ANGALIA LIVE NEWS

Thursday, October 9, 2014

MPENZI WA ZAMANI WA MPENZI WAKO ANAPOKUWA KIRUSI HATARI!



Niwazi kila mmoja wetu ana historia katika maisha yake ya kimapenzi. Huenda mpaka sasa wewe msomaji ulishawahi kuwa na uhusiano na watu zaidi ya mmoja.

Wala siyo ajabu! Yawezekana pia kati ya wale uliowahi kuwa nao wapo uliomwagana nao kwa shari lakini wapo pia ulioachana nao kiroho safi.

Jambo ambalo leo nataka kulizungumzia ni hili la mtu kuendelea kuwa na mawasiliano na mpenzi wake wa zamani eti kwa sababu waliachana kwa heri.

Huenda mlifika mahali mkaona bora kila mtu awe na maisha yake na hatimaye wewe ukampata mwingine ambaye anaonesha kukupenda na yeye bado yuko singo au amepata kiburudisho kingine. Swali ni je, unaona ni sahihi kuendelea kuwasiliana na ‘ex’ wako kama kawaida?

Unadhani mpenzi wako wa sasa akijua anatakiwa kuchukulia poa tu? Huenda nikawa na mawazo tofauti lakini ninachojua mimi ‘ex’ wako ni kirusi hatari kwenye uhusiano wako wa sasa. Hata kama mliachana vizuri, kuna haja gani kuendelea kuwasiliana naye na wakati mwingine kukutana?

Sisemi kwamba ukishaachana naye basi muwe maadui, lahasha! Ninachomaanisha hapa ni kwamba, ule ukaribu wenu ni lazima uyeyuke. Kama ulikuwa na namba yake, ni vyema ukaifuta na ukamtaarifu kabisa kwamba uko na mtu mwingine hivyo yeye hana nafasi tena kwenye maisha yako.

Ukijaribu kufuatilia sana, wapo ambao waliachana na wapenzi wao lakini bado wanaendelea kuwasiliana kwa siri sana na kusaidiana kama ilivyokuwa zamani. Hebu jiulize, mpenzi wako akijua atakufikiriaje?
Kama kweli mlikubaliana kuachana baada ya kuwa pamoja kwa muda mrefu, unadhani kwa ukaribu wenu hakuna siku shetani atawapitia? (sijui awapitie muende wapi).

Naandika makala haya kwa ushahidi. Wapo ambao waliachana na wapenzi wao, wakaendeleza ukaribu kwa siri sana na wakawa wanachepuka. Si wanajuana, ni suala la kukumbushia tu!

Mbaya zaidi wapo ambao baada ya kuendeleza ukaribu wao walijikuta wakinogewa tena na kuamua kurejeana licha ya kila mmoja kwa muda huo kuwa na uhusiano mwingine.Mimi nadhani inapotokea umeachana na mpenzi wako na ukapata mtu mwingine, wa zamani epukana naye ili kujenga mazingira ya kumfanya mpenzi wako wa sasa asikufikirie tofauti.

Nikuambie tu kwamba kwa namna baadhi ya watu walivyo na wivu ukikutana na mpenzi wako wa zamani kisha ukamuonesha tabasamu tu, ‘mtu’ wako hawezi kuchukulia poa, labda awe ni bwege.
Hawezi kuchukulia poa kwa kuwa anaweza kuhisi bado mnapendana na kuachana kwenu ilikuwa bahati mbaya tu. Matokeo yake atakuwa na wewe lakini atakuwa hana amani akihisi ipo siku mnaweza kumaliza tofauti zenu na mkarudiana.

Nini cha kufanya ili mpenzi wako wa zamani asikuharibie uhusiano wako wa sasa?
Iko hivi, baadhi wana roho mbaya sana, unaweza kuachana naye leo na ukawa umepata mtu mwingine lakini kwa kuwa hataki kukuona mwenye furaha, atataka kukutibulia.

Unaweza kushangaa hata kama hujampa namba yako ya simu, ataitafuta kisha ataanza kukupigia simu usiku au kukutumia sms zinazoweza kumfanya mpenzi wako aamini bado mnaendelea.
Anaweza pia akikutana na wewe akaonyesha kukuchangamkia sana kana kwamba kuna kitu kinaendelea.

Unachotakiwa kufanya wewe ni kumtahadharisha kwamba una mtu wako na hatafurahi kuona mnaendelea kuwa karibu kwa namna yoyote.Mtake asahau yaliyopita na achukulie kama vile hamjawahi kuwa wapenzi. Akikupigia simu au kukutumia sms kuwa mkali na ikiwezekana umshirikishe mpenzi wako ili ajue huyo ‘ex’ wako anakufanyia visa ili kukuharibia.

Ukikutana naye msalimie lakini yasiwepo mazungumzo ya ziada. Mwisho wewe mwenyewe unatakiwa kujaribu kumsahau kabisa. Utafanikisha hilo kwa kujaribu kusahau mazuri aliyowahi kukufanyia na kukumbuka mabaya aliyokutendea.Kumbuka una kila sababu ya kuulinda uhusiano wako wa sasa kwa gharama yoyote hivyo usikubali mpenzi wako wa zamani akakuharibia.

GPL

No comments: