ANGALIA LIVE NEWS

Tuesday, November 11, 2014

Sumaye:Kwa nini najitosa kusaka urais

Waziri Mkuu Mstaafu, Frederick Sumaye

Waziri Mkuu Mstaafu, Frederick Sumaye, ametaja sababu tatu za kuwania urais katika uchaguzi mkuu wa mwakani, akieleza kuwa mojawapo ni kukuza uchumi unaogusa maisha ya Watanzania wengi.

Akizungumza na NIPASHE wiki iliyopita katika mahojiano maalum nyumbani kwake Kiluvya, nje kidogo ya jiji la Dar es Salaam, Sumaye (64), alisema suala la pili linalomsukuma kuwania nafasi ya kuwa mkuu wa nchi ni vita dhidi ya rushwa, ufisadi na dawa za kulevya.

Alitaja kipaumbele chake cha tatu kuwa ni kuunda serikali inayowajibika kwa umma, kwa kuweka watu ambao wataweka mbele maslahi ya umma badala ya maslahi binafsi.

“Mimi nimeshasema kwamba muda ukifika nitajitosa tu kwa sababu Watanzania wengi wananiambia nijitose na sina sababu ya kuwakatalia. Muda ukifika na mimi nitatangaza… kwamba sasa na mimi nipo rasmi kwenye kinyang’anyiro hicho,” alisema Sumaye.

Sumaye ambaye anashikilia rekodi ya kukalia kiti cha Waziri Mkuu kwa miaka 10 mfululizo zaidi ya wengine wote walioshikilia nafasi hiyo chini ya uongozi wa awamu ya tatu ya Rais Mstaafu Benjamin Mkapa, alisema iwapo atafanikiwa kuteuliwa na CCM kushika wadhifa huo, atakuwa na vipaumbele vichache ili aweze kuvisimamia kwa ukamilifu.

Sumaye aliulizwa kuwa, “Kama ukajitosa na chama (CCM), kikakuidhinisha, nini vitakuwa vipaumbele vyako?.Sumaye alifafanua kwa kutaja vipaumbele hivyo vitatu.
“Mimi nitakuwa na vipaumbele vichache. Kipaumbele cha kwanza ni kukuza uchumi… sasa uchumi una makando kando mengi. Nitataka nchi iwe na uchumi imara, usiotetereka. Uchumi ambao unajumuisha wananchi walio wengi ili kubadilisha maisha ya Watanzania.”

“La pili ni kupambana na maovu hasa rushwa kwa sababu hata uchumi ukipambana nao, kama rushwa imekithiri utakuwa unabeba maji kwa gunia… wewe unafikiri unabeba maji kumbe hamna kitu. Kwa hiyo lazima kupambana na rushwa, ufisadi, dawa za kulevya na maovu yote haya,” alisema na kuongeza:

“La tatu ni kuweka madarakani serikali ambayo itawajibika kwa umma, siyo serikali au watu walioko kwenye serikali ambao wanajiangalia wao. Kama hutaki wewe kuwa mwisho umma ukawa wa kwanza, basi wewe hutafaa, itabidi tu utupishe. Mimi nina amini ukishaweka hivyo vipaumbele wananchi watapata huduma zinazotakiwa, kwa hiyo huduma za jamii zitaboreka. Elimu itaboreka, afya itaboreka, maji yatapatikana, barabara zetu zitakuwa nzuri na wananchi uchumi wao utapanda kwa hiyo kila mwananchi atajiweza.

Priorities (vipaumbele), ukizizidisha unajichanganya... weka chache, zisimamie, utaona nyingine zinajirekebisha zenyewe.”Akifafanua kuhusu kipaumbele cha kwanza, alisema ni lazima kufanyike marekebisho ya uchumi ili ukuaji wa uchumi uweze kugusa wananchi wengi.

Alisema ukuaji wa uchumi wa Tanzania hivi sasa ni mzuri kwa kuwa unaongezeka kwa asilimia saba, jambo ambalo ni zuri, lakini (bahati mbaya) ni kwamba haugusi maisha ya watu wengi.

“Suala la kukua kwa uchumi na uchumi wa aina gani ni vitu viwili tofauti. Lazima tuwe na uchumi ambao unakua, lakini ambao kila mtu anafaidi,” alisema.Alisema kuna nchi ambayo uchumi wake unakuwa kwa hadi zaidi ya asilimia 10, lakini unalenga familia moja au kikundi cha watu wachache, jambo ambalo kitaifa uchumi utaonekena unakuwa lakini kiuhalisia unanufaisha watu wachache tu.

“Sasa hapa kwetu napo uchumi haujakaa vizuri, haujaenea kwa watu wengi. Njia ni kuangalia ni maeneo gani tutawekeza nguvu. Leo tuna rasilimali kama madini na gesi, hatuwezi kunufaika wote kwenye madini, lakini yanaweza kutumika kuinua uchumi unaogusa watu wengi,” alisema.

Alisema manufaa ya rasilimali kama madini na gesi yanaweza kuonekana kwa kuleta mageuzi makubwa kwenye sekta ya kilimo ili kikue kwa asilimia nane au tisa kwa mwaka badala ya nne za sasa.

Alisema uboreshaji huo wa sekta ya kilimo unapaswa kwenda sambamba na uboreshaji wa viwanda hasa vinavyotumia malighafi zinazopatikana nchini kama pamba, korosho, matunda na miti.

“Tukiweka viwanda vya mbao, badala ya kuuza pamba sasa tukatengeneza nguo, tukaacha kuuza kahawa punje na korosho zikabanguliwa nchini, hapo tutakuza uchumi unaogusa watu wengi,” alisema.

Alisema sekta nyingine kama gesi na mafuta zinazohitaji uwekezaji wa fedha nyingi na utaalamu mkubwa, serikali inapaswa kuzisimamia kikamilifu ili uvunaji wake uwanufaishe wananchi wengi.


VITA DHIDI YA RUSHWA
Akizungumzia vita dhidi ya rushwa na ufisadi, alisema hali ni mbaya nchini na kwamba ikiachwa iendelee itawaumiza wananchi na itafika mahali watashindwa kuvumilia.

“Mtu atakapoona kwamba anashindwa kupata huduma mpaka atoe rushwa, hao watakapokuwa wengi watakataa na wakikataa itakuwa mbaya. Kwa hiyo serikali lazima kwa nguvu zake zote ipambane na rushwa na ufisadi katika ngazi zote kuanzia ofisi za umma hata za binafsi,” alisema.

Alisema rushwa inachangiwa na ubinafsi uliokithiri na udhaifu katika utawala kiasi kwamba hadi imefikia hatua mtu anapopewa kazi ya umma lazima aibe ili aonekane ni shujaa.

Alisema viongozi wanapaswa kujua kwamba wakipewa kazi ya umma wanatakiwa wawe wawazi na kueleza vipato vyao.“Lazima turudi kwenye uwajibikaji. Kama wewe ni Katibu Mkuu au ni Waziri, tunaona unafanya vitu vya ajabu, inabidi tukuulize mwenzetu una mgodi? Inafika mahali jamii inaona kama uchumi wako unakuwa tu kiajabu ajabu, inaonekana kama ni sifa wakati zamani haikuwa hivyo.”

Alisema viongozi wa umma wanapaswa kuwa wawazi na kama mapato yao ni halali hakuna atakayesumbuliwa kwa kuwa siyo dhambi kwa kiongozi kuwa tajiri, bali muhimu ni kuona kuwa anauupata (utajiri) kwa njia halali.

Alisema viongozi pia wanapaswa kueleza namna ambayo maslahi binafsi hayataingilia maslahi ya umma iwapo wanamiliki kampuni au hisa kwenye kampuni binafsi na hiyo itasaidia kuhakikisha kwamba wanautumikia umma ipasavyo.

“Watu hawana tatizo kama wewe una mali, tatizo ni kwamba mali hizi umezipata sawa sawa (kihalali)? Isiwe ni mali za kutuibia.”

UWAZIRI MKUU MIAKA 10
Kuhusu mafanikio yake wakati akiwa Waziri Mkuu, nafasi aliyoitumikia kwa miaka 10 mfululizo na kuwa mtu pekee aliyedumu katika nafasi hiyo kwa kipindi kirefu zaidi nchini, alisema ni kwa sababu yeye ni mchapakazi, mwadilifu na mwaminifu.

Aidha, alisema yeye ni mtendaji mwenye bidii na mpenda haki na ndiyo mambo aliyokuwa akiyasimamia kwenye uongozi wake na hadi sasa bado anaamini kuwa hayo ni mambo ya msingi kuzingatiwa na kila kiongozi.

“Hayo ni mambo muhimu kwa kiongozi yeyote yule,” alisema Sumaye.
CHANZO: NIPASHE

4 comments:

Anonymous said...

hakuna anaekutaka, Sumae wewe mwenyewe umeifilisi nchi. au zimeisha??

Anonymous said...

ANAJIKOSHA KWA KUWA ANAJIJUA ALIVYOWATIA WA TZ. UMASKINI YEYE PAMOJA NA MKAPA, HATUMTAKI SUMAYE.

Anonymous said...

Waachieni vijana washike nchi, ya wazee hayana mshiko, ni wizi tuu

Anonymous said...

mHESHIMIWA Sumaye tunakuomba ukaendelee kupumzika huko Kiluvya au Meru tu ulishatuongoza hakuna kipya utakacholeta ni sifa unatafuta bila kuwapa maendeleo yeyote yale waTz. CCM KAENI KANDO KABISA. HAKUNA ANAYEWEZA KUKOMESHA RUSHWA NA UFISADI KAMWE KWANINI MSIFANYE SASA HIVI MKIWA NDANI???