ANGALIA LIVE NEWS

Friday, October 3, 2014

MKUTANO WA MAAFISA MIPANGO WAFUNGULIWA RASMI

Mkutano wa kitaalamu ambao unawakutanisha wataalamu mbalimbali kutoka tasnia za mipango, uchumi, takwimu na maendeleo, wenye wajibu wa kusimamia uchumi na mipango umefunguliwa rasmi na kuwakutanisha kwa pamoja wakurugenzi wa sera na mipango, maafisa mipango kutoka kwenye wizara, Serikali za Mitaa, idara na wakala wa Serikali, pamoja na taasisi za kitaaluma na watafiti wanaojishughulisha na masuala ya maendeleo na uchumi.

Akizungumza wakati wa ufunguzi wa mkutano huo, Balozi (Mstaafu) Dkt. Lumbanga alisema kuwa wachumi na maafisa mipango wana wajibu mkubwa katika kuishauri serikali juu ya njia bora na madhubuti za kupambana na umaskini na kuharakisha maendeleo kwa jamii ya Watanzania.

“Muna dhima kubwa katika kushauri kitaalamu juu ya namna nzuri za kupunguza tatizo sugu la umaskini miongoni mwa Watanzania,” alisema.

Balozi (Mstaafu) Dkt. Lumbanga aliwasihi washiriki kutumia fursa hiyo kujadili kwa kina na kubadilishana uzoefu juu ya sera, mipango na kujenga mtandao wa masuala ya maendeleo ya kitaaluma.

Akizungumza wakati wa ufunguzi wa Mkutano huo, Katibu Mtendaji wa Ofisi ya Rais, Tume ya Mipango, Dkt. Philip Mpango alisema kuwa lengo kuu la mkutano huo ni kutoa fursa ya kuwakutanisha kwa pamoja wataalamu hao na kujenga uelewa wa pamoja juu ya uendeshaji wa shughuli mbalimbali za Serikali.

Aliongeza kuwa Mkutano huo, unatoa fursa za kujadiliana kwa pamoja juu ya mafanikio na njia za kukabiliana na changamoto kwa kubadilishana uzoefu na ujuzi kwenye masuala hayo.

“Mkutano huu ni muhimu katika kuimarisha utendaji kazi wa kada hizi kwa minajili ya kusukuma gurudumu la maendeleo ya kiuchumi na kijamii nchini,” alisema Dkt. Mpango.

Kwa mujibu wa ratiba ya mkutano huo, Mada mbalimbali zinawasilishwa kwa kutilia mkazo masuala mbalimbali ya kimaendeleo yanayojitokeza hivi sasa, ambapo mkutano huo unajadili masuala ya Maendeleo ya Tasnia ya Wapanga Mipango (wachumi, maafisa mipango na watakwimu) na Maandalizi ya Mpango wa Pili wa Maendeleo wa Miaka Mitano (2015/16 – 2020/2021).

Mada nyingine ni pamoja na Mwongozo wa Usimamizi wa Uwekezaji katika Sekta ya Umma ambao una lengo likiwa kuimarisha utendaji, ufanisi na uwajibikaji katika matumizi ya rasilimali za umma zilizotengwa kwa ajili ya miradi na program za maendeleo. Pamoja na mada ya Namna bora ya kujiandaa na Uchumi wa Gesi.

Washiriki wa mkutano huu ni pamoja na wakurugenzi wa sera na mipango, maafisa mipango kutoka kwenye wizara, Serikali za Mitaa, idara na wakala wa Serikali, pamoja na taasisi za kitaaluma na watafiti wanaojishughulisha na masuala ya maendeleo na uchumi.
Katibu Mtendaji wa Ofisi ya Rais, Tume ya Mipango, Dkt. Philip Mpango akisoma hotuba wakati wa mkutano wa mwaka wa wachumi na maafisa mipango unaofanyika jijini Dar es Salaam.
Mgeni Rasmi wa mkutano wa mwaka wa wachumi na maafisa mipango, Balozi Dkt. Matern Lumbanga akizungumza na washiriki wa Mkutano huo kabla ya kuufungua rasmi.
Katibu Mtendaji wa Ofisi ya Rais, Tume ya Mipango, Dkt. Philip Mpango (Kulia) akimpongeza na kumshukuru Mgeni Rasmi wa mkutano wa mwaka wa wachumi na maafisa mipango, Balozi Dkt. Matern Lumbanga mara baada ya kuufungua rasmi mkutano huo.
Baadhi ya viongozi wa wa Ofisi ya Rais, Tume ya Mipango wakimsikiliza kwa makini Katibu Mtendaji wa Ofisi ya Rais, Tume ya Mipango, Dkt. Philip Mpango (Hayupo pichani). Kutoka Kushoto ni Naibu Katibu Mtendaji (Uchumi Jumla), Prof. Longinus Rutasitara, anayemfuatia ni Bw. Paul Sangawe (Naibu Katibu Mtendaji anayeshughulikia Biashara za Kimataifa na Mahusiano ya Kiuchumi) na Kulia ni Naibu Katibu Mtendaji (Huduma za Jamii na Masuala ya Idadi ya Watu) Bibi Florence Mwanri.
Washiriki wa mkutano wa mwaka wa wachumi na maafisa mipango wakimsikiliza Katibu Mtendaji wa Ofisi ya Rais, Tume ya Mipango, Dkt. Philip Mpango (Hayupo pichani).
Washiriki wa mkutano wa mwaka wa wachumi na maafisa mipango wakimsikiliza Katibu Mtendaji wa Ofisi ya Rais, Tume ya Mipango, Dkt. Philip Mpango (Hayupo pichani).
Washiriki wa mkutano wa mwaka wa wachumi na maafisa mipango wakimsikiliza Katibu Mtendaji wa Ofisi ya Rais, Tume ya Mipango, Dkt. Philip Mpango (Hayupo pichani).
Washiriki wa mkutano wa mwaka wa wachumi na maafisa mipango wakimsikiliza Katibu Mtendaji wa Ofisi ya Rais, Tume ya Mipango, Dkt. Philip Mpango (Hayupo pichani).
Washiriki wa mkutano wa mwaka wa wachumi na maafisa mipango wakiwa katika picha ya pamoja na Mgeni Rasmi Balozi Dkt. Matern Lumbanga (katikati waliokaa) pamoja na viongozi waandamizi wa Ofisi ya Rais, Tume ya Mipango.

Picha na SAIDI MKABAKULI

No comments: