ANGALIA LIVE NEWS

Thursday, November 6, 2014

Polisi Dar lawamani kuachia mtuhumiwa wa kubaka mlemavu

Mratibu wa Kituo cha Usuluhishi cha Chama Cha Waandishi wa Habari Wanawake (Tamwa), Gladness Munuo
Jeshi la Polisi Mkoa wa Ilala limelalamikiwa kwa madai ya kumkingia kifua mtuhumiwa wa ubakaji wa mtoto wenye ulemavu wa kusikia (15), lakini katika hali ya kushangaza, mtuhumiwa huyo mkazi wa Dar es Salaam (jina tunalihifadhi) ameachiwa huru kwa madai kuwa mtoto huyo ni mzoefu wa kufanyiwa vitendo hivyo.

Mtuhumiwa huyo ambaye anadaiwa kufanya kitendo hicho mwishoni mwa mwezi uliopita katika eneo la Vingunguti Mtambani, Manispaa ya Ilala jijini, anadaiwa kuwa baada ya kufanya ukatili huo, baba wa mtoto huyo alitoa taarifa kituo kidogo cha Polisi Vingunguti na kupewa fomu maalum ya matibabu (PF3).

Akizungumza na waandishi wa habari jijini Dar es Salaam jana, baba wa mtoto huyo (jina linahifadhiwa), alisema baada ya kupewa PF3, alimpeleka mtoto huyo zahanati ya Mnyamani ambako ilibainika kwamba mtoto huo alishawahi kufanyiwa vitendo hivyo ingawa haikuonyesha kama siku hiyo alibakwa.


Baba huyo alidai kuwa baada ya kumhoji mwanawe na wataalum wa lugha ya alama, alieleza kuwa alikuwa kwa mtuhumiwa huyo na mara zote amekuwa akimwingilia na kumlipa Sh. 500 na mara ya mwisho alimlipa Sh. 4,000.

Alidai kutokana na maelezo hayo, kesi hiyo ilipelekwa kwa mpelelezi wa kituo cha polisi Buguruni ambaye hata hivyo, alimshauri akamalizane na mtuhumiwa kwa sababu mwanae ni mzoefu na kwamba hakuna ushahidi wa kuingiliwa na mtuhumiwa.

Mratibu wa Kituo cha Usuluhishi cha Chama Cha Waandishi wa Habari Wanawake (Tamwa), Gladness Munuo, alisema wazazi na walezi wamekuwa na moyo wa kutoa taarifa, lakini wanakosa ushirikiano kwenye vituo vya polisi pamoja na mahakama kwani kesi hizo zinaangaliwa na wanasheria wa serikali na kutoa uamuzi ziende mahakamani au zisiende.

Alisema wanahitaji ushirikiano kutoka kwa madaktari, maofisa wa ustawi wa jamii, polisi pamoja na Mahakama kwani utekelezaji wa kesi hizo umekuwa tofauti na makubaliano kati ya Tamwa, Polisi pamoja na Mahakama.

Hata hivyo, NIPASHE ilimtafuta Kamanda wa polisi Mkoa wa Ilala, kuelezea suala hilo, lakini simu yake ya mkononi iliita bila kupokelewa.
 
CHANZO: NIPASHE

No comments: