ANGALIA LIVE NEWS

Monday, November 10, 2014

BAADA YA SITTI KUVUA TAJI LA MISS TANZANIA 2014 MAPYA YAIBUKA

Miss Tanzania 2014 aliyejivua taji Sitti Mtemvu akipata upako kutoka kwa Nabii Yaspi Bendera
Miss Tanzania 2014 aliyevuliwa taji, Sitti Abbas Mtemvu akipanda jukwaani kupata maombi ya Nabii Yaspi Bendera.


Stori: Chande Abdallah, Deogratius Mongela na Musa Mateja wa GPL
TENA! Saa chache tu baada ya Miss Tanzania 2014 aliyezua tafrani la kuchakachua umri kwa kujipunguzia miaka 2 ya kuzaliwa, Sitti Abbas Mtemvu kujisalimisha kwa kujivua taji mwenyewe, mapya yameibuka na Ijumaa Wikienda lina mzigo mkononi!


YAMEIBUKAJE?
Mapya hayo yameibukia ndani ya Kanisa la Revelation Church lililopo Buza–Kipera jijini Dar kwa Nabii Yaspi Bendera ambaye amezungumzia ishu ya Sitti kujivua taji mwenyewe.

HUYU HAPA
“Alikuja kwangu nikamwombea, akapata taji. Hata alipopata alikuja kushukuru, nilimwambia aendelee kudumu kwangu hadi atakapokwenda kwenye taji la dunia (Miss World) lakini hakufanya hivyo, akawa haji tena.

“Hivi, nitoe mfano mmoja. Kama mtu akienda kwa mganga kuomba apewe dawa ili apate ujauzito, akishapata akaenda kwa mganga mwingine kuomba amfanyie dawa ili ujauzito huo usitoke. Je, siku ukitoka nani analaumiwa, mganga wa kwanza au wa pili?


TAFSIRI YAKE HAPA!
Kwa tafsiri rahisi sana ya mazungumzo ya nabii huyo, Sitti alikwenda kanisani kwake akaomba baraka ili ashinde taji la Miss Tanzania, akashinda lakini baadaye alihama kanisa na kwenda kusali kwingine mpaka alipovua taji.

Nabii Yaspi aliandelea kudai kwamba, kama Sitti angeendelea kudumu kwenye kanisa lake na kuombewa maombi ya nguvu, asingevua taji na angefanikiwa kwenda Miss World 2015 ambako pia angetwaa taji la dunia.
Lakini baada ya kutwaa taji alienda kanisa jingine akiwa na taji lake, matokeo yake mambo yakawa magumu mpaka alipolazimika kuvua taji hilo.

KUMBE ALISHAONYWA

Habari nyingine kutoka kwa mtu asiye msemaji wa kanisa hilo zinasema kuwa, baada ya kutwaa taji, Sitti alionywa na Nabii Yaspi kwamba kutaibuka vikwazo katika nafasi yake hiyo lakini alichotakiwa kufanya ni kudumu katika maombi ya kanisa hilo ili vikwazo hivyo vifutike lakini kwa sababu hakufanya hivyo matokeo yake ni hayo!

SITTI AMEFIKAJE HAPA?

Siku chache baada ya Sitti kutwaa Taji la Miss Tanzania 2014 katika shindano lililochukua nafasi ndani ya Ukumbi wa Mlimani City, Dar, Oktoba 11, mwaka huu, yaliibuka madai kwamba, mrembo huyo alichakachua umri akidai ana miaka 23 wakati ana miaka 25.


Sheria za Miss Tanzania, mrembo mwenye miaka 25 haruhusiwi kushiriki mashindano hayo.
Katika madai hayo, ilisemekana kwamba, mrembo huyo alizaliwa Mei 31, 1989 kwenye Hospitali ya Aga Khan jijini Dar. Lakini yeye cheti alichokipeleka kwenye Kamati ya Miss Tanzania akidai alikipata kwa Wakala wa Usajili, Ufilisi na Udhamini (Rita) kilionesha mlimbwende huyo alizaliwa Mei 31, 1991 hivyo ana miaka 23.

PASPOTI NDIYO CHANZO
Mazito yote yaliyompata Sitti, chanzo ni hati yake ya kusafiria (paspoti) ambayo ilibandikwa kwenye mitandao ya kijamii ikionesha mrembo huyo ambaye ni binti wa Mbunge wa Jimbo la Temeke kwa tiketi ya CCM, Abbas Mtemvu, alizaliwa Mei 31, 1989.

KESI BADO MBICHI!
Katika barua yake kwa Kamati ya Miss Tanzania aliyoiandika Novemba 5, mwaka huu na kufika ofisi za kamati hiyo, Novemba 6, mwaka huu, saa 9:25 mchana, Sitti alisema ameamua kwa hiyari yake kuvua taji hilo baada ya kusakamwa na vyombo vya habari kwamba alichakachua umri.

“Leo nalivua taji rasmi nililopewa na binadamu lakini alilonipa mwenyezi Mungu bado ninalo. Mwisho naomba radhi Watanzania wote kwa uamuzi huo niliochukua,” ilisomeka sehemu ya barua hiyo ya Sitti.
Nafasi ya Sitti imetwaliwa na mshindi wa pili, Lilian Kamazima aliyetokea Arusha.

Hata hivyo, kuna ushahidi wa kutosha kutoka Rita na Idara ya Uhamiaji kwamba, umri wa miaka 25 uliopo kwenye paspoti ya kusafiria ya Sitti ambayo imesambaa kwenye mitandao ya kijamii ndiyo sahihi!
Kwa maana hiyo, Sitti kujivua taji anakuwa amemalizana na kesi ya wananchi waliokuwa wakimkomalia, lakini kesi ya kughushi cheti cha kuzaliwa bado inamhusu kwa sababu kwa sheria za Tanzania, mtu akithibitika kudanganya umri kifungo chake ni miaka 3 jela na jamhuri inaweza kumshtaki kwa kusimamia kesi yenyewe.

NI HISTORIA KWA MISS TANZANIA
Hii ni mara ya kwanza katika historia ya mashindano ya Miss Tanzania yaliyoanza nchini mwaka 1994 baada ya kufutwa awali ambapo mshindi wa kwanza anajivua taji ingawa pia haikuwahi kutokea mshiriki kuvuliwa taji kwa kosa lolote lile.

ILIWAHI KUTOKEA MISS KUDANGAYA SHULE

Mwaka 1995, Miss Tanzania alikuwa ni Emily Adolf, mwanafunzi wa kidato cha pili Shule ya Sekondari ya Central, Dodoma. Ushindi wake ulileta malumbano baada ya kubainika alishiriki akiwa mwanafunzi huku akidai alimaliza. Alifukuzwa shule lakini hakuvuliwa taji.

WEMA ALINUSURIKA NA UMRI
Mwaka 2006, Miss Tanzania, Wema Isaac Sepetu naye alinusurika kuvuliwa taji kwa madai kwamba alidanganya umri wake. Wema alidaiwa kushiriki mashindano hayo akiwa na miaka 17, yeye akadai ana 18 lakini vuguvugu la wananchi kumkomalia miaka hiyo haikuwa kama sasa.

4 comments:

Anonymous said...

Hii ndiyo sababu nchi za Kiafrika haziwezi kuendelea.

Anonymous said...

Sasa huyo kiongozi wa dini anashabikia uongo wa umri? Basi dunia imekwisha!

Anonymous said...

Hivi kwani ni Africa tu ndo miujiza ya MUNGU inatokea? Tatizo si uwepo wa MUNGU bali ni udanganyifu wa hawa "watumishi wa MUNGU". Kila kitu MUNGU....Watanzania tuamke na tuache huu ulimbukeni wa kumtegemea MUNGU kwenye kila jambo wakati yeye aliacha walimwengu wajitawale na wafanye maamuzi yao bila yeye kuwaingilia. Ni vyema kuwa na imani na kuishi kwa miiko ya dini zetu mbalimbali ila si busara kufanya dini kama biashara ambayo inatoa njia mkato kwa maendeleo au shida zetu mbalimbali

Anonymous said...

I absolutely agree with you. Waafrica na huyu mungu, mpaka miss Tanzania? Weird.