ANGALIA LIVE NEWS

Monday, October 6, 2014

NINI CHA KUFANYA MPENZI WAKO ANAPOWASILIANA NA EX WAKE?-3


6. Anaendelea kumpa misaada mbalimbali. Ukiona mpenzi wako anaendelea kumsaidia ex wake kama kumtumia muda wa maongezi, fedha za matumizi au kodi ya chumba, ujue bado wanapendana na anafanya hayo kwa sababu anaamini ipo siku watarudiana.

7. Bado anazo zawadi walizokuwa wanapeana kipindi cha nyuma. Ukiona mpenzi wako bado anatunza zawadi walizowahi kupeana na ex wake kipindi cha mapenzi yao, ni dhahiri kwamba bado anampenda na wanaendelea kuwasiliana.

Yawezekana pia kwenye simu yake bado kuna sms au picha walizokuwa wakitumiana kipindi cha nyuma, amezihifadhi hataki kuzifuta! Hiyo ni dalili kwamba bado anampenda.

MBINU ZA KUKABILIANA NA TATIZO HILI
Kuna usemi wa wahenga kwamba ukishalijua tatizo ni rahisi sana kukabiliana nalo ndiyo maana kabla ya kukupa mbinu za kupambana na tatizo la mpenzi wako kuwasiliana na ex wake, nimeanza kwa kukupa dalili ambazo ukiziona, ujue bado anampenda ex wake na wanaendelea kuwasiliana.

1. ZUNGUMZA NAYE
Tafuta muda ambao wewe na mpenzi wako mtakuwa mmetulia, unaweza kumtoa ‘out’ halafu mkiwa huko, zungumza naye kwa upole, muulize kwa nini anaendelea kuwasiliana na mpenzi wake wa zamani na mueleze jinsi unavyoumizwa na tabia hiyo. Kama kweli anakupenda, atakusikiliza na hatakuwa tayari kuona unaumia tena kwa tabia yake hiyo, ataacha.

2. MPE MUDA
Yawezekana umekutana na mpenzi wako ikiwa ni kipindi kifupi tangu aachane na mpenzi wake aliyekutangulia. Katika mazingira kama hayo, ni lazima ataendelea kumkumbuka kwa sababu bado hajakubaliana na ukweli.

Mpe muda wa kutuliza akili yake, hata kama bado anawasiliana naye, kuwa mpole kwake na mueleze kwamba anachokifanya, kinamuumiza yeye mwenyewe na wewe pia. Usiwe mkali, mpe muda aukubali ukweli yeye mwenyewe.

3. MFANYIE MAMBO MAZURI
Ni ukweli unaoshangaza kwamba watu wengi, hasa wanawake huwapenda wapenzi wao baada ya kuishi nao kwa muda fulani kutokana na mambo mazuri wanayowafanyia.
Inawezekana umekutana naye, ukamueleza hisia za moyo wako na mkaanzisha uhusiano wa kimapenzi lakini itamchukua muda kukuingiza ndani ya moyo wake na kuanza kukupenda na akishafanya hivyo, itamchukua muda mrefu kukusahau hata mkiwa mmeachana.

Mfanyie mambo mazuri ambayo taratibu yataanza kumfanya amsahau mpenzi wake aliyepita na kukupa kipaumbele wewe. Japokuwa ni kazi ngumu, usikate tamaa na endelea kumfanyia mambo mazuri kila siku. Utashangaa baada ya muda, kumbukumbu zote za mpenzi wake wa zamani zimeisha kabisa.

4. MUACHE ACHAGUE MWENYEWE
Ikiwa mbinu zote za hapo juu zimeshindwa kukusaidia, nafikiri ni muda muafaka wa wewe kuchukua uamuzi mgumu. Mweleze wazi kwamba anatakiwa kuchagua moja, kurudi kwa mpenzi wake wa zamani au kuwa na wewe. Kama bado hamjaoana, unaweza hata kukaa naye mbali kwa muda ili afanye uamuzi sahihi. Atakaporudi kwako kwa mara nyingine, hatarudia tabia yake ya kuwasiliana na ex wake.

Angalizo: Epuka kuzozana, kutukanana au kupigana na ex wa mpenzi wako kwani itakuwa ni sawa na kumwagia petrol kwenye moto. Utawapa sababu ya kuwa pamoja tena.

GPL

No comments: