Mfanyakazi wa idara ya usalama Marekani akizunguka nje ya uzio wa White House
Vyombo vya habari vya Marekani vinaripoti juu ya ukiukaji mwingine mkubwa wa usalama unaohusiana na jukumu la idara ya usalama yenye kumlinda Rais Barack Obama na familia yake.
Ripoti zinaeleza kwamba mlinzi wa kampuni moja binafsi ya usalama akiwa na bunduki alipanda kwenye lifti na bwana Obama wakati wa ziara yake kwenye kituo cha kudhibiti na kuzuia magonjwa cha Marekani-CDC mjini Atlanta mwezi uliopita wakati alipokwenda kuzungumzia mlipuko wa Ebola.
Mlinzi huyo alianza kumpiga picha bwana Obama akitumia kamera ya kwenye simu yake ya mkononi akipuuzia ombi la idara ya usalama la kumtaka kuacha kufanya hivyo.
Idara ya usalama haikujua kwamba mlinzi huyo alikuwa na bunduki hadi alipofukuzwa kazi na mkuu wake na ndipo iliarifiwa baadae kwamba alipatikana na hatia mara tatu kwa kumvamia na kumpiga mtu.
Tukio hilo la Atlanta lilitolewa saa kadhaa baada ya mkuu wa idara ya usalama Julia Pierson kutoa ushahidi mbele ya kamati maalumu ya bunge kuhusu mwanajeshi mmoja wa zamani ambaye aliruka uzio wa White House na kukimbia kuingia kwenye jengo la White House kabla ya kukamatwa. Tukio hilo lilitokea Septemba 19 ikiwa ni siku tatu baada ya tukio la Atlanta.
Julia Pierson
Bibi Pierson aliiambia kamati maalumu ya bunge la Marekani inayohusika na masuala ya usalama kwamba Omar Gonzalez mwenye umri wa miaka 42 alifanikiwa kumpita ofisa mmoja kabla ya kukamatwa karibu na ukumbi ambao unafanyiwa sherehe katika White House.
Awali idara ya usalama ilieleza kwamba Gonzalez alikamatwa mara baada ya kuingia katika jengo hilo kupitia mlango wa mbele uliokuwa wazi na kwamba alikuwa hana silaha kwa wakati huo.
Credit:VOA
No comments:
Post a Comment