Mbeya. Askofu Kiongozi wa Kanisa la Moravian Tanzania, Alinikisa Cheyo amezuiwa na waumini wa kanisa hilo kuingia katika ofisi yake iliyopo Jakaranda, Mbeya kwa saa 18.
Cheyo, ambaye pia ni Askofu Mkuu wa Kanisa la Moravian Jimbo la Kusini Magharibi, alifungiwa mlango na waumini wa kanisa hilo Usharika wa Jakaranda kumzuia asiingie mpaka atakapoitisha mkutano na kumrudisha Mchungaji Nosigwe Buya ambaye alimhamisha.
Akizungumzia hatua hiyo mbele ya waumini wengine, Mchungaji wa usharika huo, Jamson Mwilugumo alisema walifunga mlango huo kushinikiza Askofu Cheyo abadili msimamo wa kumwondoa Mchungaji Buya na kumrejeshea wadhifa wake wa Mwenyekiti wa Halmashauri Kuu ya jimbo hilo.
Jitihada za Askofu Cheyo kuwasihi waumini hao kufungua milango iliyokuwa imefungwa kwa minyororo hazikufua dafu hadi alipoomba msaada wa Mkuu wa Wilaya ya Mbeya, Dk Norman Sigala.
Baada ya kufika katika eneo hilo, Dk Sigala ambaye aliambatana na Kamanda wa Polisi Mkoa wa Mbeya, Ahmed Msangi aliwataka waumini hao wafungue mlango huo na kutoa maelekezo kwa Askofu Cheyo kuhakikisha kuwa anaitisha mkutano wa Halmashauri Novemba 15, mwaka huu bila kukosa ili kumaliza mgogoro huo.
Kauli hiyo ilipokewa kwa furaha na waumini hao ambao walifungua mlango.
Akizungumza mbele ya Dk Sigala, Askofu Cheyo alikubali kuitisha mkutano kumaliza mgogoro huo kama kiongozi huyo wa Serikali alivyoelekeza.
Mgogoro ulikoanzia
Mgogoro huo ulianza Aprili 30, mwaka huu katika mkutano wa Halmashauri hasa katika suala la ujenzi wa Shule ya Sekondari ya Mbozi. Ilidaiwa kuwa katika kikao hicho, Askofu Cheyo aliamuru Buya na makamu wake watoke nje ya kikao na kufanya uchaguzi mpya na kumchagua mwenyekiti.
Mgogoro huo uliibuka tena Julai 15, mwaka huu wakati waumini hao walipofunga ofisi hizo kwa zaidi ya saa tano wakishinikiza kuitishwa mkutano wa halmashauri ya usharika huo.
Katika mgogoro huo, Askofu Cheyo amekuwa akisema kwamba unatokana na baadhi ya watu wenye uroho wa madaraka.
Mwananchi
No comments:
Post a Comment