Ukisikia tu Viva Christmas, ujue mwaka umeisha na kwa sisi wazazi unaanza kufikiria ada za shule!
Basi, nimekuwa nikikutana na watu wengi wanaolalamika kutendwa na wenza wao, wakihoji bahati mbaya waliyonayo, kwani kila wakiwapata wenzao, uhusiano wao hudumu kwa muda mfupi au mara nyingine huwa ni urafiki usiyo na raha kutokana na karaha za kila siku.
Wengine, hufikia hata hatua ya kuniuliza juu ya wanawake wa aina gani ndiyo hupendwa sana na wanaume. Swali hili daima huwa gumu kulijibu kutokana na ukweli kuwa mapenzi ni hisia za mtu, ambazo hazina ujumla. Mimi naweza kumpenda sana Asha kwa sababu kwangu ana vigezo vyote, lakini akaja Samson akakwambia kati ya wanawake wabaya aliowahi kuwaona, huyu wangu anaongoza.
Ndiyo maana nimewahi kusema mara kadhaa, kwamba mapenzi ni hisia za mtu, vile anavyojisikia ndivyo anavyopenda, vinginevyo tusingewaona walemavu wakiwa na waume au wake. Lakini si umewahi kuwaona wanandoa ambao mmoja wao ni mwenye ulemavu wa kuzaliwa nao?
Wanawake wengi wana ndoto ya jinsi gani wangekuwa kama wangebarikiwa kuwa wazuri kwa umbo na sura ili wawapeleke puta wanaume. Ndiyo, wanawake warembo wanalipa. Kila mwanaume anapenda kuwa na msichana mwenye sura na umbo zuri ili anapokatiza naye mtaani watu waseme naam, kitu kimetulia!
Kila mmoja anampenda mrembo anayevutia kwa sababu anajenga heshima mbele ya washkaji zake, kwamba yeye ndiyo mjanja kwa sababu kuopoa mtoto mzuri kama huyu, siyo jambo la mchezo!
Lakini kuna kitu kimoja ambacho watu wengi hawaonekani kukitambua pale unapozungumzia kuhusu wasichana warembo. Hivi una orodha ya warembo walio katika ndoa?
Wanawake warembo siyo kimbilio namba moja la wanaume wanaotaka kuoa. Wanawaogopa kwa sababu nyingi, lakini kubwa zaidi ni usumbufu usio wa lazima kutoka kwao. Hawa wakishajitambua kuwa wao ni ‘visu’, huwa na nyodo nyingi ambazo wakati mwingine huwa ni kero kwa mume.
Silaha yao kubwa ni uzuri wao, kwamba kama unaona vipi, niache, wenzio wananihitaji. Lakini licha ya hiyo, pia kuna kitu kinaitwa stress, wanawake warembo walio katika ndoa wanaleta stress kwa waume zao.
Mume hana amani moyoni na kama mke anafanya kazi ofisi nyingine ndiyo hatari zaidi. Kwa uzuri ule, bosi atamuacha kweli? Kwa urembo ule, wenye fedha zao hawatamtamani kweli?
Ili kujiondoa katika stress kama hizo, wanaume hupenda kuoa mdada mwenye uzuri wa wastani, lakini zaidi mwenye tabia zinazofanana na mke, wazungu wanasema wife material.Maana ya kuleta mada hii ni kukupa moyo wewe dada ambaye unadhani haudumu au hauolewi kwa sababu hauna sura au umbo la kuvutia. Kuolewa au kumpata mwenza mwenye kukufaa ni kwa jinsi wewe mwenyewe unavyojiweka mbele ya wanaume.
Mke anaanza kujitengeneza mwenyewe tokea siku ya kwanza anayokutana na mwanaume wake, jinsi unavyozungumza, unavyofanya na unavyolichukulia penzi lenu.
Mtu anaweza kumtamani mwanamke, mwenye sura ya kawaida tu kwa ajili ya kujistarehesha, lakini busara anayokutana nayo, ucheshi anaouona na maono anayosikia, yakamfanya kujikuta akihama kutoka kumfikiria kama chombo na starehe na kumuona kama anayestahili kuwa mwanandoa.
GPL
No comments:
Post a Comment