ANGALIA LIVE NEWS

Tuesday, October 14, 2014

HOTUBA YA PONGEZI KWA MH.RAISI WA TANZANIA, RAISI WA ZANZIBAR NA VIONGOZI WOTE WALIOFANIKISHA KUPATIKANA KWA KATIBA INAYOPENDEKEZWA.


Ndugu viongozi wote wa serikali ya Chama Cha Mapinduzi diaspora, wawakilishi wa serikali ya Tanzania ndani na nje ya nchi, taasisi za kitaifa na kimataifa, mashirika ya kijamii, mashirika binafsi, viongozi mbalimbali; itifaki imezingatiwa.

Awali ya yote napenda kumshukuru M/Mungu kwa kutupa uzima na afya njema kuweza kutekeleza majukumu yetu ya kila siku ikiwemo kusimamia sera na utendaji wa serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kupitia Chama Cha Mapinduzi huku diaspora. Pia napenda kuchukua fursa hii kumshukuru na kumpongeza Raisi wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na M/kiti wa Chama Cha Mapinduzi kwa kuchagua mwakilishi wa Diaspora kutuwakilisha kwenye mchakato huu na kuona umuhimu wa kufungua matawi ya CCM nje ya nchi. Ni wazi raisi wetu anatujali, anatupenda na kututhamini na sisi tunamuahidi kumuunga mkono ktk kila nyanja ya maendeleo. 


Nikiwa kama mratibu wa matawi ya Chama Cha Mapinduzi Marekani na Muwakilishi wa Matawi ya Diaspora; mimi Loveness Mamuya kwa niaba ya wana CCM wote waishio Marekani na Diaspora tunapenda kutoa pongezi za dhati kwa Dr Jakaya Mrisho Kikwete (Raisi wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania) pamoja na Dr Ali Mohamed Shein (Raisi wa Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar) kwa kuanzisha, kusimamia na kufanikisha mchakato wa katiba mpya na hatimaye kupatikana kwa katiba inayopendekezwa. Ni wazi kwamba hekima, busara, weledi na upendo wenu kwa Tanzania ni hazina isiyo futika. Sisi wana CCM diaspora tumefarijika sana na tunathamini jitihada zenu za ziada ktk kupambana na changamoto mbalimbali ambazo zilikuwa na malengo ya kukwamisha mchakato huu. Aidha tunawaombea maisha marefu yenye utulivu na mafanikio kwa kipindi chote hiki hadi kuelekea 2015 mkapate kutimiza ahadi ya kuvikamilisha vipengele muhimu vya katiba inayopendekezwa.  Kama taifa linavyoweza kuficha mambo nyeti ya nchi yetu, basi yakafiche majina yenu kwa wino wa dhahabu. 



Shukrani pia zimuendee Mh Samuel Sitta (M/kiti wa Bunge Maalum la Katiba) pamoja na makamu wake Mh Samia Suluhu Hassan kwa kusimamia kanuni, sheria na taratibu zilizowekwa na hatimaye kufanikisha zoezi zima la kupatikana katiba inayopendekezwa. Ni wazi kwamba kazi yenu haikuwa rahisi na kuna kipindi iliwabidi mfanye maamuzi magumu lakini kasi na viwango vyenu vimetupatia katiba inayopendekezwa mapema kabla ya kikomo mlichowekewa. Ari na kujitoa kwenu kusimamia bunge la katiba ni historia ambayo itasomwa na vizazi vyote vya watanzania. Nyinyi ni mashupavu na mashujaa wa vita dhidi ya matabaka yote ya vyama vya siasa, udini na ukabila na hatimaye mmefanikiwa kwa kiasi kikubwa sana kutupatia katiba ambayo inawajali watanzania wote licha ya tofauti zetu za kimazingira, kiutawala na kiufanisi. Mapenzi yenu ya dhati kwa Tanzania yetu ni ishara ya matumaini na imani ya Tanzania njema huko mbeleni. Kama taifa linavyoweza kuficha mambo nyeti ya nchi yetu, basi yakafiche majina yenu kwa wino wa dhahabu. 

Shukrani za dhati ziwafikie wajumbe wote wa bunge maalum la katiba kwa kuchambua, kuboresha na kurekebisha mambo ya msingi yanayohusu taifa letu pamoja na kutanguliza maslahi ya taifa kwanza. Umakini na uwajibikaji wenu ndio silaha ya kila mtanzania ktk kuifikia dira ya maendeleo ya taifa letu. Asanteni kwa kutambua makundi yote ktk jamii na kuyatendea haki. Asanteni kwa kuwa mabalozi wa wakulima, wafugaji, wavuvi, wachimba madini, wafanya biashara wakubwa na wadogo, sekta binafsi, walemavu, wakina mama, wasomi, vijana, watoto na wazee. Hii imetudhirishia kwamba uteuzi wa Dr Jakaya Mrisho Kikwete kwenu ni wa busara na wa kipekee. Hongereni sana kwa kazi nzuri mliyoifanya na tunaamini hata yule mjumbe aliyetangulia mbele ya haki anajivunia kazi nzuri mliyoifanya. Mungu aendelee kuilaza roho yake mahala pema peponi. Kama taifa linavyoweza kuficha mambo nyeti ya nchi yetu, basi yakafiche majina yenu kwa wino wa dhahabu. 

Nitakuwa mchoyo wa fadhila na shukrani kama sitatoa pongezi zangu za dhati kwa tume ya mabadiliko ya katiba chini ya M/kiti wao Mh Joseph Sinde Warioba kwa kutupatia rasimu ya katiba mpya ambayo ndio msingi wa kwanza na wa muhimu ktk upatikanaji wa katiba mpya. Katiba inayopendekezwa ina 82% ya michango yenu na hivyo ni wazi kwamba mnastahili pongezi kwa juhudi na uadilifu wenu ktk kukusanya, kuchambua na kuwasilisha rasimu ya katiba. Hakika watanzania tunajivunia umahiri wenu na tutawakumbuka ktk kila hatua ya mendeleo ya taifa letu. Kama taifa linavyoweza kuficha mambo nyeti ya nchi yetu, basi yakafiche majina yenu kwa wino wa dhahabu. 

Mwisho kabisa, natoa ari kwa watanzania hasa wana CCM wote ndani na nje ya nchi kwamba safari bado inaendelea, kupata jambo lolote zuri ni lazima tupambane. Tunawaomba watanzania wote tukapambane ktk zoezi la kupiga kura kwa kuiunga mkono katiba inayopendekezwa. Ni wajibu wa kila mmoja wetu kuisoma, kuipitia na kuielewa katiba inayopendekezwa na kuwaelimisha wale ambao hawawezi kufanya uchambuzi wa kina. Hayati Mwl Nyerere alisema watanzania tuna maadui watatu; nao ni umaskini, ujinga na magonjwa. Leo hii wapo matajiri wa uwezo lkn maskini wa mawazo, wapo wasomi wa vyeti lkn wajinga wa kufikiri na wapo wazima wa afya lakini wagonjwa wa akili. Hawa ndio maadui zetu watanzania, twendeni tukapambane nao na tusikubali watuyumbishe kwa namna yoyote ile. Tukaipigie katiba inayopendekezwa kura ya NDIO ili tupate katiba ambayo itatuvusha mbele kwa zaidi ya miaka 50 inayokuja. Mungu akatubariki na akatuongoze ktk kusimamia, kuitetea na kuipigania Jamhuri ya Muungano wa Tanzania. Kama taifa linavyoweza kuficha mambo nyeti ya nchi yetu, basi yakafiche majina ya watanzania wote watakao ipigia katiba inayopendekezwa kura ya NDIO kwa wino wa dhahabu. 

Mwisho kabisa, naomba watanzania wenzetu mtambue kwamba nchi  yetu inasifika duniani kwa amani, umoja, utulivu na upendo. Kuna jitihada za makusudi zinafanywa na baadhi ya watu wasio na malengo ya dhati na nchi yetu kuweza kuichafua. Kwa pamoja tuwatambue, tusikubali na tujiweke mbali na watu hawa. Kwa pamoja tukaijenge Tanzania bora ya vizazi vyetu vya jana, vya leo na vya kesho. Waswahili wanasema, "mkataa kwao ni mtumwa." Sisi wana CCM diaspora tunaipenda na tutaendelea kuiwakilisha Tanzania yetu popote tuendako. Hongera Dr Jakaya Kikwete,  Hongera Dr Ali Mohamed Shein! Shime Chama Cha Mapinduzi. Mungu ibariki Tanzania, Mungu wabariki watanzania. 
Asanteni sana.

Imewasilishwa na Ndugu Loveness Mamuya;
Kada Mzalendo na Mratibu wa Matawi ya Chama Cha Mapinduzi,
(USA/ Diaspora)