ANGALIA LIVE NEWS

Thursday, October 9, 2014

Prof. Lipumba kunguruma Mtwara

Aandaliwa mapokezi makubwa
Baada ya serikali kutangaza kuruhusiwa kwa mikutano ya hadhara katika mikoa ya Kusini ya Mtwara na Lindi kwa takribani mwaka mmoja, Chama cha Wananchi (CUF) Mkoa wa Mtwara, kinafanya maandalizi ya kumpokea Mwenyekiti wa chama hicho, Prof, Ibrahim Lipumba, ambaye atafanya mikutano ya hadhara miwili mjini Mtwara.

Kiongozi huyo ambaye yupo mkoani humo kwa ziara ya kikazi, anatarajiwa kuwasili Mtwara mjini Oktoba 13, mwaka huu.

Akizungumza na NIPASHE katika ofisi za CUF mjini Mtwara, Katibu wa chama hicho mkoani humo, Said Kulaga, alisema anaandaa barua kwa ajili ya kuomba kibali polisi cha mapokezi ya kiongozi huyo.

“Mwenyekiti (Lipumba) yupo katika mkoa wetu kwa ziara ya kikazi, tunaishukuru serikali kufungua mikutano, naandaa barua kwa ajili ya kuomba kibali kwa OCD cha kumpokea Mwenyekiti wetu, naamini tutakubaliwa kwa sababu tamko limetoka ” alisema na kuongeza:


“Tutakuwa na mapokezi makubwa ya pikipiki, magari, bajaji pamoja na magari na yatakayoanzia Ghalani Mikindani saa 2:00 asubuhi na baadaye atazindua ofisi ya chama mkoa.”

Alisema baada ya uzinduzi huo, Prof Lipumba atazindua matawi matatu ya chama hicho kabla ya kiongozi huyo kufanya mkutano wa adhara Ghalani Mikindani.

Kulaga, alisema siku ya pili ya ziara yake, Prof. Lipumba atakuwa na mkutano na viongozi wa CUF wa wilaya, jumuiya za kata na matawi yote ya chama hicho, na kisha atahutubia wananchi wa Mtwara mjini katika uwanja wa Mashujaa.

Akizungumza na NIPASHE kwa njia ya simu, Mkuu wa Mkoa wa Mtwara, Kanali Mstaafu Joseph Simbakali, alisema: “Sina neno juu ya tamko hilo maana tayari serikali imetangaza kuruhusu mikutano na hakuna serikali mbili,” alisema na kuongeza:

“Mimi nitakupa maneno, lakini nimeazima ya Baba wa Taifa, ‘uhuru wa kujitawala bila demokrasia ni udikiteta, lakini uhuru bila nidhamu ni fujo.”

Alisema kuruhusiwa kwa mikutano hiyo isiwe mwanzo wa fujo, matusi na kejeli na kuonya kuwa endapo mtu atajihusisha na uvunjaji wa amani na kuleta vurugu sheria itachukua mkondo wake.
 
CHANZO: NIPASHE

No comments: