
Rais Kikwete alisema juzi mjini Dodoma baada ya kukabidhiwa Rasimu ya Katiba inayopendekezwa iliyoandaliwa na Bunge Maalum la Katiba (BMK), alisema kuwa kura ya maoni ya kuipitisha Katiba hiyo au kuikataa itafanyika wakati wowote kabla ya uchaguzi mkuu wa mwakani.
Makamu Mwenyekiti wa Chadema, Profesa Abdallah Safari, aliwambia waandishi a habari mjini hapa jana kuwa kwa kauli hiyo imevitia hofu vyama vya siasa kwa kuwa inakiuka makubaliano yake na vyama hivyo yaliyofikiwa katika mkutano uliofanyika Agosti 31, mwaka huu.
Katika mkutano huo uliomkutanisha Rais Kikwete na viongozi wa vyama vya siasa vyenye usajili wa kudumu kupitia Kituo cha Demokrasia Tanzania (TCD), pamoja na mambo mengine, walikubaliana kwamba kura ya maoni itaitishwa baada ya uchaguzi mkuu unaotarajiwa kufanyika Oktoba mwakani.
Vile vile, walikubaliana kwamba ili kuuboreha uchaguzi mkuu wa mwakani, mwezi ujao Bunge la Jamhuri ya Muungano litafanya marekebisho katika sheria ya uchaguzi kwa kuruhusu kuundwa kwa tume huru ya uchaguzi, kuruhusu mgombea binafsi, kuruhusu matokeo ya uchaguzi wa rais kuhojiwa mahakamani na kutaka mshindi wa urais kupata zaidi ya kura asilimia 50.
Profesa Safari alisema wasiwasi wao ni kuwa kama kura hiyo itapigwa kabla ya uchaguzi mkuu, daftari la kudumu la wapiga kura halitasimamia haki kwa kuwa halitakuwa limeshaboreshwa na vile vile tume huru ya uchaguzi haitakuwa imepatikana.
Alisema siyo msimamo rasmi wa chama wala Umoja wa Katiba ya Wananchi (Ukawa) na kwamba, watatoa msimamo rasmi baadaye baada ya kufanya utafiti wa kina kupitia kila kipengele kilichomo katika Rasimu ya Katiba inayopendekezwa.
Makamu Mwenyekiti wa Chadema Zanzibar, Said Issa Mohamed, alimlalamikia Rais Kikwete kwa kuelekeza watu wapi wapige kura wapi kwakati wa kura ya maoni.
Mwenyekiti wa Baraza la Wazee Taifa, Hashim Juma Issa, alimlaumu Rais Kikwete kwa kuonyesha dharau kwa kuikataa rasimu ya Jaji Warioba na kuifurahia ya BMK, kukubali BMK kuendelea bila Ukawa na sherehe za juzi kufanyika bila Ukawa na na Jai Warioba kuwapo.
CHANZO: NIPASHE
No comments:
Post a Comment