ANGALIA LIVE NEWS

Tuesday, October 21, 2014

‘Tanzania hakuna maabara kupima ebola’

Dar/Mwanza. Wizara ya Afya na Ustawi wa Jamii imesema Tanzania haina maabara yenye uwezo wa kuthibitisha vipimo vya ebola hivi sasa na kwamba inapotokea mtu kudhaniwa kuathiriwa na virusi vya ugonjwa huo, vipimo vyake ni lazima vithibitishwe nje ya nchi.
Hata hivyo, wakati kauli hiyo ikitolewa na Msemaji wa Wizara ya Afya, Nsachris Mwamaja jana, Kaimu Mganga Mkuu wa Mkoa wa Mwanza, Dk Yusuf Bwire amesema vipimo hivyo vinaweza pia kupatikana Mbeya.
Dk Bwire alikuwa akizungumzia vipimo vya mkazi wa Sengerema, Mwanza, Salome Richard (17) aliyefariki dunia katika Hospitali Teule ya wilaya hiyo akihofiwa kuwa na dalili za ugonjwa huo.
“Kuna vitu viwili hapa, kwanza majibu ya vipimo vya ebola kwa mgonjwa anayedaiwa kufa na ugonjwa huo bado havijatoka, lakini taarifa zilizopo vipimo hivyo vinaweza kufanyika Nairobi au Mbeya. Tunaweza kupata majibu wiki ijayo au Jumatano kama vitapelekwa huko,” alisema Dk Bwire.
Kuhusu kutokuwapo kwa vipimo hivyo, Mwamaja alisema Wizara ya Afya imeliweka wazi na Mganga Mkuu wa Serikali ameshaeleza mkakati wa kuziongezea uwezo maabara kadhaa nchini kwa kushirikiana na Shirika la Afya Duniani (WHO) ili zifikie viwango vya kupima magonjwa ya hatari na ya milipuko ikiwamo ebola.
“Tunachoeleza mara kadhaa ni kwamba sisi tuna uwezo wa kupima, ila ili kuthibitisha vipimo vya ebola ni lazima tupeleke vipimo hivyo Kemri Nairobi. Hiyo ndiyo hali halisi iliyopo kwa sasa,” alisema Mwamaja.
Awali, Septemba mwaka huu, Waziri wa Afya, Dk Seif Rashid alisema Serikali inafanya mpango wa kuimarisha maabara ya Taasisi ya Utafiti wa Magonjwa ya Binadamu (NIMR) ili iwe na uwezo mkubwa wa kupima magonjwa mengi pamoja na ebola na ukarabati wake unatarajiwa kugharimu Dola za Marekani 560,000.
Akizungumzia vipimo vya mgonjwa wa Sengerema, Mkuu wa Mkoa wa Mwanza, Evarist Ndikilo alisema jana kuwa japo haijathibitishwa kuwapo kwa ebola mkoani mwake, hatua za tahadhari za kupambana nao zimeshaanza kuchukuliwa na kuwatahadharisha wakazi wa Mwanza kuwa makini; “mtu anapojisikia homa aende haraka kituo cha afya”.
Alisema tayari watumishi wa afya 822 wameshapata mafunzo kupambana na ugonjwa huo na kuiagiza Bohari Kuu ya Dawa (MSD) mkoani Mwanza kusambaza dawa kwenye hospitali zote za wilaya.
Alisema tayari amepokea jozi 150 za vifaa maalumu kutoka Wizara ya Afya na Ustawi wa Jamii kwa ajili ya wahudumu na kutenga vyumba maalumu kwenye hospitali za wilaya kwa ajili ya wagonjwa watakaogundulika.
Mwananchi

No comments: