ANGALIA LIVE NEWS

Monday, November 10, 2014

UMUHIMU WA KUTOKA ‘OUT’ NA UMPENDAYE

NI Jumatatu nyingine tunapokutana katika uwanja wetu huu mzuri, tukijuzana na kuelimishana kuhusu mambo mbalimbali yahusuyo mapenzi. Mada yetu ya leo ni kama inavyojieleza hapo juu.

Je, mara ya mwisho kwa wewe na mpenzi wako kutoka ‘out’ ilikuwa ni lini? Una desturi ya kutoka na umpendaye, mkaenda mahali tulivu ambapo mtapata muda wa kujadiliana na kubadilishana mawazo kuhusu maisha na mapenzi? Kama jibu lako ni hapana, unaishi kwenye mapenzi yaliyokosa uhai. Maisha yanaenda kasi sana, wanandoa wengi au watu ambao wapo kwenye uhusiano wa kimapenzi, wanajikuta wakikosa kabisa nafasi ya kuwa pamoja kutokana na kila mmoja kuweka kipaumbele katika kazi, biashara au shughuli nyingine za utafutaji pesa au malezi ya watoto.

Matokeo yake, watu wengi wanaishi kwa mazoea tu lakini katika uhalisia, mapenzi yanakuwa yamepungua sana au hayapo kabisa.

KUTOANA OUT HUFUFUA MAPENZI

Watafiti wa mapenzi wanaeleza kwamba hakuna kazi ngumu kama kuishi pamoja wewe na mpenzi wako, iwe ni kwenye ndoa au uhusiano wa kawaida wa kimapenzi kwani ni rahisi sana watu kuchokana. Hata kama unampenda vipi, lazima kuna muda utamchoka au utachoshwa na mazingira ambayo mmekuwa mkiishi siku zote.

Unapofikia hatua hii, kitu pekee kinachoweza ku-refresh akili na hisia zako, ni wewe na umpendaye kutoka pamoja na kwenda sehemu tofauti kama ufukweni, hotelini au sehemu yoyote tulivu ambayo mtakaa pamoja, mtakunywa au kula na kufurahi. Kitendo hiki kinatajwa kuwa siri kuu ya kufufua mapenzi na kuondoa ile hali ya kuchokana.

Haijalishi umeishi kwa muda gani na mpenzi wako, hata kama mna miaka kibao, lazima muendelee kutoana out mara kwa mara. Hata kama tayari mmeshazaa watoto na wamekuwa wakubwa, suala la out halikwepeki kama mnataka kuishi kwa amani na upendo. Wengi wanaamini kwamba mpenzi mpya pekee ndiye anayetakiwa kutolewa ‘out’, jambo ambalo siyo sahihi.

Mkirudi, kila mmoja atashangaa kwamba mapenzi yake kwa mwenzake, yatazidi maradufu, kama kulikuwa na migogoro ya hapa na pale, itaisha na mtaendelea kuishi kwa amani na furaha.

SIYO LAZIMA UWE TAJIRI KUTOKA OUT
Wengi tunasumbuliwa na kasumba kwamba ili kumtoa mpenzi wako out, ni lazima waleti yako iwe imejaa, lazima mkatumie fedha nyingi au lazima umpeleke sehemu ya gharama. La hasha, siyo lazima kabisa.
Kwa mfano, inakugharimu nini wewe na mpenzi wako kutoka na kwenda ufukweni, mkaagiza soda, maji au vinywaji mnavyovipenda, mkakaa kwenye mchanga wa bahari na kupunga upepo mwanana?

Hata kama hakuna ufukwe hapo mnapoishi, mnaweza kutoka na kwenda sehemu yoyote tulivu, iwe ni kwenye uwanja wa mpira muda ambao hakuna watu, sehemu za milimani au mahali popote ambapo mtakuwa wawili tu, inatosha kabisa. Unaweza kununua matunda, vinywaji au vitafunwa mnavyovipenda, mkaenda navyo mpaka sehemu mliyoichagua, siyo lazima uwe na fedha nyingi.

MAMBO YA KUZINGATIA MKIWA OUT
Ili mtoko wako na umpendaye ukamilike, kuchagua sehemu ya kwenda ni jambo la kwanza lakini kubwa zaidi, lazima ujue kwamba mkiwa ‘out’, unapaswa kufanya nini ili mpenzi wako afurahi na kufufua upya hisia za mapenzi ndani ya moyo wake.

Ukishindwa kujua nini cha kufanya na kipi hutakiwi kabisa kufanya mkiwa out, badala ya kufufua mapenzi, unaweza kujikuta unaongeza ufa hivyo ni lazima kila mmoja ajue anatakiwa kufanya nini anapokuwa out.
Tukutane wiki ijayo ili kujuzana nini unatakiwa kufanya na kipi hutakiwi kabisa kufanya mnapotoka out na umpendaye. Vitabu vya ufundi katika mapenzi vinapatikana kwa wakazi wa Dar. Piga namba za hapo juu kwa maelezo.

GPL

No comments: