Arusha. Mtu anayedaiwa kuwa kiongozi mkuu wa kundi la watu wanaohusika na matukio ya milipuko ya mabomu na umwagiaji tindikali viongozi wa dini ameuawa kwa kupigwa risasi na jeshi la polisi.
Mtuhumiwa huyo Yahaya Hassan Omari Hela (31), maarufu kwa jina la Yahaya Sensei, mkazi wa Mianzini jijini Arusha aliuawa kwa kupigwa risasi mguuni na makalioni.
“Mtuhumiwa aliuawa saa 5.30 usiku wa Oktoba 19, alipojaribu kuwatoroka polisi waliokuwa wakimsafirisha kwenda nyumbani kwao Chemchem wilayani Kondoa kuonyesha alikoficha mabomu,” alisema Kamanda wa Polisi Arusha, Lebaratus Sabas alipozungumza na waandishi wa habari jana.
Alisema Hela alikuwa mwalimu wa karate na judo na alikuwa muasisi na kinara wa matukio ya ugaidi yaliyojitokeza Arusha, Zanzibar, Mwanza na Dar es Salaam.
“Mtuhumiwa alikamatwa akiwa mkoani Morogoro Oktoba 6 mwaka huu na kusafirishwa hadi Arusha,” alisema.
Sabas alisema mtuhumiwa alikiri kuhusika kwenye matukio kadhaa ya kigaidi na kukubali kwenda kuwaonyesha polisi yalipo baadhi ya mabomu yaliyofichwa huko Kondoa.
“Polisi waliokuwa wakimsafirisha walilazimika kumpiga risasi kwenye mguu na kalio la kulia baada ya kujaribu kutumia uzoefu wake wa judo na karate ili kukabiliana nao kwa nia ya kutoroka.
“Alifariki wakati akipatiwa matibabu katika Hospitali ya Mount Meru alikopelekwa kwa matibabu,” alisema Kamanda Sabas.
Kamanda Sabas ambaye hata hivyo hakukidhi kiu ya waandishi kuhusu mazingira ya kifo cha mtuhumiwa huyo alidai, marehemu Yahaya alikiri kuhusika na tukio la bomu lililolipuka katika Kanisa la Mtakatifu Joseph Mfanyakazi, eneo la Olasiti Mei 5, mwaka jana.
Katika tukio hilo, watu watatu walipoteza maisha huku zaidi ya 62 wakijeruhiwa.
Pia alidai mtuhumiwa huyo ndiye kinara wa mlipuko wa bomu katika mkutano wa Chadema uliokuwa ukifanyika viwanja vya michezo vya Soweto Arusha, Juni 15, mwaka jana, watu wanne walipoteza maisha huku zaidi ya 60 wakijeruhiwa.
Tukio jingine Kamanda Sabas alisema ni lile la Julai 11, mwaka jana, mtuhumiwa na wenzake kadhaa walimmwagia tindikali usoni Sheikh Said Juma Makamba.
Februari 12, mwaka huu, mtuhumiwa na wenzake pia walidaiwa kummwagia tindikali Sheikh Hassan Bashir wa msikiti wa Tindigani ulioko eneo la Unga ltd jijini Arusha pamoja na kuhusika na tukio la Februari 28, mwaka huu ambapo yeye na wenzake, walimwagia tindikali Sheikh Mustapha Kiago wa msikiti wa Bondeni, Arusha.
Kamanda alidai kuwa Aprili 13, mwaka huu, mtuhumiwa pamoja na wenzake walihusika na tukio la bomu katika Baa ya Night Park, eneo la Mianzini lililosababisha kifo cha mtu mmoja huku wengine 10 wakijeruhiwa.
Tukio la Aprili 13 mwaka huu pia linadaiwa kuratibiwa na kutekelezwa na mtuhumiwa akishirikiana na wenzake ambapo lilirushwa nyumbani kwa Sheikh Sudi Ali Sudi (37) ambaye ni Mkurugenzi wa Answar Muslim kanda ya Kaskazini.
Mwananchi
No comments:
Post a Comment