvua samaki mchana), ikatuokoa. Tulipofika nchi kavu, mke wangu alikuwa amekunywa maji, hivyo walimpeleka Hospitali ya Mkoa Maweni kwa matibabu na alilazwa wodi namba 5.”

Alipoulizwa kuhusiana na kukodi mitumbwi badala ya boti, Hamisi alisema alipata ofa ya kununua mafuta lita 10 ndiyo maana alikubali kuwasafirisha watu kwenye mitumbwi ya kuvulia samaki.

Alisema hiyo ilitokana na wakodishaji wa boti kumtaka anunue lita 30, ambazo hazikuwa ndani ya uwezo wake.

“Mimi ninamshukuru Mungu sana kwa kunusurika pamoja na mke wangu, kwani ni wengi waliokufa. Mimi Mungu ameniona na mke wangu tuendelee kuishi. Kwa sababu watu wengi walipanda mitumbwi hiyo. Hata wale, ambao hawakuwa wamealikwa kwenye harusi. Bali watu wa Kijiji cha Kigalye, ambao walikuwa Kigoma mjini, baada ya kuona mitumbwi miwili ya bure ipo, walipanda,” alisema Hamisi.

Alisema wakati wanakwenda kufunga ndoa katika Kijiji cha Mwandiga, walitanguliza muziki katika Kijiji cha Kigalye, hivyo maharusi walikuwa ili sherehe zianze.

“Mimi nasikitika sana kuona ajali hii, kwani kabla hatujapanda mitumbwi Hiace tatu tulizokuwa tumekodi, mbili ziligongana. Na wakati tunakwenda kupanda mitumbwi, nayo ikazama na kuua watu 10. Tunamshukuru Mungu kwamba, mama mkwe, baba mkwe, mama yangu na baba yangu wamenusurika katika ajali hiyo,” alisema Hamisi.

Aliongeza: “Ni jambo la kumshukuru Mungu, kwani mara nyingi mitumbwi inapozama na kuua watu, huwa samaki zinavuliwa kwa wingi. Mimi ninavyoona ajali hii ina mkono wa mtu.”


MARIAMU ALONGA
Bibi harusi, Mariamu akizungumza na NIPASHE jana alisema baada ya kupata mchumba, yeye na mumewe, Hamisi waliona ni vizuri wakafunge ndoa kwa shangazi yake katika Kijiji cha Mwandiga.

Alisema wazazi wake, ambao anaishi nao katika Kijiji cha Kigalye, walitengana siku nyingi.

Mariamu alisema wanamshukuru Mungu kutokana na yeye na mumewe kuwa wa kwanza kuokolewa.

“Tulipokaribia kufika nchi kavu, huku mume wangu akiwa amenishika mkono kwa kuwa anajua kuogolea, mitumbwi ya ‘kachinga’ ikaja ikatuokoa na kutupeleka nchi kavu. Kisha mimi nikazimia. Nimekuja kuzinduka niko wodi namba tano ya Hospitali ya Mkoa ya Maweni,” alisema Mariamu.

Alisema alishangazwa sana na tukio la mitumbwi yote miwili kuzama na kusababisha vifo vya watu 10.

Aliungana na mumewe kuhisi ajali hiyo kuwa imetengenezwa, ingawa anamshukuru Mungu kuona ndugu zake pamoja na ndugu za upande wa mumewe kwa kunusurika katika ajali hiyo.
 
CHANZO: NIPASHE

No comments: