Dodoma/Dar/Mikoani. Ni wiki ya shida. Wiki hii inatarajiwa kuwa ya vikao mfululizo na mijadala isiyokoma. Ndiyo wiki inayotarajiwa kuuweka hadharani mtikisiko wa tano katika Serikali ya Rais Jakaya Kikwete wakati ripoti ya uchunguzi wa sakata la IPTL itakapowasilishwa rasmi kwa wabunge na Taifa kwa jumla mjini Dodoma keshokutwa na kuhitimisha minong’ono na uvumi
Ni wiki ambayo Bunge litaamua juu ya hatua za kuchukua dhidi ya vigogo wa Serikali ambao wamekuwa wakitajwa kuhusika na ufisadi huo wa kuchota au kunufaika na Sh306 bilioni katika Akaunti ya Tegeta Escrow iliyoko Benki Kuu ya Tanzania (BoT).
Ripoti hiyo inayosubiriwa, itawasilishwa na Kamati ya Bunge ya Hesabu za Serikali (PAC), inayoongozwa na Zitto Kabwe, ambayo itatoa mapendekezo juu ya hatua za kuchukua.
Wabunge wa vyama mbalimbali, jana walikuwa na vikao kadhaa wakijipanga jinsi ya kushughulikia sakata hilo mara tu ripoti itakapowasilishwa.
Wabunge wa CCM jana jioni walikutana kuwekeana msimamo kuhusu sakata hilo huku kukiwa na taarifa kwamba baadhi yao, hasa walioonyesha kushabikia ripoti hiyo, wamekaripiwa na kupewa mwongozo wa kuilinda Serikali.
Habari za ndani zinasema kuna juhudi kubwa zinafanywa ili kuhakikisha Baraza la Mawaziri halivunjwi kwa mara ya pili, baada ya tukio la mwaka 2007 alipojiuzulu aliyekuwa Waziri Mkuu, Edward Lowassa kutokana na kashfa ya Richmond.
Habari zaidi zilisema, juzi kilifanyika kikao kingine ndani ya Makao Makuu ya CCM, Dodoma kikiwahusisha baadhi ya wabunge, mawaziri na vigogo wanaotuhumiwa katika kashfa hiyo.
Habari zinasema kikao hicho kilipata muhtasari kutoka ndani ya PAC lakini hakikufikia mwafaka kutokana na baadhi ya wajumbe kupinga kujadili suala hilo mbele ya watuhumiwa na bila kupewa ripoti kamili ya Mdhibiti na Mkaguzi na Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG).
Vilevile, wabunge wa Kambi Rasmi ya Upinzani wanaounda Umoja wa Katiba ya Wananchi (Ukawa) nao walikutana jana kujipanga kwa ajili ya kushughulikia sakata hilo.
Mbunge wa Ubungo (Chadema), John Mnyika alisema wameitisha kikao hicho kuwekeana msimamo.
“Tunakwenda kukutana kama Ukawa ili tuwekeane msimamo jinsi gani ya kulishughulikia sakata la ufisadi wa Escrow,” alisema Mnyika.
Ripoti hiyo itawasilishwa huku kukiwa na madai kutoka Ukawa kuwa imevuja na kusambazwa mitaani na baadhi ya kurasa zenye majina ya wahusika zikichomolewa ili kuuhadaa umma.
Kurasa zilizochomolewa zimeelezwa kutawanywa kwa wabunge na mtu mmoja ambaye Ukawa haujamtaja, lakini ukitaka polisi imshughulikie.
Kamanda wa Polisi Mkoa wa Dodoma, David Misime juzi alithibitisha kumshikilia mhusika baada ya kumkamata akiwa na nyaraka za Bunge ambazo hazipaswi kuwa mikononi mwake.
Alisema walipokea taarifa za mtu huyo kutoka Ofisi ya Bunge na walipomkamata na kumpekua walikuta nyaraka za aina tatu, mbili zikiwa na muhuri wa Katibu wa Bunge na alipohojiwa alisema amepewa na mbunge mmoja aliyeambatana na watu wengine wawili (hakuwataja) ambao bado wanatafutwa.
Lipumba amvaa Pinda
Mwenyekiti wa CUF, Profesa Ibrahim Lipumba amemtaka Waziri Mkuu, Mizengo Pinda kujiuzulu au kufukuzwa kwa kushindwa kuzuia ufisadi wa fedha katika akaunti hiyo. Pia amemtaka Pinda awajibike kwa kauli yake kwamba fedha hizo hazikuwa za umma.
Lipumba aliwataja vigogo wengine wanaotakiwa kujiuzulu kuwa ni Mwanasheria Mkuu wa Serikali, Jaji Frederick Werema, Waziri wa Nishati na Madini, Profesa Sospeter Muhongo na Katibu Mkuu wake, Eliakimu Maswi.
Kadhalika, Profesa Lipumba amevitaka vyombo vya dola kuwakamata na kuwafungulia mashtaka haraka iwezekanavyo wamiliki wa Kampuni ya IPTL, James Rugemalira na Habinder Singh Sethi kutokana na kashfa hiyo.
Rugemalira na Seth wanadaiwa kuchukua Sh321 bilioni kinyume na makubaliano kwenye Akaunti ya Tegeta Escrow ambayo ilifunguliwa baada ya kutokea mgogoro wa malipo kati ya Tanesco na IPTL.
Fedha hizo zilichukuliwa kabla mgogoro huo haujapatiwa suluhisho, kitendo kinachotafsiriwa kuwa kilikuwa na mazingira ya rushwa.
Profesa Lipumba alisema akaunti ambazo vigogo wa Serikali walipitishia fedha kutoka katika Akaunti ya Tegeta Escrow zinatakiwa kusimamishwa.
Maandamano CUF
Lipumba alisema chama hicho kwa kushirikiana na wadau wengine wanaandaa maandamano kulaani vitendo vya kifisadi kwenye Akaunti ya Tegeta Escrow na kuwapongeza wabunge walioibua hoja hiyo hadi ukaguzi ukafanywa na CAG.
Alisema maandamano hayo yatafanyika baada ya mjadala wa siku mbili utakaofanyika bungeni kuhusu sakata hilo.
Alisema baada ya wabunge kujadili watafanya maandamano hayo ili kufikisha ujumbe kwa wananchi kuhusiana na ufisadi huo.
Maaskofu wambana Pinda
Kwa upande mwingine, Serikali imetakiwa kutoa majibu ya msingi juu ya sakata la IPTL ili kuepusha minong’ono inayoweza kusababisha uvunjifu wa amani nchini.
Askofu Mkuu wa Kanisa la Anglikana Tanzania, Dk Jakob Chimeledya alisema jana kuwa suala la escrow limeiweka Serikali katika hali mbaya kiasi kwamba inaweza isiaminike kwa wananchi wake.
Hata hivyo, Waziri Mkuu Mizengo Pinda hakujibu hoja hiyo moja kwa moja badala yake akasema inapokaribia kipindi cha uchaguzi kunakuwa na mambo mengi ambayo hujitokeza.
“Mara nyingi inapokaribia kipindi kama hiki si mnajua mbio zilizoko mbele yetu? Kwa hiyo kuna mambo yanakuwa ya kweli na mengine siyo ya kweli, inabidi tuangalie, lakini Serikali itaona namna ya kutoa maelezo,” alisema Pinda.
Akizungumza mbele ya mamia ya waumini wa Kanisa hilo katika ibada ya kumweka wakfu Askofu wa sita wa Dayosisi Central Tanganyika (DCT), Dk Dickson Chilongani, Askofu Chimeledya alisema ukimya wa Serikali unatia shaka.
“Tunaitaka Serikali itoe ukweli kwani sasa Taifa linaishi kwa uvumi tu jambo ambalo si la kufumbia macho na kama hivi ndivyo hamtaaminika,” alisema Askofu Chimeledya.
Mwandosya: Hatutaangalia mtu
Wakati huo huo; Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais (Kazi Maalumu), Profesa Marc Mwandosya amesema mbivu au mbichi kuhusu sakata hilo zitajulikana wiki hii na hataangaliwa mtu, bali masilahi ya chama.
Profesa Mwandosya alisema hayo jana wakati akizungumza na wanafunzi wa Chuo Kikuu cha Dodoma ambao ni wafuasi wa CCM waliopata nafasi ya kumhoji masuala mbalimbali ya chama na Serikali.
Alisema angependa watu wanaotajwa wajiondoe wenyewe hata kama hawajahusika, kwa kuwa itakuwa ni nzuri kwao na itakuwa heshima kwa chama... “Hata kama mtu hajahusika itamsaidia sana akijiondoa kwani italinda chama pia.”
Alisema kwa kuwa suala hilo linajadiliwa ndani ya vikao vya chama ambavyo naye huwa anaingia, atatoa ushauri na kuangalia jinsi gani ya kulishughulikia.
Mbeya na Arusha
Mwenyekiti Mstaafu na Mwasisi wa CCM mkoani Mbeya, Isakwisa Mwambulukutu ameshauri watu wote watakaobainika warudishe fedha na kufilisiwa mali zao na kama ni viongozi wa umma, waachishwe nyadhifa zao zote na wafikishwe kwenye vyombo vya sheria.
Mbunge wa Arumeru Mashariki (Chadema), Joshua Nassari amewataka wakazi wa jimbo lake kutochangia ujenzi wa maabara hadi watuhumiwa waliohusika na fedha za escrow watakapowajibishwa na kuzirejesha “... huu ndiyo ujumbe wangu leo hapa Kanisani.”
Alisema hayo katika ibada ya kusimikwa wachungaji Barakaeli Mungure na Lazaro Mafie wa Kanisa la Kiinjili la Kilutheri Tanzania (KKKT), Usharika wa Mulala.
Nape
Kutoka Lindi, viongozi wa juu wa CCM wamesema kila mtu atabeba msalaba wake mwenyewe katika sakata hilo kwa kuwa chama hicho hakiwezi kuwavumilia viongozi na watendaji wenye nia mbaya na Serikali yake.
Katibu wa Itikadi na Uenezi wa CCM, Nape Nnauye alisema katika mkutano wa hadhara mjini Lindi jana kuwa, chama hicho ndicho mwasisi wa maadili na miiko ya uongozi wa umma nchini kuanzia enzi za Tanu, hivyo kitaendelea kusimamia kwa vitendo dhana hiyo.
Alisema kinyume na wapinzani wanavyodai kuwa CCM imeondoa kipengele cha maadili ya umma kwenye Katiba Inayopendekezwa, chama hicho kitaendelea kuyasimamia bila woga maadili kama kilivyochukua uamuzi mgumu katika matukio ya Richmond na mengine.
Katibu Mkuu wa CCM, Abdulrahman Kinana alisema wakati wa kuomba ridhaa kwa wananchi waliahidi mambo mengi, hivyo ni wajibu wa chama kurudi kuangalia utekelezaji wake.
Alisema muda wa kuvumiliana, kubebana na kulindana umekwisha kwani imekuwa tabia na ugonjwa kwa baadhi ya viongozi kushindwa kusimamia na kukosoa pale watendaji wanaposhindwa kuwajibika ipasavyo na CCM haiwezi kufumbia macho mwenendo huo.
Imeandikwa Boniface Meena, Sharon Sauwa, Israel Mgussi na Habel Chidawali (Dodoma) Raymond Kaminyoge (Dar), Lauden Mwambona (Mbeya), Mwanja Ibadi (Lindi) na Mussa Juma (Arusha).
Mwananchi
No comments:
Post a Comment