
HABARI zenu wadau wa safu hii. Tumekutana tena kujadiliana mambo yetu ya kikubwa wakati huu mwaka unapokatika. Wengine wanafunga hesabu kwa faida na wengine wanajikusanyia madeni.
Maisha ya kimapenzi kila siku yana mapya, wanandoa wanaweza kukaa mwezi mzima bila kuzungumza, lakini siku moja isiyo na jina wanajikuta wanapendana upya na kupiga stori kana kwamba hakuna kilichotokea jana yake.
Siku hizi kutoka nje ya ndoa tumekupa jina jipya, tunasema amechepuka badala ya kubaki njia kuu. Juzijuzi hapa nilikuwa nazungumza na msomaji wangu mmoja, aliyetaka ushauri wa jinsi ya kuishi na mwanaume ambaye ni mchepuko, kwani anahisi mwenzake si mtulivu katika uhusiano wao.
Mara nyingi ushauri mzuri kwa mtu wa namna hii, ni kumwelekeza kuachana naye kwa sababu ya hatari anayoweza kuipata, hasa katika mambo ya afya, maradhi. Mtu anayetokatoka nje ya ndoa au uhusiano wake ni rahisi kupata magonjwa, kwa sababu wanaorukaruka ovyo siyo watu wa kujali afya zao.
Lakini hata hivyo, ukisema umshauri aachane naye, ataachana na wangapi? Uzoefu unaonyesha wanandoa wengi wanatoka nje ya ndoa zao, hata kama baadhi yao wataguna hadharani.
Lakini pia katika mazungumzo hayo, nikapata kujifunza kuwa wakati mwingine, mke au mume anaweza kuwa chanzo cha mwenza wake kutoka nje ya uhusiano wao. Zipo sababu nyingi zinazoweza kusababisha hali hii, lakini hapa nitaorodhesha chache.
Kelele
Kelele siyo kitu kinachomfurahisha mtu yeyote, kwa maana hiyo, zinapozidi, haijalishi zinatoka kwa nani, zinaweza kumuongoza mtu kutoka nje ambako atajifariji kuwa anapunguza ‘stress’.
Kuna baadhi ya wenzetu hawana dogo, kila kitu ni kelele tu. Baba amechelewa kidogo kufika nyumbani, kwa utetezi kwamba alikuwa akizungumza na marafiki, mama atapiga kelele hadi basi. Jambo dogo lililopaswa kuzungumzwa kwa upendo, linafanywa kubwa!
Uchepukaji
Kuna watu kiasili siyo wa kupenda sana kujihusisha na wapenzi wengi, lakini wanajikuta wakilazimika kuwa na tabia hiyo kama kulipa kisasi kutoka kwa mwenza wake.
Kila siku unasikia kesi za mume au mke wake kufumaniwa na watu wengine. Anaweza kuvumilia kwa muda, lakini anapoona mwenzake hana mabadiliko anajiuliza, hivi presha yote ya kazi gani, kwani mbona yeye anafanya, anafikiri mimi sijui eeh!
Kama mtu anatoka nje kila siku na mwenza wake anafahamu, ni lazima ajue kuwa mwisho wa siku, mwenzake atasitisha uvumilivu na hivyo ‘kulianzisha’.
Ulevi uliokithiri
Hii mara nyingi inawatokea wanaume. Ni mara chache kukutana na wanawake walio katika ulevi wa kupindukia, lakini idadi kubwa ya watu walio katika kundi hili ni wanaume.
Baadhi yao, wakinywa sana wanaweza hata kukosa nguvu ya kushiriki tendo wakiwa na wake zao. Kitendo cha kushindwa kinamfanya mwenza kuwa na mahitaji kwa muda wote. Inapotokea namna hii, mara nyingi akina mama hujikuta wakitoka nje ili kwenda kukata kiu! GPL
No comments:
Post a Comment