Advertisements

Friday, October 31, 2014

Juma Kaseja aamua kuvunja mkataba Yanga

Kipa Juma Kaseja ametoa masharti mawili mazito Yanga na kama hayatatekelezwa yuko tayari mkataba wake na klabu hiyo uvunjwe rasmi, imeelezwa.

Hata hivyo, moja ya sharti ambalo ni vigumu kutekelezeka ni pamoja na kutaka kupewa nafasi za kudaka katika Ligi Kuu ya Vodacom Tanzania Bara (VPL), ambayo hajawahi kusimama langoni msimu huu tangu pazia lilipofunguliwa Septemba 20.

Kupitia meneja wake, Abdulfatah Saleh, Kaseja ameipa masharti Klabu ya Yanga kama inataka kubaki naye immalizie fedha za usajili wake za Sh. milioni 20 na pia kuanza kumpa nafasi ya kudaka.

Kaseja, kipa huyo namba moja wa zamani wa Tanzania, hana nafasi kwenye kikosi cha kwanza cha Yanga chini ya kocha Mbrazil Marcio Maximo.


Katika kipindi cha kocha Mholanzi Hans van der Pluijm, Kaseja alikuwa anadaka kwa zamu na kipa chaguo la kwanza Yanga, Deogratius Munishi ‘Dida’.

Abdulfatah alisema jana kuwa katika mkataba wao walioingia na Yanga, walikubaliana kukamilishia malipo ya mwisho ya dau la usajili ya (Sh. milioni 20) ifikapo Januari 15, mwaka huu, lakini klabu hiyo hadi sasa alidai haijafanya hivyo.

Alisema wakati wanavumilia hilo, bado mteja wake hana nafasi kwenye kikosi cha kwanza jambo ambalo ni hatari kwa kipaji cha kipa huyo wa zamani wa Simba.

Abdulfatah alisema wanayaingiza masharti hayo yote kwa maandishi na kuyapeleka kwa uongozi wa Yanga uyatekeleze, vinginevyo hatua za kuuvunja mkataba zitafuata. Meneja huyo, hakutaka kuweka wazi lini watakabidhi barua hiyo kwa uongozi wa Yanga, hata hivyo.

Kaseja ameidakia Yanga mechi 15 tangu asajiliwe mwishoni mwa mwaka jana, akiwa kipa huru baada ya kuachwa na Simba kwa madai ya kushuka kiwango. Kati ya mechi hizo, tano ni za Ligi Kuu na moja ya Ligi ya Mabingwa Afrika.

Katika mechi hizo Kaseja amefungwa mabao 10, yakiwamo matatu Yanga ikilala 3-1 mbele ya mahasimu, Simba katika mechi ya 'ndondo ya 'Nani Mtani Jembe' iliyomfukuzisha kocha Mholanzi Ernie Brandts.

Pamoja na kuwa kipa chaguo la kwanza Simba kipindi hicho, Kaseja hakuwahi kumvutia Maximo alipokuwa akiifundisha timu ya Taifa (Taifa Stars) na wakati fulani alidiriki kuwaita Ali Mustafa 'Barthez' na Dida, akimuacha Kaseja.

Wakati Kaseja akitaka kuvunja mkataba wake na Yanga, tayari kumeshaanza kuenea taarifa kuwa timu yake ya zamani ya Simba inataka kumrejesha wakati wa usajili wa dirisha dogo msimu huu.

Alipotafutwa na NIPASHE kuzungumzia suala hilo jana, Katibu Mkuu wa Yanga, Beno Njovu alisema: "Swali lako la kwanza siwezi kukujibu maana mchezaji Juma Kaseja hana meneja anayetambulika na taasisi yoyote, iwe Yanga, TFF au hata Fifa."

Njovu alienda mbali zaidi akinukuu baadhi ya vipengele vya Fifa kwa kusema: "Mawakala wa wachezaji hawatambuliwi na Fifa tangu 2001. Mawakala wa wachezaji wanasajiliwa moja kwa moja na kila chama cha soka. Hivyo, hakuna kitu kama hicho kuwa na wakala wa Fifa wa mchezaji."

Aidha, Njovu alisema: "Jukumu la kupanga timu ni la kocha, wala si mtu yeyote."
 
CHANZO: NIPASHE

No comments: