Mbunge wa Jimbo la Kinondoni CCM, Idd Azzan
1. Kawishe Maina (66), Mhandisi:
Halmashauri ya Kinondoni ilibomoa makazi ya watu waliokuwa wakiishi Magomeni Kota kwa madai ya kuanzisha miradi lakini ni zaidi ya miaka minne hakuna kilichofanyika, kwa nini waliwasumbua watu?
Jibu: Nyumba hizo zilikuwa mali ya Halmashauri ya Wilaya ya Kinondoni na waliokuwa wanaishi ni wapangaji. Kilichotokea ni kwamba halmashauri iliamua kuvunja nyumba hizo ambazo zilkuwa chakavu kwa madhumuni ya kuboresha eneo hilo na kujenga majengo mapya ya kisasa yakiwamo maduka makubwa, apartments na maofisi.
Kilichochelewesha ujenzi huo ni taratibu za kuwapata wawekezaji. Hivi sasa wamepatikana na taratibu za kisheria zinaendelea vizuri. Suala la kuwasumbua watu halikuwapo kwa sababu, walipewa taarifa mapema za kuhama tangu 2006, pili walilipwa fedha za pango ili wahame eneo hilo na tatu walilipwa fedha za usumbufu.
2. Triphonia Kawishe (51), Mama wa Nyumbani:
Kwa nini tangu mwaka 2008 mpaka sasa, Mwananyamala, mitaa ya
Komakoma kichangani hakuna huduma ya maji wakati maeneo jirani wanapata?
Jibu: Tatizo ni kubwa Dar es Salaam ikiwamo Mwananyamala, mimi nikiwa mbunge nimekuwa nikiitaka Serikali iondoe tatizo hilo la maji kwa kuweka miundombiinu mipya. Kazi inaendelea vizuri na ifikapo 2015 itakamilika kwa kuwa hivi sasa Serikali inamalizia ujenzi wa mabomba kutoka Ruvu Chini kuja Dar es Salaam. Kuhusu Mtaa wa Komakoma na Mchangani kukosa maji ni kutokana na kuwapo kwa wezi wa maji hivyo nimewasiliana na Dawasco ili waweze kuwashughulikia na mimi nitawasaidia.
3. Gervas Rutaguzinda (38) Mwanaharakati;
Serikali ilitangaza elimu ya msingi ni bure lakini kwa nini mpaka sasa watoto wetu wanafukuzwa shule kwa kukosa michango?
Jibu: Ni kweli kitu hicho kipo lakini kuna michango ambayo wazazi kupitia kamati za shule wamekubaliana hivyo hi hiari yao kutoa lakini hairuhusiwi mtoto kufukuzwa shule kwa kutokutoa michango. Kama Gervas ana tatizo hilo, awasiane na ofisi ya mbunge ili asaidiwe kutatua kama ilivyofanyika kwa baadhi ya walioleta malalamiko.
4. Ratifa Hussein, Mama lishe
Umeshuhudia na umeona unyanyasaji unaofanywa na mgambo dhidi yetu, tumejiajiri lakini imekuwa kero na kugeuka wakimbizi, una mpango gani?
Jibu: Tayari nimeshaliwasilisha serikalini suala la mgambo kuwanyanyasa. Ninachowaomba mama lishe na wamachingani kwamba waache kufanya biashara katika maeneo ambayo hayaruhusiwi.
5. Abubakar Sadick, Kinyozi
Tangu umeingia madarakani, hujafanya lolote kudhibiti mtandao wa wauza unga, kinachotokea ni ukamataji wa vijana wasiokuwa na hatia eneo la Manyanya, unadhani bado una haki ya kuwa mbunge wangu?
Jibu: Kipo kikosi cha polisi kinachoshughulika na wauza unga kikiongozwa na Kamanda Godfrey Nzowa na kinafanya kazi nzuri na kama kuna watu ambao nitahisi wanahusika nitawawasilisha huko ili kikosi hicho kichukue hatua. Suala la kukamatwa vijana nimewaomba polisi wafanye uchunguzi wa kina kabla ya kuwakamata.
6. Cecilia Nyenzi, Mama wa nyumbani
Huduma za wauguzi bado ni kikwazo kwa wagonjwa na rushwa nje nje. Je, mpaka sasa umefanya nini juu ya tatizo hilo?
Jibu: Tumeboresha huduma za afya Jimbo la Kinondoni tofauti na ilivyokuwa awali. Wapo baadhi ya wauguzi na madaktari wenye tabia ya kuomba rushwa kwa wagonjwa tunaendelea kuwachukulia hatua za kisheria tunapowabaini ikiwa ni pamoja na kuwafukuza kazi. Tunachoomba ni wananchi kutoa taarifa pale wanapoombwa rushwa.
7. Mohamed Slenge, Ustadhi
Uliahidi kuondoa kero ya maji Kijitonyama kwa Ali Maua lakini mpaka sasa unaondoka na haujafanya lolote, umefanya jitihada gani?
JIbu: Kazi ya kuondo kero ya maji katika jimbo langu inaendelea vizuri itakapokamilika maji yatapatikana maeneo yote pamoja na mitaa ya kwa Ali Maua.
8. Willy Mwalafyale
Uliahidi kufanya matengenezo ya barabara zote za ndani ya mitaa lakini mpaka sasa kimya, wala huzungumzii tena hilo na muda wako umekwisha, kwa nini mheshimiwa?
Jibu: Barabara zote zinafanyiwa matengenezo na nyingine tumezijenga kwa kiwango cha lami. Hata sasa matengenezo na ujenzi wa barabara yanaendelea kufanyika.
9. Najim Hamadi, Mjasiriamali
Wakati wa kampeni ulikuwa na uzalendo katika ahadi zako na ulikuwa karibu na wananchi kuwasikiliza kero zao, lakini mpaka sasa hujawahi kututembelea hapa maskani Kinondoni kwa Manyanya ?.
Jibu: Uzalendo bado ninao kwani ni hulka yangu kuwa karibu na wananchi. Suala la kuja maskani hapo Manyanya halina noma nitakuja tu lakini na wewe unaweza kunitembelea kama mbunge wako.
10. Hansi John, Mjasiliamali
Kila kukicha watu wanajenga bila mpangilio, ukiwa mbunge umechukua hatua gani kuhakikisha makazi yanajengwa kwa mpangilio ili njia za mitaa zionekane?
Jibu: Kwa kushirikiana na halmashauri na Benki ya Dunia, tumeboresha makazi holela kwa kuweka barabara, vizimba vya taka, taa za barabarani, mitaro ya maji ya mvua na visima vya maji safi katika maeneo mbalimbali ya jimbo kama Kata ya Kigogo, Mwananyamala kwa Kopa na Tandale. Kazi inaendelea kwenye kata nyingine.
Mwananchi
No comments:
Post a Comment