Dar es Salaam. “Mama yangu ameshanitoa mimba mara tatu akidai kuwa mimi ni mgonjwa wa akili sitaweza kumnyonyesha mtoto wala kumtunza, lakini napenda kuwa na mtoto,” anasema binti wa umri wa miaka 16 (jina linahifadhiwa), anayeishi eneo la Iyunga mkoani Mbeya.
Anadai alipopata mimba ya kwanza alipokuwa darasa la tano mwaka 2011, mama na shangazi yake walibaini na kuamua kumpeleka kwa mganga wa jadi kumtoa kwa kutumia dawa za kienyeji.
“Nakumbuka siku hiyo baada ya kuinywa dawa hiyo inayosaidia kutoa mimba, niliumwa sana tumbo kiasi cha kuhisi nakufa, lakini baada ya kutoka nilipewa dawa nyingine na mganga nikapata nafuu,” anasema mtoto huyo.
Mtoto huyo ambaye amehitimu elimu ya msingi katika Shule ya Msingi Ikuti mkoani Mbeya, anadaiwa alipokuwa na umri wa miaka saba, aliugua ugonjwa wa degedege.
“Toka wakati huo, akili yake haijakaa sawa kuna kipindi anakuwa kama anarukwa na akili hali ambayo ndugu na hata mama yake wanaona kuwa akili zake hazijakaa sawa. Wanamchukulia kama ana kichaa cha msimu,” anasimulia Shangazi yake Mary Shitindi ambaye anaishi na binti huyo kwa sasa Msasani jijini Dar es Salaam.
Binti huyo ambaye kwa sasa ni mjamzito tena, anasema safari hii alimkatalia mama yake asimpeleke kutolewa mimba yake kwa kuwa anapenda kupata mtoto.
Inadaiwa baada ya kupata ujauzito, walimu shuleni kwake hawakuweza kubaini na hivyo kutoonekana kwake shuleni mara kwa mara, walijua ni kutokana na hali ya afya yake.
Mwandishi: Sasa Jesca (si jina halisi), nani ambaye huwa anakutia mimba ambazo unasema hii ni ya tatu?
Jesca: Rafiki yangu anaitwa John, ananipenda sana na ameahidi kunioa.
Mwandishi: Lakini umri wako haukuruhusu wewe kupata mtoto sasa wala kuolewa, kwanini umeamua kubeba mimba ulipomaliza shule ya msingi tu, kwani hutaki kuendelea kusoma sekondari?
Jesca: Mimi kuna wakati huwa ninaumwa maradhi kama ya kurukwa na akili, kwa hiyo mama yangu ananichukulia kuwa ninakichaa cha msimu, anaona sistahili kufanya kitu chochote cha maendeleo.
Hata darasa la saba lenyewe nimemaliza kwa shida tu, alikuwa hataki niende shuleni akiogopa huenda kichaa kikanipanda nikiwa huko.
Mwandishi: Sasa uliwezaje kusoma mpaka ukahitimu darasa la saba wakati mama alikuwa anakuzuia kwenda shuleni.
Jesca: Rafiki yangu John ndiye aliyenisaidia kwenda kuwaeleza walimu matatizo yangu.
Walimu walichukua hatua ya kumwita mama na kuzungumza naye na walimuahidi watanisaidia pindi hali ikinibadilikia nikiwa shuleni.
Hata hivyo, hakuwaamini, akashikilia msimamo wake. “Aliwaambia anaogopa nisije nikapotea, kichaa changu kikipanda naweza kwenda mahali nisikokujua.”
Mwandishi: Ilikuwaje mpaka ukapata mimba!
Jesca: Ni bahati mbaya tu, siku moja nilikuwa na John nyumbani kwao, wazazi wake hawakuwepo, aliniita chumbani kwake akanishawishi tufanye naye mapenzi na ndiyo ilikuwa siku yangu ya kwanza kukutana na mwanaume kimwili, basi nikapata mimba!
Msichana Jesca katika simulizi yake, anasema mimba hiyo aliipata akiwa darasa la tano mwaka 2012 “Mama na shangazi walipobaini kuwa nina mimba, waliamua kunitoa na mpaka sasa wameshanitoa mimba mbili, hii niliyonayo ni ya tatu, wanadai kuwa nina kichaa cha msimu sitaweza kumlea mtoto wala kumnyonyesha.
“Safari hii siitoi tena nitaitunza mpaka nijifungue, John ameahidi kunitunza kwa kuwa ananipenda na bahati nzuri sasa hivi amepata kazi, tutamtunza mtoto wetu tukimpata. Ndiyo maana nilimuomba shangazi anichukue nije naye huku Dar,” anasema Jesca.
MAMA YAKE JESCA:
Alipozungumza na mwandishi kwa simu kutokea Mbeya, mama yake Jesca alisema: “Ni kweli Jesca ana mimba, lakini mimi ninahofu, sijui kama atajifungua salama. Mwanangu huyu ni mgonjwa wa akili na sijui ni mwanaume gani mwenye akili mbovu aliyediriki kumpatia mimba.
Ugonjwa wake ukimjia kama ana mtoto anaweza hata kumtupa au kumfanyia kitu kibaya, ndiyo hofu yangu.”
Anasema alikuwa na mpango wa kumpeleka kijijini kwao Msangano wilayani Mbozi kwa mganga wa kienyeji akamtoe mashetani aliyotupiwa, lakini bahati mbaya shangazi yake amemchukua.
“Sasa hivi akili imemrudia kidogo na anajitambua kuwa ana mimba, hataki tuitoe mimba, nilisikia kuna mganga Msangano nikataka nimpeleke huko akatusaidie kuyatoa hayo mashetani, lakini amekataa,” anasema mama huyo.
Alipoulizwa kwa nini hakutaka kumpeleka hospitali na kung’ang’ania tiba za kienyeji alijibu kuwa: “Ugonjwa wake si wa kutibiwa hospitali, huo unatibiwa kienyeji tu.”
Akizungumzia maisha ya Jesca, John (25) anayedaiwa kumpatia mimba Jesca, anasema ni ya dhiki na familia yao inaamini sana ushirikina.
Anasema kama binti huyo angepatiwa tiba mbadala ya hospitali, angeweza kupona.
Lakini wazazi wake wanaamini kuwa ametupiwa mashetani ambayo humsumbua kila ifikapo mwisho wa mwezi yanamfanya arukwe na akili.
“Jesca ana matatizo ya malaria kali ambayo humpata mara nyingi na humsababishia kuchanganyikiwa, binafsi nilishampeleka hospitali ya Rufaa Mbeya akabainika kuwa ana malaria kali, alitibiwa na nikashauriwa niwe nampeleka mara kwa mara kupima malaria ili apate tiba na hana ugonjwa wa akili kama inavyodaiwa na mama yake,” anasema John.
Kasumba chafu za kuendekeza imani za kishirikina zinachangia vitendo vya ukatili na mauaji dhidi ya watoto kwa njia ya utoaji mimba.
Mwenyekiti wa Pro-life Tanzania, Emil Hagamu amewahi kusema kuwa katika jamii ambayo bado ina kasumba ya kuendekeza imani za kishirikina, waathirika wakubwa huwa ni wanawake na watoto wa kike.
Kwa mfano, mama yake Jesca angempeleka mwanaye hospitali angeweza kupatiwa tiba mbadala.
Mkurugenzi Mtendaji wa Chama cha Waandishi wa Habari Wanawake Tanzania (Tamwa), Valerie Msoka anasema huo ni ufinyu wa mawazo na uelewa.
Na ni kosa kubwa lililojikita katika ubaguzi na unyanyasaji wa kijinsia wa kumzuia mtoto kwenda shule na kumshinikiza atoe mimba tena kwa njia isiyo salama, inahatarisha maisha yake.
Usu Malya, mwanaharakati wa Mtandao wa Jinsia Tanzania (TGNP), anasema unyanyasaji wa kijinsia haufanywi na wanaume ama watu baki tu, bali hata ndani ya familia kama inavyoonekana kwa binti Jesca ambaye anaendelea kunyanyaswa na mama yake kwa kumnyima haki zake za msingi.
Licha ya kufanyiwa ubaguzi hata wa kimajukumu unaowapa nafuu ya kujisomea na kupumzika watoto wa kiume huku wa kike wakielemewa na majukumu, bado watu wengi wanakosea kudhani kuwa watoto wa kike hawana akili darasani na wanaogopa masomo magumu kama ya Sayansi na Hisabati.
“Ukweli ni kuwa wanashindwa kujengewa uwezo, kwa mfano, Jesca kama walimu waliweza kuwa radhi kumsaidia katika mazingira ya aina yoyote ile, angepewa nafasi si ajabu angeweza kufika mbali kimasomo,” anasema Sabina Nzowa mkazi wa Iwambi, Mbeya.
Ifahamike kuwa mtoto yeyote awe wa kike au wa kiume ana haki ya kupata elimu na kutobaguliwa.
Sheria za Tanzania zinalinda haki za mtoto tangu kutungwa kwa mimba.
Kitabu kiitwacho “Haki za Mtoto” kilichotolewa na Kituo cha Msaada wa Sheria kwa Wanawake (WLAC), Toleo la Mwaka 2008, kinasema katika uk. 3, “Sheria ya Kanuni ya Adhabu, Sura ya 16, inasema ni kosa la jinai kwa mtu kutoa mimba…. Utoaji mimba unavunja haki ya kuishi ya mtoto ambaye hawezi kujitetea.”
Ukatili aliofanyiwa Jesca umemfanya hata jamii inayomzunguka kumbagua kutokana na kukosa haki ya matibabu stahiki, hali iliyomfanya aonekane kichaa mbele ya jamii.
Mazingira ya ubaguzi, ukatili na unyanyasaji dhidi ya wanawake na watoto katika jamii, ndiyo yameifanya Tamwa na taasisi washirika kuamua kufanya utafiti maalumu kuhusu hali ya ukatili na unyanyasaji wa kijinsia nchini.
Mwalimu Victoria Nzunda, anasema bado kuna kazi ya kutoa elimu ya malezi na makuzi kwa wazazi mijini na vijijini.
“Huyu mama kama angekuwa na elimu mbadala, angeweza kumsaidia mtoto wake kwa njia nzuri badala ya hii ya kumhatarishia maisha kwa kumtoa mimba na kushindwa kumpeleka hospitali ili kubaini maradhi yanayomsumbua,” anasema Victoria.
Anasema umefika wakati sasa wa kutunga sheria mbadala itakayowabana watu wanaokwamisha maendeleo kwa kisingizio cha ushirikina.
Mwananchi
No comments:
Post a Comment