Wawakilishi hao walijitambulisha kwa majina ya Deogratius Mandago, Ibrahim Mpazi, Rashid Shaaban, John Tyaba, Gibson Kalishanga, Mwajuma Ally, Frank Kanoni, Magiri Mussa, Isack Nyakubusa, Mwalimu Vitus Lupeche, Obeid Balola, Gaspa Ulaya na Dickson Matata.
Walitoa madai hayo kupitia tamko kutoka Urambo Mashariki kuhusu Mbunge wao, Samuel Sitta, juu ya yaliyojiri katika Bunge Maalumu la Katiba.
Tamko hilo lilisomwa na mwenzao, aliyejitambulisha kuwa ni Mwanaharakati, Nyakubusa, alipozungumza na waandishi wa habari, jijini Dar es Salaam jana.
Alisema wamefuatilia mjadala wa Bunge hilo kwa makini na kwamba, moja ya sababu iliyowafanya wakutane na wanahabari jijini Dar es Salaam, ni kauli iliyotolewa na baadhi ya wabunge, akiwamo Sitta kwamba, maoni ya iliyokuwa Tume ya Mabadiliko ya Katiba iliyoongozwa na Jaji Joseph Warioba siyo ya wananchi, huku akishindwa kuonyesha sehemu na chombo kilichokusanya maoni tofauti na tume hiyo.
“Ndugu Sitta anafahamu fika yeye mwenyewe kama mbunge wetu hajawahi kufanya mkutano hata mmoja jimboni kwetu uwe wa ndani au hadhara akiomba maoni yetu juu ya katiba tunayoitaka,” alisema Nyakubusa.
Alisema Sitta pia anafahamu fika kuwa Tume ya Warioba, kama sehemu ya wajibu wake wa kisheria na kitendaji, ilikwenda jimboni humo kukusanya maoni yao na kwamba, tangu nchi ipate uhuru hadi kufikia jana, hawajawahi kuulizwa maoni juu ya katiba na chombo chochote kisheria zaidi ya tume hiyo.
“Ndiyo kusema, hakuna chombo chochote wala mtu yeyote anayeweza kuja na maoni tofauti na yale tuliyoyatoa kwa Tume ya Mabadiliko ya Katiba na bado akadai anawakilisha maoni ya wananchi,” alisema Nyakubusa.
Alisema wengi wanafahamu kiwango cha juu cha dharau kilichoonyeshwa na Sitta kwa viongozi wa dini kwa kudiriki kuwarubuni baadhi ya wajumbe wa Bunge hilo kutoa tamko kana kwamba, wao ni wawakilishi rasmi wa taasisi kuu za dini za Kiislamu na Kikristo nchini.
“Wote mnafahamu jinsi alivyotumia Bunge Maalumu kuwadhalilisha viongozi wa dini waliotumia uhuru wao wa maoni na wajibu wao kwa waumini kukosoa matumizi mabaya ya kodi za wananchi yanayoongozwa na Ndugu Sitta,” alisema Nyakubusa.
CHANZO: NIPASHE
No comments:
Post a Comment