Mbunge wa Kahama, James Lembeli akifafanua jambo alipokuwa akizungumza na waandishi. Picha na Edwin Mjwahuzi
Dodoma. Mbunge wa Kahama, James Lembeli amemtuhumu Katibu Mkuu wa zamani wa CCM, Yusuph Makamba kwamba alikuwa nyuma ya mpango mahususi wa kumhujumu ili akose ubunge katika Uchaguzi Mkuu wa 2010.
Lembeli, mmoja wa wabunge walio mstari wa mbele katika vita dhidi ya ufisadi, alisema mpango huo ulitekelezwa kwa kueneza taarifa za kuanzisha jimbo la Ushetu ambalo alitakiwa agombee badala ya Kahama, lakini baadaye msamaria mwema alimpa taarifa kwamba jimbo hilo ni halipo.
Lembeli katika mahojiano yake maalumu na gazeti hili mjini Dodoma alisema alipewa taarifa hizo saa chache kabla ya muda wa mwisho wa kurudisha fomu za kugombea ubunge na kwamba tukio hilo lilimfanya afute fomu yake ya kugombea mara mbili.
“Ulikuwa ni uhuni na ufisadi wa hali ya juu kisiasa,” alisema mwanahabari huyo wa zamani katika mahojiano hayo maalumu yaliyofanyika mjini Dodoma mapema wiki iliyopita.
Alisema mara ya kwanza alijaza kwamba anagombea Jimbo la Kahama lakini alifuta na kuandika jimbo la Ushetu baada ya kupewa taarifa za kuanzishwa kwa jimbo hilo na baadaye alifuta Ushetu na kuandika tena Kahama baada ya kugundua kuwa ulikuwa mchezo mchafu.
“Baada ya kuruka viunzi, viongozi waandamizi wa CCM wa Shinyanga, akiwamo Mwenyekiti wa Mkoa, Hamisi Mgeja walisusa kunifanyia kampeni,” aliongeza Lembeli ambaye aliibuka na ushindi wa asilimia 54.5 kati ya kura zilizopigwa.
Alisema mpango huo wa kumhujumu ulianza mapema pale baadhi ya viongozi walipokuwa wakieneza kwamba yeye (Lembeli) hatakiwi na kwamba ukweli siyo kwamba alikuwa hatakiwi na wananchi bali baadhi ya viongozi.
Hata hivyo, Makamba alipoulizwa alisema ni uzushi kwa kuwa kazi ya kugawa majimbo ni ya Tume ya Taifa ya Uchaguzi, CCM kazi yake ni kusimamisha tu wagombea.
“Niacheni nipumzike niendelee kula pensheni yangu. Sasa niko Bumbuli natoka kuswali na ninakwenda kula Iddi, niacheni nipumzike jamani, kama kuna maswali zaidi aulizwe katibu mkuu wa sasa,” alisema Makamba.
Hata hivyo, Lembeni katika mahojiano hayo alisisitiza: “Ninachodhani walikaa chini na mambo haya yalifanyika Dar es Salaam na mbaya zaidi katika ofisi ya Makao Makuu ya CCM kwa sababu ndio walioleta taarifa.”
Chimbuko la Ushetu
Kwa mujibu wa Lembeli, taarifa kwamba kuna jimbo jipya la Ushetu ambako ndiko alikozaliwa, zilimfikia yeye na wagombea wenzake saa 9:30 wakati mwisho wa kurudisha fomu ilikuwa saa 10:00 jioni.
“Wagombea wote tulikuwa tumesharejesha fomu ya kugombea Jimbo la Kahama. Ilipoletwa hiyo taarifa, Katibu wa CCM wa wilaya ya Kahama akawapigia simu wagombea wote kuwa anatuita ofisini,” alisema mtangazaji huyo wa zamani wa Shirika la Utangazaji la Ujerumani, Deutche Welle na kuongeza:
“Tulipofika pale akatuambia kuna habari mpya kwamba kuna jimbo jipya la Ushetu, kwa hiyo hapa yako majimbo mawili kuna Jimbo la Kahama na kuna jimbo la Ushetu.”
Pia, mwandishi huyo wa zamani wa gazeti la Kiongozi alisema katibu huyo aliwaambia kuwa maelekezo aliyopewa kutoka makao makuu ya CCM ni kuwataka kila mmoja afanye uamuzi papo hapo kama anagombea Kahama au Ushetu.
Lembeli alidai baada ya kuelezwa hivyo, alihoji sana ili kupata ukweli kama jimbo hilo jipya limetangazwa na CCM au NEC.
“Yule katibu akapiga simu kwa mzee (katibu mkuu wa CCM wa wakati huo, Yusuf Makamba) akawa ameacha sauti tusikie. Akamwambia ‘mzee hapa wagombea wanahoji maswali mengi’,” alisema Lembeli.
“Makamba akauliza nani huyo, akaambiwa ni Lembeli, akasema ‘huyo kijana ni mkorofi sana, mbishi sana huyo, kama hataki aache’. Nikachukua fomu nikafuta Kahama nikaandika Ushetu.”
Lembeli alisema mpango uliokuwapo ni kumfanya (yeye) achukue fomu ya jimbo ambalo halipo na atakapokuja kushtuka, muda wa kurudisha fomu na kampeni uwe umeshakwisha.
“Wakati ule mtandao wa simu ulikuwa haujasambaa kwenye jimbo zima. Muda wa mimi kufanya mashauriano kule kijijini haukuwapo na Ushetu ni eneo ambalo nilizaliwa,” alisema.
“Nafsi ikaniambia nikigombea huku mjini bila kuwa nimewaarifu kule nitakuwa nimewavunjia heshima kwa hiyo nikaamua iwe Ushetu. Sasa tukawaambia leteni fomu mpya tujaze wakasema ‘futa hapo kwenye Kahama andika Ushetu’. Nikafuta nikaandika Ushetu.”
Lembeli (58) alidai baada tu ya kufanya uamuzi huo, Mgeja ambaye wakati huo alikuwa Dar es Salaam kwenye ofisi ya makao makuu ya chama, akamtuma mke wake kuja kuchukua fomu za Jimbo la Kahama.
Kwa mujibu wa Lembeli, siku iliyofuata walianza kampeni kwa ajili ya kura za maoni ndani ya chama wakati huo wakiwa wanaamini kuna jimbo jipya la Ushetu limetangazwa na Nec.
Aliyemwokoa
Lembeli alisema: “Namshukuru sana (mtangazaji wa TBC jina tunalo). Yeye ndio aliniambia ‘Lembeli mbona nasikia sikia jambo, huko kuna nini?”
Alisema baada ya kampeni nzito za siku nne na walipokuwa wakiingia siku ya tano ya kampeni hizo ndani ya chama, akahisi kuwa kuna mchezo mchafu unaendelea.
“Nilipiga simu Tume ya Uchaguzi kuulizia nikaambiwa unasemaje, eti jimbo la Ushetu? Ushetu ndio mnyama gani. Mzee, nilipata tumbo la kuharisha,” alisema Lembeli.
“Yaani nilipoulizwa tu Ushetu ni mnyama gani nilipata tumbo la kuharisha nikajua tayari nimeshapoteza nafasi,” alisema Lembeli katika mahojiano hayo.
“Siku ya tano ikaja simu kutoka CCM ya kutuita wale tuliokuwa tunagombea Ushetu wakatuambia makao makuu walikuwa wameghafilika kulikuwa hakuna jimbo linaitwa Ushetu.”
“Kwa hiyo nyie mlikuwa mnagombea Ushetu kama mnataka kuendelea kugombea Jimbo la Kahama futeni hapo Ushetu weka Kahama. Nikafuta Ushetu nikaweka Kahama na hapo hapo Mgeja akajitoa,” alisema.
“Mimi naamini kulikuwa na mchezo kwa sababu kulikuwa na haja gani ofisi kuu ya chama kusema kitu ambacho hakipo? Hata baada ya kushinda kura ya maoni, bado vita ilihamia Dodoma,” alisema.
Baada ya kutokea sakata hilo, Mkurugenzi wa Uchaguzi wa wakati huo, Rajabu Kiravu alilazimika kutoa ufafanuzi kuwa Tume ya Uchaguzi haikuwa imeanzisha jimbo jipya la Ushetu kama ilivyokuwa imetangazwa awali na Katibu wa CCM wa Wilaya ya Kahama, Sospeter Nyigoti ambaye ndiye aliyewaambia wagombea kuwa Ushetu ni jimbo jipya.
Jina lake kupitishwa
Alisema katika majina yaliyochukua muda mrefu kujadiliwa katika vikao vya chama vya uamuzi ya wagombea mjini Dodoma, lilikuwa lake.
“Namshukuru sana Rais Jakaya Kikwete kwa sababu ndiye aliyesimama kidete kutaka haki itendeke,” alisema Lembeli ambaye pia ni Mwenyekiti wa Kamati ya Bunge ya Ardhi, Maliasili na Mazingira.
Lembeli alisema baada ya jina lake kupitishwa, viongozi wakubwa ndani ya chama Mkoa wa Shinyanga hawakukanyaga kwenye Jimbo la Kahama kumfanyia kampeni diwani, mbunge wala Rais.
“Viongozi waandamizi wa chama hawakugusa kabisa kwenye kampeni kwenye jimbo langu. Kwa maana hiyo, mkoa haukumfanyia kampeni Rais kwenye jimbo la Kahama,” alisema.
“Niliachwa peke yangu lakini walitaka kumuonyesha mwenyekiti (Kikwete) siwezi ili kama nikishindwa, waseme ‘si unaona tulikwambia kwamba huyu bwana hakubaliki’.”
Lembeli alisema pamoja na yeye kushinda kura ya maoni kwa tofauti ya kura nne tu, lakini alipokwenda kwa wananchi aliibuka na ushindi wa kishindo kwa kupata kura 32,531.
Wagombea wengine katika jimbo hilo walikuwa Dotto Lubala wa Chadema aliyepata kura 20,912 na Hassan Makapa wa CUF aliyeambulia kura 3,950.
Mwananchi
No comments:
Post a Comment