ANGALIA LIVE NEWS

Thursday, October 16, 2014

EBOLA NI JANGA LA DUNIA

Kasisi wa Hispania ambaye aliambukizwa virusi vya Ebola nchini Liberia akisafirishwa kwenda kupata matibabu nchi mwao.

Kwa kuongezeka kwa idadi ya vifo na ugonjwa kuendelea kusambaa, harakati za kutafuta tiba ya Ebola zinaendelea.

Wataalam tayari wanajua mengi kuhusu virusi hivi na namna vinavyoshambulia, lakini kupambana navyo kwa kutumia dawa ni jambo jipya.

Tangu Ebola ilivyobainika mwaka 1976, kila mlipuko umekuwa ukidhibitiwa kwa masharti ya hali ya juu kuhusu usafi-kutengwa kwa wagonjwa na wanaohisiwa kuambukizwa ugonjwa virusi vya Ebola, kuwahakikisha wafanyakazi wa vituo vya afya na hospitali kuvaa nguo zinazostahili kuzuia maambukizo na kufanya usafi wa hali juu na utupaji salama wa taka zinazotokana na kumhudumia mgonjwa.

Hakuna dawa za kutibu Ebola kwa sababu kutengeneza dawa hizo ni gharama kubwa, na mpaka sasa makampuni makubwa ya kutengeneza dawa bado hayajaona soko kubwa. Hilo linabadilika.
Lengo linaloeleweka.

Virusi vinaweza kuingia mwilini kupitia majimaji ya mwili wa mgonjwa kama damu, matapishi, kinyesi kupitia sehemu ya jeraha la ngozi au kamasi au machozi kama vile ya macho.

Wakiwa wameingia ndani ya mwili, wanazaliana haraka katika damu, na kushambulia seli.

Ugonjwa huu si wa kuambukiza kama mafua. Kukaribiana kwa karibu sana na mtu aliyeambukiza virusi vya Ebola ndiko kunakosababisha virusi vya Ebola kumwingia mtu mwingine. Maambukizo pia yanaweza kutokea kwa kugusana na matandiko yaliyolaliwa na mgonjwa wa Ebola, nguo na mahali alipoketi mgonjwa.

Yote haya yanafahamika kwa karibu miaka 40, lakini sasa limekuwa tishio kubwa duniani.
Zana za Matibabu

Madaktari wanaelekeza nguvu zao katika njia mbili:

Matibabu kusaidia watu ambao tayari wameambukizwa na virusi vya Ebola.

Chanjo za kuwakinga watu kuambukizwa virusi vya Ebola.

Kuna majaribio mbalimbali yamefanyika kuhusu chanjo na dawa za kutibu Ebola zikiwa katika kuandaliwa, lakini bado hazijafanyiwa majaribio kamili kwa ajili ya usalama au ufanisi wake.

Dawa za majaribio kama vile ZMapp tayari zimegawiwa kwa wagonjwa katika maeneo ya mlipuko wa Ebola, lakini hazijawatibu wagonjwa wote. Wafanyakazi wawili wa mashirika ya misaada kutoka Marekani na raia mmoja wa Uingereza walipona baada ya kutumia dawa hii, lakini daktari wa Liberia na kasisi wa Hispania wamefariki dunia.

Dawa hii awali ilifanyiwa majaribio kwa wanyama, na wataalam wanasema bado haifahamiki kama dawa hii inaongeza fursa za mgonjwa kupona.

Akiba ya dawa hizi ni ndogo sana na watengenezaji wa dawa hii wanasema itachukua miezi kadhaa kuongeza uzalishaji.

Matumizi ya damu ya watu walionusurika pia nayo inafanyiwa majaribio kama tiba. Inafikiriwa kuwa damu hii huenda ikawa na chembechembe zinazoweza kupunguza makali ya virusi. Lakini hii inachukua muda wa mgonjwa-bado watahitaji miili yao kujua namna ya kupambana na virusi hivi.

Chanjo

Majaribio ya chanjo yalianza nchini Marekani mwezi huu.

Marekani, Uingereza na Canada zinafanya majaribio ya chanjo mbalimbali dhidi ya Ebola katika maabara.

Lengo ni kupata dozi 20,000 zitakazoweza kutumika Afrika Magharibi mapema mwaka ujao.

Kwa kawaida inachukua miaka mingi kwa binadamu kufanyiwa majaribio kabla ya kupata chanjo kamili itakayothibitishwa kwa matumzi.

Lakini hii ni dharura kwa ajili ya mlipuko wa Ebola kwamba majaribio ya chanjo yanaharakishwa katika kiwango cha kushangaza.

BBC

No comments: