ANGALIA LIVE NEWS

Friday, November 21, 2014

Spika Kificho afichua siri ya migogoro ndani ya vyama

Spika wa Baraza la Wawakilishi Zanzibar,Pandu Ameri Kificho.

Spika wa Baraza la Wawakilishi Zanzibar, Pandu Ameri Kificho, amesema migogoro mingi inayozuka ndani ya vyama vya siasa inasabishwa na kutokuheshimiwa kwa taratibu na kanuni za kidemokrasia ambazo ndiyo msingi wa utawala bora.

Aliyasema hayo wakati akifungua maadhimisho ya Siku ya Kimataifa ya Kidemokrasia yaliofanyika kilimani visiwani hapa na kuwataka vijana kujitambua na kuwa tayari kushiriki katika nafasi mbalimbali za uongozi.

"Migogoro imekuwa kikwazo cha maendeleo ya demokrasia ndani ya vyama kutokana na kutoheshimika kanuni na taratibu za uendeshaji wa vyama vyenyewe," alisema Alisisitiza kuanzishwa kwa Baraza la Vijana Zanzibar kutasaidia vijana kuwaunganisha na kutambua haki zao za msingi hasa katika nyanja za uongozi.

“Vijana wana fursa muhimu katika ujenzi wa demorasia kwani wao ndiyo viongozi watarajiwa, lazima watambue haki zao za msingi,” alisema Spika Kificho.

Alisema wakati uliopo kama vijana wataunganishwa na kushirikishwa katika mambo muhimu, maendeleo ya nchi yatapatikana kwa vile hakuna nchi inayoweza kupiga hatua ya maendeleo bila ya kuwapo kwa nguvu kazi ya vijana.

Ofisa vijana kutoka Wizara ya Uwezeshaji, Ustawi wa Jamii, Maendeleo ya Vijana, Wanawake na Watoto, Shaibu Ibrahim, alisema kwamba muswada wa sheria uliopitishwa na Baraza la Wawakilishi, tayari umeshasainiwa na Rais wa Zanzibar kwa kuanzishwa kwa Baraza la Vijana.

Hata hivyo, alisema Sheria ya Baraza haitaruhusu vijana kutumia chombo hicho kwa harakati za kisiasa na yeyote atakayefanya hivyo atakuwa amekwenda kinyume cha sheria na atapoteza sifa za kuwa mwanachama wa baraza hilo.

Alisema muundo wa baraza hilo utakuwa kuanzia ngazi ya shehia, wilaya hadi taifa na lengo kubwa la kuanzishwa baraza hilo ni kuunganisha vijana kuwa na sauti moja na kuhakikisha wanashirikishwa katika nafasi za uongozi, utayarishaji wa bajeti pamoja na utungwaji wa miswaada ya sheria.
CHANZO: NIPASHE

No comments: