ANGALIA LIVE NEWS

Saturday, December 27, 2014

2014 ULIKUWA MWAKA WA DIAMOND, SOKA ILIBAKIA KATIKA SIASA


MCL
By EDO KUMWEMB (email the author) 

Na amefunga kazi kwa habari iliyotokea majuzi kuwa yeye ni miongoni mwa watu wanaomlipa mshahara Haruna Moshi Boban pale Friends Rangers.
MWAKA 2014 ulikuwa mwaka wa Diamond Platinumz. 
Mwanamuziki aliye bize kujitangaza kimataifa. Mwanamuziki anayeshinda tuzo nyingi anazoshiriki.
Na amefunga kazi kwa habari iliyotokea majuzi kuwa yeye ni miongoni mwa watu wanaomlipa mshahara Haruna Moshi Boban pale Friends Rangers.
Huku katika soka ulikuwa mwaka wa masikhara kama kawaida. Kuna upuuzi mwingi umeendelea kama kawaida. Ni kama upuuzi wa mwaka juzi, mwaka huu, na ni kama itakavyoendelea kuwa mwakani.
Wakati Diamond akiwa bize kujitangaza kimataifa, hakuna mchezaji yeyote wa Tanzania aliyetoka kwenda kujitangaza nje. Sanasana tulimpokea Shomari Kapombe aliyekuwa Ufaransa akijiandaa kucheza soka la kulipwa.
Tulichoambulia ni picha yake tu akiwa na nyota wa zamani wa Ufaransa, William Gallas. Ni mwaka ambao taifa lilijaribu kupata wachezaji imara wa timu ya taifa kupitia kwa wachezaji wasiocheza daraja lolote. Uongo huu ulioitwa Maboresho ulichekesha sana. Lakini sasa wajanja wamebadili kauli na wameita wachezaji wa Ligi Kuu na kuwaita maboresho.
Ulikuwa ni mwaka wa vioja kama kawaida. Lakini pia ulifanana na mwaka jana hasa lilipokuja katika suala la mechi ya mtani Jembe.
Yanga walimfukuza kocha wao Marcio Maximo kwa staili ile ile waliyotumia kumfukuza Ernie Brandts. Walimfukuza kwa mechi ya bonanza dhidi ya watani wao wa jadi, Simba.
Mwaka huu pia tulishuhudia mchezaji kutoka Taifa la Brazil, Emerson akisajiliwa na timu kubwa nchini Yanga, lakini alicheza kwa dakika 45 tu na kutimuliwa. Haikutimia wiki kamili tangu aliposaini mkataba klabuni hapo. Ulikuwa mwaka wa vioja sana huu. Acha upite.
Ni mwaka ambao tulishuhudia pia mfungaji bora wa Ligi Kuu msimu uliopita, Amiss Tambwe akiachwa bure na klabu yake, tena bila ya matatizo yoyote ya kinidhamu klabuni kwake. Acha huu mwaka upite tu.
Ni mwaka ambao ndoto za Taifa Stars kucheza michuano ya Afcon 2015 zilikoma rasmi katika ardhi ya Msumbiji. Ina maana kama kuna uwezekano wowote wa kucheza Afcon, basi itakuwa 2017. Lakini kwa mwenendo wa soka la nchi yetu nina hofu kuwa kama Mungu akitupa pumzi tunaweza kukutana Desemba 2016 kujadili jinsi tulivyokosa kushiriki michuano ya 2017.
Na hukuhuku katika michuano ya kimataifa, Yanga ilimsikiliza kocha wake, Maximo na kujitoa katika michuano ya Kombe la Kagame. Walitoa sababu zisizoridhisha kupitia kwa Maximo lakini niliamini kuwa ile ingekuwa michuano ambayo ingekiweka kikosi chao fiti.
Matokeo yake walimfukuza kocha huyohuyo kwa madai ya kwamba kikosi chao kilikuwa hakichezi vizuri mechi zake. Wangechezaje vizuri wakati walikimbia maandalizi ya msingi Rwanda?.Emmanuel Okwi namchukulia kama Mtanzania mwenzetu kwa sababu alikuja nchini akiwa mdogo. Aliziwakilisha tabia zetu kwa kufanya mambo yasiyoeleweka kidogo. Mwaka huu alifanikiwa kucheza timu mbili.
Ni kama ilivyokuwa kwa mwaka jana alivyocheza mechi mbili. Inaonekana kuwa kitu cha kawaida kwake.
Na inadaiwa kuwa katika siku ya uhamisho ya dirisha dogo la alikuwa anataka kwenda zake Azam.
Huu ulikuwa mwaka mwingine wa vurugu katika soka na wala hauleti matumaini ya kutufikisha popote. Na ndiyo maana haishangazi kuwa hata katika viwango vya Fifa, Taifa Stars ilikuwa inapiga hatua tano mbele kisha inapiga hatua saba nyuma.
Ni kama mwanamuziki maarufu wa kizazi kipya, Profesa J alivyoimba katika Wimbo wa Mtazamo alioshirikishwa na Afande Sele. Na ndiyo maana haikushangaza kuifunga Benin mabao 4-0 kisha wiki chache zilizofuata tukafungwa mabao 3-0 na Burundi. Hatujawahi kuwa katika mwendelezo wa ubora. Mwaka 2015 unakuja. Hakuna kitu tunachoweza kufanya katika michezo kama wadau wote hawawezi kubadili fikra zao na kuufanya mchezo wa soka kuwa biashara kama zilivyo biashara nyinginezo.
Tukiamini katika hilo tutaondoa uhuni katika michezo. Tutatengeneza sera na katiba imara kwa ajili ya kuinua michezo. Heshima itarudi kama ilivyo katika sekta nyingine.
Tusipofanya hivyo, mchezo wa soka utaendelea kuonekana wa kihuni daima milele katika ardhi ya Tanzania.
Taifa litaendelea kuzipoteza ajira ambazo hatuzioni. Tutaendelea kupotea mabilioni ya kodi kutoka kwa wanamichezo na klabu zetu. Kwa sasa hatuwezi kuziona kodi hizo kwa sababu watu wanajitengenezea kiholela tu jezi za Yanga na Simba pale Chang’ombe.
CREDIT:MWANASPOTI

No comments: