Advertisements

Wednesday, November 19, 2014

Wasira: Ubora wa mgombea muhimu kuliko chama 2015

Arusha. Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais (Uhusiano na Uratibu), Stephen Wasira amesema ubora wa mgombea ndiyo utakaokuwa msingi wa ushindi katika Uchaguzi wa Serikali za Mitaa Desemba 14 na Uchaguzi Mkuu 2015.
Akizungumza mjini Arusha mwishoni mwa wiki, Wasira anayetajwa kuwa mmoja wa watu wanaowania kuteuliwa kugombea urais kupitia CCM, alisema hakuna chama kitakachoshinda kwa kutegemea umaarufu wake au wingi wa wanachama wake.
Alisema upigaji kura ungekuwa unazingatia chama, basi CCM isingehangaika kupiga kampeni na kujinadi kwani ndicho chenye wanachama wengi nchini na hivyo kingeshinda kirahisi.
Utafiti wa Twaweza
Akijibu swali la nini maoni yake kuhusu utafiti wa Taasisi ya Twaweza kuhusu urais mwakani, Wasira alisema: “Kwanza sijausoma utafiti wenyewe kujua vigezo na sampuli ya utafiti wao, lakini lililodhahiri ni kwamba ubora wa mgombea au wagombea ndiyo msingi wa ushindi kwenye uchaguzi.”
Waziri huyo aliyekuwa jijini Arusha kuhudhuria vikao vya CCM kupitia nafasi yake ya ulezi wa chama hicho Mkoa wa Arusha alisema kipindi cha viongozi kufikiria ukubwa na umaarufu wa vyama vyao nyakati za kampeni na uchaguzi kimepitwa na wakati, badala yake kila chama lazima kiwapime, kuwachuja na kupata wagombea bora.
“Ndani ya CCM tayari tumebaini hilo ndiyo maana tuko makini kwenye uteuzi wa wagombea wa nafasi mbalimbali kuanzia chaguzi za ndani na nje ya chama,” alisema.
Alisema CCM na viongozi wake wanaujua ukweli huo kuwa wananchi hawaangalii itikadi zao za vyama wakati wa kupiga kura, bali ubora wa mgombea. “Wananchi hawapigi kura kwa kuzingatia uanachama wa vyama vyao. Hapana! Wanaangalia ubora wa mgombea. Mgombea bora hushinda hata kama chama chake kina wanachama wachache katika eneo husika,” alisema na kuongeza:
“Nawatoa hofu wanaCCM kuhusu uchaguzi wa Serikali za Mitaa na Uchaguzi Ukuu mwakani. Chama kitasimamisha wagombea bora ili kujihakikishia ushindi kama uchaguzi uliopita.”
Azungumzia Ukawa
Akijibu swali la iwapo CCM imeingiwa hofu ya kushindwa kwenye chaguzi kuanzia Serikali za Mitaa baada ya vyama vikuu vya upinzani nchini vya kuungana na kuunda Ukawa, Wasira alijibu kwa kejeli akisema:
“Hakuna anayekatazwa kuota ndoto. Kuota ndoto ni jambo la kawaida na kila mtu anaruhusiwa kuota. Ila ukweli unabaki kuwa ndoto ni ndoto tu, ndiyo maana anayeota akiamka hutambua kuwa alikuwa ndotoni.
Alisema Ukawa inayoundwa na vyama vya NCCR-Mageuzi, CUF na Chadema kufikiria ushindi dhidi ya CCM kwa kuungana kwao ni ndoto itakayoyeyuka wakiamka usingizini.
Alisema ingawa muungano huo ni jambo jema kwa vyama vya ushindani, lakini hauwezi kuwa tishio kwa CCM yenye misingi imara, mtandao mpana na rasilimali watu kila pembe ya nchi kulinganisha na vyama vingine vya siasa. “Licha ya changamoto na mabadiliko makubwa katika uwanja wa siasa yanayotokea nchini, CCM bado kinaendelea kubakia kuwa chama kikuu, imara na chenye misingi inayoihakikishia ushindi siyo tu kwenye uchaguzi wa serikali za mitaa mwaka huu, bali hata Uchaguzi Mkuu ujao 2015,” anasema Wasira.
Mnyukano CCM
Akizungumzia minyukano ya wenyewe kwa wenyewe ndani ya CCM kuwania nafasi ya kuteuliwa kupeperusha bendera ya chama hicho, Wasira alisema ni dalili ya kuimarika na kukubalika kwa chama miongoni mwa wanachama wenyewe na jamii kwa ujumla.
“Chama kisichotoa matumaini hakiwezi kushuhudia mnyukano wa wanachama kuwania uteuzi. Watu kuchuana na kushindana kwa nguvu ndani ya chama ni kudhihirisha kuwa chama kiko hai na imara. Watu hawawezi kugombania kisichofaa.
“Ukiona watu wanachuana kuwania uteuzi ndani ya CCM ujue kinakubalika ndiyo maana watu wana matumaini ya kushinda kufanikiwa malengo yao kupitia tiketi ya chama. Ingawa ubora wa mgombea ni jambo la kuzingatiwa.”
Akizungumzia tuhuma za rushwa na rafu ndani ya CCM
Wasira alisema: “Kwamba kuna rushwa na matumizi ya fedha kuwania uteuzi ndani ya CCM ni jambo ambalo siwezi kulizungumzia kwa sababu sijalishuhudia. Lililo dhahiri ni kwamba wanaoshindwa au waliowaunga mkono kushindwa lazima watalalamika.”
Hata hivyo, alisema CCM imeweka misingi na utaratibu bora wa kudhibiti vitendo vya rushwa ndani na nje ya chama kuhakikisha kinapata wagombea bora watakaokihakikishia ushindi dhidi ya wagombea kutoka vyama vingine vya siasa.
“Wana CCM wasihofu. Chama kiko macho dhidi ya vitendo vyovyote vinavyokiuka taratibu, kanuni na katiba ya chama. Kuna vyombo na vikao vinavyofuatilia kila kinachoendelea kuanzia ngazi ya mashina hadi Taifa na uteuzi wa wagombea utazingatia ubora mgombea mwenyewe utakaotuhakikishia ushindi.”
Alisema vikao vya chama hicho kila ngazi vitatumika kupitia na kufanya uteuzi kulingana na majukumu na madaraka ya kikatiba na kuwataka wanachama kuacha malalamiko na hoja inayoweza kusababisha nyufa ndani ya chama, hivyo kunufaisha vyama vingine.
Wasira alikuwa akirejea malalamiko ya baadhi ya wanachama kuhusu kura za maoni ndani ya chama hicho kuwania uteuzi kwenye uchaguzi wa Serikali za Mitaa Desemba 14, mwaka huu na kwa nafasi yake ya mlezi wa mkoa, alipokea malalamiko kutoka wilaya mbalimbali kuhusu rafu zinazodaiwa kuchezwa ngazi ya vitongoji na vijiji.
CCM Mkoa wa Arusha ina historia ya kupoteza uchaguzi kutokana na mgawanyiko unaosababishwa na matokeo au mchakato wa kura za maoni. Mwaka 1995, Jimbo la Karatu lilinyakuliwa na Chadema kupitia Dk Willibrod Slaa baada ya vikao vya uteuzi kupuuza maoni ya wananchi kupitia kura za maoni kwa kumteua Patrick Quorro badala Dk Slaa aliyeshinda kura za maoni.
Baada ya kukatwa jina, wananchi Karatu wakamwomba Dk Slaa kuhamia Chadema na kugombea ubunge na alimbwaga Quorro aliyesimamishwa na CCM.
CCM pia kilikipoteza kiti cha Arusha Mjini mwaka 2010 baada ya Chadema kupitia kwa mgombea wake, Godbless Lema kutumia mpasuko uliosababishwa na kura za maoni ndani ya CCM.
Katika uchaguzi mdogo Arumeru Mashariki, Chadema kiliishinda tena CCM kwa Joshua Nassari kuibuka kidedea dhidi ya Sioyi Sumari ambaye uteuzi wake uligubikwa na tuhuma za matumizi ya fedha huku ukiacha mpasuko ndani ya chama hicho tawala.
Kama alivyosema Wasira, matokeo ya majimbo hayo matatu kunyakuliwa na Chadema dhidi ya wagombea wa CCM kunadhihirisha kuwa wapigakura hawafuati vyama, bali ubora na ushawishi wa mgombea.
Kauli ya Wasira kuhusu ubora wa mgombea katika ushindi inakuja siku chache baada ya taarifa ya utafiti wa Twaweza kuonyesha kuwa Waziri Mkuu wa zamani, Edward Lowassa na aliyempokea nafasi hiyo, Mizengo Pinda, wote kutoka CCM wanaongoza kwa kuungwa na mkono na wengi katika ngazi ya urais. Hata hivyo, wanasiasa, wasomi na makundi mbalimbali ya kijamii wamepinga utafiti huo wakidai umeacha maswali mengi likiwamo la kwa nini haukushirikisha wanawake ambao nao wanatajwa urais 2015?

Wanaopinga utafiti huo pia wanatoa hoja kuwa wengi wa waliohojiwa wana wastani wa miaka 50 na kuendelea, kada inayosadikika kukiunga mkono CCM kulinganisha na vijana ambao wengi wanaviunga mkono vyama vingine vya upinzani.
MWANANCHI

No comments: