Advertisements

Thursday, October 30, 2014

Masahihisho

Hivi karibuni kumezuka taarifa za upotoshwaji zilizotolewa kwenye mitandao ya kijamii kwamba Serikali ya Tanzania imemteua Bw. Salaah  (Pichani Mkurugenzi wa Home Shopping Centre) kuwa Konseli wa Heshima (Honorary Consul) kwenye mji wa Guangzhou kwenye Jimbo la Guandong. Watoa taarifa hizo, hawakutoa ushahidi wowote kuthibitisha madai yao zaidi ya kutoa picha mbalimbali za Bw.Salaah kutoka kwenye mitandao mingine ya kijamii.
Taarifa hizo sio za kweli. Kwa mujibu wa Sheria na Kanuni za mahusiano ya kidiplomasia ya China, nafasi ya Konseli wa Heshima haitambuliki 'mainland' China.  Kwa maneno mengine hakuna nchi yoyote duniani inayoweza kuteua mtu kuwa Konseli wa Heshima katika eneo lolote la China isipokuwa Hong Kong ambako kuna mamlaka huru za utawala zinazofuata sheria zake.
Kwa faida ya umma, ni vema kufafanua kwamba Nchi ya China inakubali nchi za Nje kufungua Ubalozi kamili (Embassy) ambao makao yake yanatakiwa kuwepo katika mji Mkuu wa China- Beijing na Konseli Kuu ama kwa lugha iliyozoeleka Ubalozi Mdogo (General Consulate) ambao unaweza kufunguliwa kwenye makao Makuu ya mji wowote ule katika Majimbo ya China.
Watu wengi wamekuwa wakichanganya Ubalozi Mdogo au Konseli Kuu (General Consulate) na Konseli (Ubalozi) wa Heshima  (Honorary Consulate).   Konseli Kuu (General Consulate) ni sehemu ya Ubalozi (ndio maana wengi huuita Ubalozi Mdogo) ambapo kiongozi wake na maafisa wake wote ni watumishi wa Serikali kutokea Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa.  Masharti ya kuwa Mkuu wa Konseli 'General Consulate' lazima uwe Afisa Mwandamizi wa Mambo ya Nje mwenye uzoefu usiopungua miaka 10 ya Utumishi katika Wizara ya Mambo ya Nje.
Kwa muktadha huo, taarifa kwamba Bw.Salaah ameteuliwa kuwa Balozi wa Heshima wa Tanzania huko Guangzhou sio kweli kwasababu Sheria za China haziruhusu uwepo wa nafasi hiyo.  Aidha, Bw Salaah hawezi kuwa Balozi Mdogo (Consul General) kwakuwa yeye sio mwajiriwa wa Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa.  Hivyo habari zinazosambazwa kwenye mitandao ya kijamii sio za kweli na zinalenga kuupotosha umma.

Imetolewa na Idara ya Habari
Wizara ya Mambo ya Nje na Ushiriano wa Kimataifa
Tarehe 30 Oktoba, 2014

1 comment:

Anonymous said...

jamaa anakula sahani mmoja na watu wa mjengoni na anabebwa naye si siri.
so lazima mtakuja hapa na kumkosha kosha kwa jikiii na kutia shoe shiner.