ANGALIA LIVE NEWS

Monday, November 3, 2014

Mwandosya: Alichokosea Warioba ni Serikali tatu tu

Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais (Kazi Maalumu), Prof Mark Mwandosya.

Katiba inayopendekezwa tayari imekabidhiwa kwa Rais Jakaya Kikwete na Rais wa Zanzibar, Dk Ali Mohammed Shein, ikisubiri kupigiwa kura ya maoni mwakani.
Hatua hiyo imefikiwa baada ya Bunge la Katiba chini ya Mwenyekiti wake, Samuel Sitta kumaliza kuipitia Rasimu ya pili ya Katiba hiyo iliyowasilishwa bungeni hapo na aliyekuwa mwenyekiti wa Tume ya Mabadiliko ya Katiba, Jaji Joseph Warioba.
Bunge Maalumu lilianza Februari mwaka huu likiwa na jumla ya wajumbe 629; wajumbe 419 kutoka Tanzania bara na wajumbe 210 Zanzibar. Idadi hiyo inajuimusha pia wajumbe 201 walioteulia na Rais kutoka makundi mbalimbali.
Wajumbe wavutana
Wakati Bunge hilo likiendelea na kazi kulitokea mtafaruku na kutoelewama kwa baadhi ya wajumbe, mpasuko ambao ulianza mara baada ya mvutano wa nani aanze kulihutubia Bunge hilo kati ya Jaji Warioba na Rais Jakaya Kikwete.
Wajunbe kadhaa hasa wa kutoka chama tawala CCM, walithubutu hata kutoa kauli za kejeli na maudhi dhidi ya Jaji Warioba wakieleza kuwa alichowasilisha bungeni siyo maoni ya wananchi bali maoni yake mwenyewe binafsi.
Mtazamo wa Profesa Mwandosya
Lakini tofauti na msimamo wa wajumbe hao, Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais asiye na wizara maalum, Profesa Mark Mwandosya anasema Rasimu ya Katiba iliyoandaliwa na Tume ya Mabadiliko ya Katiba chini ya Jaji Warioba ni nzuri na kumkejeli kiongozi huyo kwa kazi hiyo ni kumkosea heshima.
Profesa Mwandosya akaeleza kuwa rasimu hiyo ndiyo iliyokuwa msingi wa mchakato wote wa Mabadiliko ya Katiba tofauti na maelezo ya baadhi ya watu kuwa ilikuwa mbovu na ilitengenezwa kukidhi maslahi binafsi.
“Hapa naomba nifafanue vizuri kuwa rasimu ya Jaji Warioba ilikuwa nzuri na ndio maana bungeni hakukuwa na rasimu nyingine iliyotumika kutengeneza Katiba inayopendekezwa,” anasema Profesa Mwandosya.
Kwa mujibu wa Profesa Mwandosya, ukiachilia mbali masuala ya idadi za Serikali kuwa mbili au tatu, mapendekezo yaliyokuwa kwenye Rasimu hiyo yalikuwa ni mazuri na yalikuwa na masilahi ya wananchi ambayo ndiyo haswa umuhimu wa kufanya marekebisho ya katiba.
“Haya masuala ya Serikali mbili au tatu ni ya kwetu sisi wanasiasa, hayawahusu wananchi kwani unapozungumzia idadi ya Serikali unatuzungumzia sisi viongozi wa kisiasa hivyo yale yote yalioyokuwepo kwenye ile rasimu yalikuwa yanalenga maslahi ya wananchi wetu,” anasema
Lugha za kejeli na maudhi dhidi ya Jaji Warioba
Profesa Mwandosya anasema kuwa kutolewa kwa lugha za kejeli na kumbeza Warioba ilikuwa mbinu za majadiliano katika kutaka kushinda hoja ya Serikali tatu.
“Katika eneo kama lile ni lazima utumie lugha ambayo ilikuwa siyo nzuri kwa tume ya Warioba ili kuweza kusisitiza jambo fulani au ni njia ya ushawishi ili kuweza kupata ushindi, hivyo tunapaswa kuachana na maneno na maudhi yaliyofanyika wakati ule tufuate msingi katika kuhakikisha tunapata Katiba Mpya kwa maslahi ya wananchi wetu,” anasema.
Anasema kuwa huwezi kuzungumza vizuri kama unataka kushinda jambo fulani au kusisitiza katika majadiliano kama ya Bunge Maalumu la Katiba, kwani pale kila upande ulitaka kushinda hivyo ndiyo maana kulitokea lugha kama zile,” anasema.
Kutozingatia maoni ya Wananchi
Kuondolewa kwa baadhi ya vipengele vilivyokuwa katika rasimu hiyo vya kutaka Mawaziri wasiwe Wabunge na wananchi kuwa na mamlaka ya kuwajibisha wabunge wake anasema kuwa maoni ya wananchi yaliyotolewa haikuwa kura ya maoni.
Anasema kuwa wamefuatilia katiba zote Duniani hakuna inayoonyesha wananchi kuwajibisha wabunge bali haki yao ya kuwawajibisha wabunge wataitumia wakati wa uchaguzi mkuu ambapo wabunge wengi wamekuwa wakishindwa katika chaguzi mbali mbali kutokana na kuwajibishwa na wananchi wake.
“Mfano mzuri wa wananchi kuwajibisha wabunge ni katika chaguzi mbali mbali kuanzia mwaka 2000 ambapo wabunge wengi wamekuwa wakishindwa kutetea nafasi zao kutokana na kushndwa kufanya vizuri katika majimbo yao hadi leo ukitaka kutafuta wabunge walioingia bungeni mwaka 2000 tupo wachache hata 20 hatuzidi’anasema
Kuhusu mawaziri kutokuwa wabunge anasema kuwa kuna mifumo miwili ambayo inayotumika dunaini ikiwa ni pamoja na mfumo wa Kimarekani na Kiingereza”ambapo sisi tunatumia ule wa kiingereza wa kuwajibisha Serikali ndani ya Bunge” anasema.
Anafafanua zaidi kuwa hata Serikali ya Kenya imegundua kuwa ilifanya makosa katika hilo ambapo kwa sasa inampango wa kubadilika na kuanza kutumia mfumo wa kuwajibisha Serikali ndani ya Bunge kwa mawaziri kuwa Wabunge.
Aidha Profesa Mwandosya anawaomba wananchi, kuisoma, kuijadili na kuilewa katiba hiyo kuweza kuipigia kura ya ndiyo au hapana kulingana na jinsi alivyoilewa.

Anasema wananchi ndiyo wenye kauli ya mwisho ya kuikubali au kuikataa katiba hiyo kwa kupiga kura ya ndiyo au hapana “kwani matokeo ya kura ya maoni ndiyo yatakuwa na majibu ya kweli kuhusu uhalali wa katiba hiyo.
Mwananchi

1 comment:

Anonymous said...

Asante Mhes. Mwandosya ila ukweli unabakia kuwa ukweli Tanzania bado siasa ya vyama vingi haijakaa sawia kwa kuwa CCM inadhani kuwa ndio yenyewe tuu na hakuna mwingine anayeweza. Hata wewe mwenyewe Mwandosya ukiamua kuwa mkweli nje ya CCM na ukaonekana unalengo la kuibadili Tanzania kisiasa na kiUchumi na maendeleo ya kweli ukifuta ufisadi utakubalika 90%..