ANGALIA LIVE NEWS

Wednesday, November 12, 2014

Ripoti ya Hoseah yavuruga Bunge

Naibu Spika,Job Ndugai akiwaonya wa Upinzani bunjgeni jana kabla ya kutokea mtafaruku. Picha na fidelis Felix

Dodoma. Sakata la uchotaji wa Dola za Marekani 200 milioni katika akaunti ya Tegeta Escrow limeendelea kuibuka kwa sura mbalimbali bungeni. Safari hii, Bunge limetakiwa kueleza ni kwa nini Ripoti ya Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (Takukuru) isifikishwe katika chombo hicho cha kutunga sheria sambamba na ile ya Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG).
Hayo yalijitokeza bungeni jana baada ya wabunge kadhaa kusimamia wakitaka mwongozo wa Spika kuhusu uchunguzi huo, hasa kutokana na kuwapo taarifa kuwa ripoti ya CAG itawasilishwa bungeni mwishoni mwa mwezi huu, lakini ile ya Takukuru ambayo pia inachunguza suala hilo, haitapelekwa bungeni wala kujadiliwa.
Uchunguzi wa Akaunti ya Escrow uliamuliwa na Serikali baada ya Mbunge wa Kigoma Kusini (NCCR-Mageuzi), David Kafulila kulipua ufisadi uliotokana na utata katika uchotaji wa fedha kwenye akaunti hiyo katika Benki Kuu ya Tanzania (BoT) baada ya kutokea mgogoro wa kibiashara baina ya Shirika la Umeme Tanzania (Tanesco) na Kampuni ya kufua umeme ya IPTL.
Katika mgogoro huo, Tanesco ilikuwa inabishia kiwango cha fedha ilichokuwa inalipa kwa gharama za uwekezaji kwa IPTL, ndipo ikaamuliwa na Mahakama ifunguliwe akaunti hiyo ili fedha ilizokuwa inalipa ziendelee kuwekwa huko hadi mgogoro utakapokwisha. Kesi hiyo iliamuliwa katika mazingira yanayoelezwa kuwa na utata na fedha hizo kuchukuliwa haraka na IPTL.
Jana, baada ya kipindi cha maswali na majibu, wabunge kadhaa walisimama wengi wakiwa wa upinzani wakitaka mwongozo kuhusu lini ripoti hizo mbili zitawasilishwa bungeni hasa baada ya ile ya Takukuru kuelezwa na Mkurugenzi Mkuu wake, Dk Edward Hoseah kuwa imekamilika na kukabidhiwa kwa Waziri Mkuu.
Mbunge wa Arumeru Mashariki (Chadema), Joshua Nassari ndiye aliyefungua mlango wa kuomba mwongozo wa Spika akitaka kujua ni lini ripoti hiyo itawasilishwa na kwa nini isiambatane na ile ya CAG kwa kuwa zote zinatokana na maazimio ya Bunge kutaka uchunguzi huo ufanyike.
Pia Nassari alihoji kwa nini mjadala wa ripoti ya CAG umepangwa siku mbili za mwisho kabla ya kumalizika kwa mkutano wa Bunge.
“Naomba maelezo kwa nini hii ya Takukuru haitaletwa wakati imeelezwa kuwa Waziri Mkuu ameshakabidhiwa?” alihoji Nassari.
Akijibu, Naibu Spika, Job Ndugai alisema Kamati ya Uongozi imeshajadili suala hilo na kuamua kwamba ripoti ya CAG itapitia kwenye Kamati ya PAC inayoongozwa na Zitto Kabwe na kuwasilishwa bungeni.
“Ripoti ya CAG itawasilishwa kwenye Kamati ya PAC na wabunge mtakabidhiwa nakala kama tulivyokubaliana kwenye Kamati ya Uongozi,” alisema Ndugai na kuongeza:
“Ripoti itawasilishwa tarehe 26 mwezi huu kama ilivyorekebishwa kwenye ratiba. Kuhusu suala la kupangwa mwishoni ni suala la kanuni kwa kuwa huwa tunaanza na shughuli za Serikali kwanza halafu ripoti zinafuata.”
Kuhusu ripoti ya Takukuru, Ndugai alisema haiwezi kuwasilishwa bungeni kwa kuwa taasisi hiyo ikishamaliza shughuli zake inaweza kuchukua hatua kwa kupeleka taarifa kwa Mkurugenzi wa Mashtaka (DPP) kwa ajili ya hatua zaidi.
“Ripoti ya Takukuru haiwezi kuja hapa, tutajadili nini? Takukuru wakishachunguza wanachukua hatua,” alisema Ndugai.
Akizungumzia ripoti ya Takukuru kuwasilishwa kwa Waziri Mkuu, Ndugai alisema si kweli, bali alichopewa ni mwenendo wa uchunguzi hivyo akawaomba wabunge wawe na subira kuhusu suala hilo.
Kauli ya kwamba ripoti ya Takukuru haitawasilishwa bungeni ilizua minong’ono na wabunge kadhaa kusimama. Ndugai alitoa nafasi kwa Zitto huku Kafulila akiwa amesimama.
Zitto alisema kamati yake itahitaji taarifa ya ziada kutoka Takukuru kuhusu mambo ya jinai ambayo yanazungumzwa kwa kuwa taarifa ya CAG haitoshi.
“Maelezo ya Naibu Spika yako sawa kabisa lakini ripoti ya Takukuru itatusaidia katika suala la uchunguzi. Hakuna namna tunaweza kukwepa ripoti ya Takukuru,” alisema Zitto.
Alimwomba Ndugai kuiagiza Serikali kuwasilisha ripoti zote mbili na mahojiano ya wanaohusika yafanyike kwa uwazi ili minong’ono iishe.
“Kumekuwa na minong’ono inatembezwa kwa wabunge kuwa kuna watu wamehongwa au wanalipwa fedha kuhusu suala hili, haya mambo yafanyike kwa uwazi na kumaliza minong’ono hiyo,” alisema Zitto.
Baada ya maelezo hayo ya Zitto, Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais (Kazi Maalumu), Profesa Mark Mwandosya alisimama na kueleza kuwa Serikali itaangalia jinsi gani watakavyoweza kusaidia ripoti hiyo ya Takukuru kuwasilishwa ili kuepuka jinai.
Alisema kwa maana ya kuisaidia kamati, basi Takukuru wanaweza wakaitwa mbele ya kamati na kutoa maelezo hayo ili yaweze kuwasaidia.
Ushauri huo ulikubaliwa na Ndugai huku baadhi ya wabunge wakionekana kutokuridhika.
Akichangia mpango wa maendeleo wa mwaka 2015/16, Mwenyekiti wa Kamati ya Nishati na Madini, Victor Mwambalaswa alisema anashangaa kusikia taarifa kwamba kamati yake imewekwa mfukoni na Waziri wa Nishati na Madini, Profesa Sospeter Muhongo kuhusu sakata hilo.
Alisema taarifa hizo siyo za kweli kwa kuwa wizara hiyo inafanya kazi nzuri na kazi ya wabunge ni kusimamia utendaji wa Serikali.
“Kuna wabunge wanasema eti kamati yangu imewekwa mfukoni na Muhongo. Huyu ni rafiki yangu nimesoma naye, sasa sijui ana mfuko kiasi gani aweze kutuweka sisi. Tunachopaswa ni kuisimamia Serikali kama wabunge,” alisema Mwambalaswa ambaye pia ni Mbunge wa Lupa (CCM).
Akichangia mpango huo, Mbunge wa Sikonge (CCM), Juma Nkumba aliwaomba wabunge kuwa na subira kwenye sakata hilo: “Suala la Escrow ikifika kipindi litashughulikiwa, naomba wenzangu tuwe na subira na wale ambao wanalitumia suala hili vibaya waache.”
Alisema kama kuna watu wanaohusika watawajibishwa kama walivyowajibishwa wengine kwa kuwa suala linalohusu masilahi ya nchi halina mbunge wa upinzani wala wa CCM.
Wiki iliyopita Mbunge wa Nyamagana (Chadema), Ezekia Wenje akichangia hoja ya mpango wa maendeleo 2015/16 alisema kuna taarifa kwamba kuna naibu waziri mmoja anaandaliwa kisaikolojia ili atolewe kafara ya ufisadi huo.
Mwananchi

No comments: