ANGALIA LIVE NEWS

Sunday, November 9, 2014

Western Jazz ilivyotesa na mtindo wa Saboso katika muziki

Tabora. Bendi ya Western Jazz ilikuwa kongwe miongoni mwa bendi za wakati wake na ilianzishwa mwaka 1959, kabla ya nchi yetu haijapata Uhuru.
Umaarufu wa bendi hiyo ulipanda zaidi baada ya wimbo wake wa Vigelegele kuibwa na bendi kongwe kutoka Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo, Soukos Stars waliokarabati na kuuimba upya. Hali iliyo iliibua upya hisia za mashabiki wa muziki kwa Western Jazz.
Bendi hiyo ilijipatia umaarufu mkubwa nchini na nje ya mipaka yetu hadi ilipotoweka katika medani ya muziki mwishoni mwa miaka ya 1970.
Pamoja na umaarufu wote huo, historia ya bendi hiyo haiwezi kukamilika iwapo utaliweka pembeni jina la Mzee Idd Nhende, ambaye ndiye aliyepata wazo la kuanzisha Western Jazzo mwaka 1959.
Kwa kuwa wakati huo miji mingi ndiyo ilikuwa imeanzishwa, watu wengi walihamia mijini kutoka maeneo mbalimbali na kujaribu kutafuta wenzao waliotoka sehemu moja na kuwa na vikundi vya kusaidiana hata kuwaunganisha watu wa sehemu hizo.

Wakoloni waliokuwa wakitawala nchi Tanganyika wakati huo, waliigawa katika majimbo. Majimbo hayo baadhi yalikuwa Northern Province, Southern Highlands Province na Western Province
Wanamuziki wa wakati huo walianzisha bendi wakizipa majina ya maeneo hayo waliyotoka, hivyo kama ambavyo waanzilishi wa Rufiji Jazz walitoka Rufiji, ndivyo ilivyokuwa kwa Kilwa Jazz, Ulanga Jazz na kadhalika.
Kwa vile Nhende alitoka Nzega Mkoa wa Tabora uliokuwa katika Jimbo la Magharibi yaani Western Province, naye aliamua kuanzisha bendi ya watu kutoka magharibi, ndipo alipoanzisha Bendi ya Western Jazz, mwaka 1959.
Mzee Nhende aliweza kupata fedha za kuanzishia bendi hiyo baada ya kuuza baadhi ya ng’ombe wa mama yake na kufanikiwa kununua vyombo aina ya Grampian kutoka duka la vyombo vya muziki lililojulikama kama Souza Junior lililokuwepo Mtaa wa Mkwepu, jijini Dar es Salaam.
Wakati huo bendi za aina yake, ilikuwa ni Dar Jazz pekee, ambayo ilikuwa na magita ya umeme. Kufuatia hali hiyo Mzee Nhende akawa na kazi ya kuwatafuta wapigaji, ambapo alimfuata mpiga gita la umeme wa kwanza Haus Dibonde ‘msukuma’, aliyekuwa akipigia Bendi ya Dar Jazz, iliyokuwa chini ya Mzee Muba.
Baada ya hapo akawapata wanamuziki wengine kutoka Bendi ya Ulanga Jazz. Wakati huo chombo cha Banjo kilikuwa muhimu, hivyo akamtafuta mpiga Banjo kutoka Bendi ya Cuban Marimba, ambayo wakati huo ilikuwa na tawi jijini Dar es Salaam lililokuwa chini ya Mzee Mwaipungu.
Mwaka mmoja baadaye alipata uhamisho wa kwenda mji wa Morogoro, akalazimika kuongeza wasanii wengine ili kuimarisha bendi wakati yeye akiwa hayupo.
Alimpata mwimbaji mahiri wakati huo David Makwaya, Ally Rashid (huyu ameacha muziki karibuni akiwa Msondo) na mpiga Saxyphone kutoka Zanzibar.
Kwa bahati mbaya mpiga gitaa Haus akapatwa na kichaa katika mazingira yaliyohusishwa na ushirikina kutokana na ushindani mkubwa wa bendi uliokuwepo, hivyo walifuatwa wanamuziki watatu kutoka Tabora Jazz.
Wanamuziki hao walikuwa wametoka pamoja katika bendi iliyokuwa na makazi huko Mwanza, ambayo iliitwa Kimbo Twist Band na kuhamia Tabora Jazz. Waliochukuliwa kutoka Tabora Jazz kwenda Western Jazz walikuwa ni Rashid Hanzuruni, Kassim Ponda na Omar Kayanda.
Baada ya kazi nzuri, Rashid Hanzuruni ambaye alikuwa mkung’utaji wa gitaa la solo, naye akarukwa na akili katika mazingira yaleyale ya mpiga solo wa kwanza Haus Dibonde.
Bendi ikalazimika kumrudisha Hanzuruni Tabora ambako alikaa mpaka mauti yake yalipomfika.
Baadaye Wema Abdallah akachukua nafasi ya Hanzuruni ya kupiga solo.
Nidhamu ilikuwa ni moja ya kigezo cha kuwa mwanamuziki katika Western Jazz wakati huo. Haikujali umaarufu wa mtu kwani mwanamuziki yeyote alikuwa na nafasi kubwa ya kutimuliwa kwa utovu wa nidhamu.
Hivyo tatizo la utovu wa nidhamu lilifanya Wema Abdallah kuondolewa katika bendi hiyo.
Western Jazz ilikuwa ikipiga midundo ya vyombo vya muziki vilivyoshabihiana kwa karibu na ile ya Tabora Jazz kufuatia wanamuziki Wema Abdallah na Rashid Hanzuruni kupeleka aina hiyo ya midundo huko Western Jazz waliotokea Tabora Jazz.
Bendi ikapata ‘kifaa’ kingine baada ya kumnyakua mpigaji mzuri wa gitaa la solo, Shamba Abdallah kuziba pengo la Wema. Shamba alionyesha umahiri mkubwa kwa kushiriki katika kupiga solo kwenye nyimbo za Rosa na zingine nyingi.
Ukumbi wa nyumbani wa Bendi ya Western Jazz ulikuwa ukiitwa Alexander Hall, ambalo baadaye ukaja kuitwa DDC Kariakoo.
Ushindani kati ya bendi uliendelea miaka hiyo, hivyo uliilazimu Bendi ya Western kununua ‘drums’ baada ya wenzao wa Kilwa Jazz kuzipitisha drums zao walizonunua kwa minajili ya kuwaringishia.
Walinunua kutoka kwa bendi moja ya Wagoa iliyoitwa ‘De Mello Brothers’. Western walirekodi santuri kadhaa chini ya mkataba waliosaini kwa Lebo ya Phillips ya Kenya.
Hatimaye Western Jazz ikipiga katika mtindo wao wa Saboso na ilitoweka katika anga la muziki mwishoni mwa miaka ya 1970.
Kabla ya hapo, Wetern ilitoka na vibao vingi vilivyopendwa na mashabiki wake nchini, baadhi zikiwa ni Rosa, Jela ya Mapenzi, Helena no 1& 2 na Vigelegele.
Sehemu ya wimbo maarufu wa Vigelegele inasema:
“Vigelegele ndiyo furaha jamaa hehehe, utamu wa ngoma ni kushangiliwa jamaa hehehe,cherekochereko na mayowe mengi, hehehe. Makofi mengi na vibwebwe, ndiyo furaha, hayo, hutokea, pamoja, Western, mayowe, kwa wingi, njoo uonee, furaha, furaha…”
Wimbo huo uliwatoa ‘udenda’ wakongwe wa muziki Soukous Stars na kujiamria kuurekodi pamoja na ule wa Dada Asha wa Tabora Jazz.
Kwa utaalamu mkubwa walionao, Soukous walizichakachua nyimbo hizo pamoja na nyingine na kuziweka katika album moja iitwayo Nairobi by Night.
Hata hivyo hakuna taarifa zozote zinazoonyesha kwamba wahusika wa Western Jazz na Tabora Jazz kama walifaidika au kulipwa chochote kwa nyimbo zao kurekodiwa na bendi hiyo.
Mwandishi wa makala haya anapatikana kwa namba: 0784331200, 0767331200 na 0713331200.
Mwananchi

No comments: