ANGALIA LIVE NEWS

Sunday, November 30, 2014

Yametimia

Waziri wa Nishati na Madini, Profesa Sospeter Muhongo

Katika hali inayoonyesha yametimia, Bunge limeazimia Waziri wa Nishati na Madini, Profesa Sospeter Muhongo, Katibu Mkuu, Eliakim Maswi, Mwanasheria Mkuu wa Serikali Jaji Fredrick Werema, wajumbe wa bodi ya wakurugenzi Tanesco, James Rugemalira na mmiliki wa kampuni ya IPTL, Harbinder Singh Sethi, wawajibishwe kwa kuhusika katika sakata la Akaunti ya Escrow IPTL.

Hatua hiyo ifikiwa baada ya kufutwa kwa maazimio 12 yaliyowasilishwa awali kuhusu hatua za kuchukuliwa dhidi ya wahusika wa tuhuma hizo.

Maazimio hayo yaliyoitwa Hoja Maalumu Mpya ya Bunge yaliyosomwa na Mwenyekiti wa Kamati ya Hesabu za Serikali (PAC), Zitto Kabwe jana jioni, pamoja na mambo mengine yalitaka vyombo vya dola , polisi na Takukuru kuwachunguza watuhumiwa wote waliotajwa kwenye ripoti ya PAC.

Wahusika hao ni pamoja na waziri Muhongo, Katibu Mkuu, Maswi , Mwanasheria Mkuu wa Serikali, Werema, wajumbe wa bodi ya wakurugenzi Tanesco, Rugemalira na mmiliki wa kampuni ya IPTL , Sethi.

Maazimio hayo yalisema watuhumiwa wamesababisha hasara, taifa kukosa kodi, fedha kutumika kutoa rushwa kwa baadhi ya viongozi, wabunge, majaiji wakuu wa taasisi za umma, viongozi wa dini.

“Vitendo vilivyofanywa na watu hawani haramu ndiyo maana watu wote waliohusika na jinai wachukuliwe hatua za kinidhamu,” alisema.

Kadhalika Bunge limependekeza Rais aunde Tume ya Kijaji ya Mahakama kuwachunguza majaji wa Mahakama Kuu, Aloysius Mujulizi na Profesa Eudes Ruhangisa, waliodaiwa kuhusika kwenye sakata hilo.

Zitto alisema Bunge linapendekeza kwa kuzingatia katiba Rais aangalie uwezekano wa kuwasimamisha kazi majaji hao wakati uchunguzi unaendelea kama katiba inavyomuelekeza.

“Bunge linapendekeza Rais kuunda kijaji ya uchunguzi kuchunguza tuhumka dhidi majaji hao”

Katika mapendekezo yake limetaka pia serikali kuunda taasisi ya kushughulikia rushwa kubwa ili kuipunguzia mzigo Takukuru ambayo inaonekana imeelemewa na mzigo huo.

“Bunge linaazimia serikali iandae muswada wa mapitio ya sheria ya Takukuru ili kuwezesha kuanzisha taasisi mpya ya kushughulikia , kudhibiti vitendo vya rushwa kubwa , ufisadi, na uhuhjumu uchumi ili kuipunguzia taasisi mzigo.”

Pia Bunge limemshauri Rais kutengua uteuzi wa viongozi waliotajwa na ripoti ya CAG na Takukuru, ambao ni Waziri wa Nishati na Mdini, Profesa Muhongo, Katibu Mkuu Maswi , Mwansheria Mkuu wa Serikali Jaji Werema, Waziri wa Ardhi Professa Anna Tibaijuka, na Wajumbe wa Bodi ya Tanesco.

Kwa kuwa wengine wametajwa kushiriki kuhamisha fedha kutoka kwenye akaunti ya Escrow kwenda kwa wamiliki binafsi na wapo waliopokea fedha hizo za rushwa kutoka kwa wamiliki hao akiwamo Rugemalira.

Pia taarifa maalumu ya Bunge ilitaka Benki Kuu kuitangaza Benki ya Stanbic na nyingine zilizohusika na zitakazobainika kuwa zilishiriki kuhamisha fedha hizo zitajwe kuwa ni taasisi za fedha zinazohusika kutakatisha fedha haramu.

Bunge lilishauri wenyeviti wa Kamati za Bunge waliodaiwa kupokea mgawo wa fedha za Escrow kutoka kwa Rugemalira, Mwenyekiti wa Kamati ya Bajeti, Andrew Chenge, na Mwenyekiti wa Kamati ya Katiba na Sheria, William Ngeleja, wavuliwe madaraka kutokana na kutajwa kupokea mgawo huo.

Kadhalika Mwenyekiti wa Kamati ya Nishati na Madini, Victor Mwambalaswa, naye avuliwe madaraka kutoka na sakata hilo kumhusisha.

Bunge limeazimia pia serikali iwasilishe mikataba yote ya umeme iliyoingia baina ya wawekezaji na serikali ziwasilishwe bungeni kabla ya kumalizika bunge la bajeti la mwaka 2015/16.

“Tanesco imepata hasara kutokana na mikataba mibovu serikali iwasilishe mikataba yote ya uwekezaji mapema iwezekanavyo kabla ya kumalizika bunge la 2015/16.”

Maazimio hayo yaliwasilishwa baada ya pande zote- kambi ya upinzani na CCM pamoja wabunge wengine wa TLP na UDP kukubalina kufuta mapendekezo ya awali na kuwasilisha taarifa maalumu.

Bunge lilikuja na maazimio mapya yaliyoshirikisha kambi ya CCM na ya upinzani na kikao hicho kilikubaliana kuwa maazimio yote ya wabunge na ya serikali na ya upinzani yaondolewe na maazimio mapya yawasilishwe.

Imeandikwa na Betrice Bandawe, Gaudensia Mngumi, Moshi Lusonzo na Muhibu Said
CHANZO: NIPASHE JUMAPILI

No comments: