ANGALIA LIVE NEWS

Monday, October 6, 2014

NOAH INAYODAIWA KUTEKA WANAFUNZI JIJINI DAR YAZUA KIZAAZAA

Hofu kubwa imewakumba wakazi wa Wilaya za Ilala na Temeke, jijini Dar es Salaam kufuatia kuzagaa kwa uvumi wa kuwapo wahalifu wanaotumia gari aina ya Noah yenye rangi nyeusi na kupita shuleni na kuwateka watoto na kwenda kuwachuna ngozi. 
Uvumi huo ulianza kuzagaa Oktoba Mosi, mwaka huu, maeneo tofauti katika wilaya hizo, hususan katika shule za msingi.Walimu wakuu wa baadhi ya shule walithibitisha kusikia uvumi huo na hivyo, kuwapa tahadhari wanafunzi. 
Waandishi wa habari w walitembelea Shule za Msingi Vituka, Yombo na Bwawani, ambako wanafunzi na walimu wa shule hizo wameingiwa na wasiwasi mkubwa. 
Wasiwasi huo ulizuka baada ya gari aina ya Noah lililotumiwa na waandishi wa NIPASHE kufika katika shule hizo kwa ajili ya kupata taarifa zaidi. 
Mwalimu Mkuu Msaidizi wa Shule ya Msingi Vituka, Flora Mbaule, alisema taarifa kuhusu gari hilo amezisikia kutoka kwa watu. 
“Siwezi kuthibitisha kuwapo kwa tukio hilo. Ila nimesikia kuwa kuna Noah nyeusi, ambayo inabeba wanafunzi sijui kama wanawapa lifti au kuwarubuni kwa vyakula,” alisema Mbaule. 
Alisema Oktoba Mosi, mwaka huu, walipokea barua kutoka kwa Afisa Elimu wa Manispaa ya Temeke, Onorina Mumba, iliyosainiwa na Mkurugenzi wa Manispaa hiyo, Photdas Kagimbo, inayowaelekeza wawatangazie wanafunzi kwamba, wachukue tahadhari kupanda gari aina ya Noah au la aina yoyote. 
Alipoulizwa na NIPASHE jana, Ofisa Elimu wa Manispaa hiyo, Mumba alisema kwenye barua walizowandikia walimu wakuu wa shule hizo hawakutamka magari aina ya Noah na kwamba, uvumi kuhusu magari hayo ni uzushi. 
Alisema walichokieleza ni kuwataka walimu wakuu wawatangazie wanafunzi kwamba, wanapotoka shule wasiwe wanasambaa hovyo na kwenda mitaani, badala yake waende moja kwa moja nyumbani. 
Mkurugenzi wa Manispaa hiyo, Kagimbo alipoulizwa na NIPASHE jana, alisema hana uhakika kama barua hiyo ilielezea suala la Noah, lakini akasema yaliyodaiwa katika uvumi huo ni uzushi. 
“Yaliyozungumzwa ilikuwa ni uvumi, hakukuwa na ukweli wowote,” alisema Kagimbo.Afisa Elimu Mkoa wa Dar es Salaam, Raymond Mapunda, alipoulizwa na NIPASHE jana kuhusiana na hili, hakukiri wala kukanusha kuhusiana uvumi huo. 
“Siwezi kusema nina taarifa au sina. Muulize afisa elimu wa Manispaa ya Temeke badala ya kuniuliza mimi,” alisema Mapunda.
Baadhi ya wanafunzi waliohojiwa na NIPASHE walithibitisha kutangaziwa na walimu wao kuhusu kuchukua tahadhari hiyo na kwamba, taarifa hizo waliwafikishia pia wazazi nyumbani. 
“Nilipokea barua kutoka manispaa jana (Oktoba mosi) kwamba, niwatangazie wanafunzi taarifa hizo za wanafunzi kutekwa. Ila hapa shuleni kwangu hakuna aliyekumbwa na tukio hilo,” alisema Mbaule. 
Alisema alipata taarifa za wanafunzi watatu wa Shule ya Msingi Vituka kupotea Jumapili ya Septemba 28, mwaka huu na kusema hawakurudi tangu walipotoka nyumbani asubuhi. 
Aliwataja wanafunzi hao kuwa ni Hawa Alex, Angle Alex na Lemisa Peter, ambao wote wanaishi katika nyumba moja.Hata hivyo, alisema kupotea kwa watoto hao hakuhusiani na gari hilo, kwani walipotea katika siku, ambayo haikuwa ya shule. 
NIPASHE ilifika katika nyumba, ambayo wanafunzi hao wanakoishi na kuzungumza na ndugu yao, aliyejitambulisha kwa jina la Diana Mwakyusa. 
Mwakyusa alisema wanafunzi hao waliaga kwamba, wanakwenda kanisani, lakini hawakurudi hadi Jumatano ya Oktoba mosi, mwaka huu wakisema walikuwa Mlandizi. 
“Mama, ambaye ni mlezi wa watoto hawa amesafiri leo (Oktoba 2) kuelekea Mbeya kwa kuwarudisha watoto hao baada ya kulalamika kwa muda mrefu kuwa wanataka kurudi kwao,” alisema Diana. 
NIPASHE pia ilitembelea Shule ya Msingi Yombo na kuzungumza na wazazi, ambao walikuwa karibu wakifanya biashara eneo hilo. 
Mmoja wa wazazi, ambaye ni mfanyabiashara wa bidhaa ndogondogo, Mwajabu Omari, alisema uvumi huo wameusikia mtaani ingawa hawajauthibitisha.
Mwalimu Mkuu wa Shule hiyo, Christina Kasyupa, alisema kumekuwapo na uvumi huo ingawa hakuna mwanafunzi yeyote wa shuleni hapo aliyekumbwa na tatizo hilo wala mzazi kulalamika. 
“Mngekuja siku ya jana (Oktoba Mosi) sidhani kama mngeweza kupita na gari yenu, ingepona, kwani wazazi walikuwa wameweka kambi hapa shuleni na shule za jirani. Pia polisi walifika eneo hili, ingawaje wao wanasema walifika kufuatilia suala la kikosi cha uhalifu cha mbwa mwitu,” alisema Kasyupa. 
Kamanda wa Polisi Mkoa wa Ilala, Mary Nzuki, alithibitisha kuusikia uvumi huo, lakini akasema hakuna kesi yeyote, ambayo imeripotiwa katika ofisi yake.“Uvumi huo nimeusikia na umezagaa sana mitaani. Lakini sijapokea kesi yoyote ya mtoto kutekwa na Noah hiyo,” alisema Nzuki. 
Naye Kamanda wa Polisi Mkoa wa Temeke, Kihenye Kihenye, alisema hana taarifa za wanafunzi wa shule za msingi kutekwa.
CHANZO: NIPASHE

No comments: