Dar es Salaam. Rais Jakaya Kikwete amesema Serikali inafanyia kazi utaratibu wa kufunga mfumo wa kuona matukio yote yanayoendelea jijini hapa ili kupunguza tatizo la uhalifu.
Akizungumza jana katika uzinduzi wa Barabara ya Mwenge-Tegeta, alisema suluhisho la wizi wa miundombinu ya barabara na kukwapua mali za wananchi, linakuja kwa kuwa kila litakalofanyika litaonekana.
“Hawa wezi wa miundombinu na ukwapuaji kwa kutumia bodaboda dawa yao inakuja...tunajenga uwezo wa kufahamu kinachotokea maeneo yote ya Dar es Salaam humu barabarani na mitaani na hadi Juni mwakani mradi utakuwa umekwisha au umefikia pazuri,” alisema.
Alisema baada ya kukamilisha mradi huo jijini hapa, utaendelea na mikoa mingine
Kuhusu foleni
Rais Kikwete alisema tatizo la foleni ya magari Dar es Salaam halitamalizwa kama watu wanavyofikiri kwa kuwa linasababishwa na kasi ya maendeleo.
Alisema miaka 10 iliyopita hali haikuwa hivyo, barabara zilitosha, lakini sasa hali ya maisha imeboreshwa na watu wananunua magari kila siku.
Rais Kikwete alisema Serikali inaendelea kupunguza foleni ikiwamo upanuzi wa barabara kuu za jiji, ujenzi wa barabara za pete na kuanzisha ujenzi wa miji ya kisasa ya pembezoni.
Jitihada nyingine ni mradi wa treni za kisasa zenye hadhi ya kimataifa, usafiri wa kivuko kati ya Bagamoyo na Dar es Salaam na ujenzi wa Mradi wa Mabasi yaendayo Kasi (Dart) ambao awamu ya kwanza unakaribia kukamilika.
“Kuna watu wanazungumza uwezekano wa kupanua barabara mitaa ya Uhuru au maeneo mengine katikati ya jiji, hilo haliwezekani na tusibaki tunalaumu tu. Lile eneo halina namna ya kupunguza foleni vinginevyo ubomoe majengo ili kupanua barabara jambo ambalo nchi nyingine hazifanyi hivyo,” alisema Rais Kikwete.
Upanuzi Barabara ya Mwenge-Tegeta yenye Kilomita 12.9 ulianza mwanzoni mwa mwaka 2011 na umegharimu Sh99.6 bilioni.
Mwananchi
No comments:
Post a Comment