ANGALIA LIVE NEWS

Thursday, October 16, 2014

MWANRI: ZINGATIENI WELEDI WAKATI WA KUANDAA MAANDIKO YA MIRADI

Kaimu Katibu Mtendaji wa Ofisi ya Rais, Tume ya Mipango, Bibi Florence Mwanri (aliyesimama) akizungumza na baadhi ya viongozi waandamizi wizara za viwanda na biashara, fedha, uchukuzi, nishati na madini pamoja na viongozi waandamizi kutoka Ofisi ya Rais, Tume ya Mipango, Zanzibar.
Kaimu Katibu Mtendaji wa Ofisi ya Rais, Tume ya Mipango, Bibi Florence Mwanri (aliyesimama) akizungumza na baadhi ya viongozi waandamizi wizara za viwanda na biashara, fedha, uchukuzi, nishati na madini pamoja na viongozi waandamizi kutoka Ofisi ya Rais, Tume ya Mipango, Zanzibar.
Bibi Maryam Khamis (Wapili kulia) Mtaalam wa uchumi kutoka Ofisi ya Rais, Tume ya Mipango, Zanzibar akizungumza katika kikao hicho.
Pichani ni baadhi ya viongozi waliohudhuria Kikao hicho. Kushoto ni Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka ya Ukanda Maalumu wa Uwekezaji nchini (EPZA), Dkt. Adelhelm Meru.
Mmoja wa wajumbe wa kikao hicho, Bw. Aunyisa Meena kutoka Wizara ya Viwanda na Biashara akichangia mada.

Na Saidi Mkabakuli
Wapanga mipango nchini wameaswa kuzingatia weledi wakati wa kuandaa maandiko ya miradi yanayowasilishwa kwa wafadhili ili kuongeza ushindani dhidi ya nchi nyingine wakati wa uwasilishaji wa maombi ya kupatiwa ufadhili wa miradi ya maendeleo.

Wito huo umetolewa na Kaimu Katibu Mtendaji wa Ofisi ya Rais, Tume ya Mipango, Bibi Florence Mwanri wakati alipofanya mazungumzo na viongozi waandamizi kutoka wizara za viwanda na biashara, fedha, uchukuzi, nishati na madini pamoja na viongozi waandamizi kutoka Ofisi ya Rais, Tume ya Mipango, Zanzibar.

Bibi Mwanri alisema kuwa kuna ushindani mkubwa kwa nchi zinazoomba ufadhili wa miradi ya maendeleo hivyo uandishi wa maandiko yenye kuzingatia weledi na viwango vya kimataifa ni msingi katika kuongeza ushindani na kuweza kuwashawishi wafadhili kuvutiwa na miradi husika.

“Katika kukabiliana na ushindani hatuna budi kujikita katika weledi na kuandika maandiko yenye kuweza kuvutia wafadhili ili waweze kuja kuwekeza nchini kwetu, ili tuweze kutimiza ndoto zetu za kuifanya Tanzania kuwa nchi yenye uchumi wa kati kufikia mwaka 2025” alisema Bibi Mwanri.

Mwezi Juni mwaka 2011, Serikali iliandaa Mpango wa Kwanza wa Maeneleo (2011/12 – 2015/16) kwa lengo la kutekeleza Dira ya Taifa ya Maendeleo 2025 ambapo Mpango huu ulihitaji takribani trilioni 40 ili kutekeleza miradi mbali mbali ya maendeleo kwa kipindi cha miaka mitano.

Kwa mujibu wa Mpango huo, vyanzo vya utekelezaji wake ni pamoja na Ubia Kati ya Sekta ya Umma na Sekta Binafsi (PPP); uwekezaji wa kigeni; Hati Fungani kwa Waishio Ughaibuni; Hatifungani za ndani; Hati Fungani katika Masoko ya Nje; Mifuko ya Pensheni na hifadhi ya jamii; na makubaliano ya ushirikiano wa kiuchumi wa nchi zinazoendelea.

No comments: