
Mafundi wakiendelea na ujenzi wa uwanja wa Simba uliopo eneo la Bunju jijini Dar es Salaam. Picha na Maktaba
Viwanja vingi vya wazi ambavyo vilitengwa kwa shughuli za michezo vimevamiwa na kufanyika ujenzi wa matumizi mengine kinyume na mipango ya awali.
UKOSEFU wa viwanja vya michezo ni tatizo ambalo limekuwa likiuandama zaidi mchezo wa soka unaopendwa na wengi.
Viwanja vingi vya wazi ambavyo vilitengwa kwa shughuli za michezo vimevamiwa na kufanyika ujenzi wa matumizi mengine kinyume na mipango ya awali.
Wakati miaka ya nyuma ilikuwa vigumu kuwa na shule isiyo na uwanja wa michezo, siku hizi ni kawaida kuona shule tena yenye wanafunzi wengi lakini haina sehemu ambayo wanafunzi hao watajihusisha na michezo.
Jambo la kusikitisha ni kwamba tatizo limekuwa likiongezeka siku hadi siku na sasa hadi baadhi ya klabu za Ligi Kuu Bara hazina viwanja vyao.
Baadhi ya klabu zinatumia viwanja vya kukodi na nyingine zinatumia viwanja ambavyo katika hali ya kawaida isingetarajiwa kwa klabu ya Ligi Kuu kutumia viwanja hivyo.
Katika hali ya kushangaza zipo klabu kongwe ambazo pamoja na kuwa na viwanja vyao lakini hawaonyeshi kuthamini viwanja hivyo na kuwa na mikakati ya kuviboresha.
Klabu hizo za Simba na Yanga hadithi ya kuwa na viwanja vyenye hadhi japo ya kufanyia mazoezi imeendelea kupuuzwa na kufanana na kisa cha funika kombe mwanaharamu apite.
Tumekuwa tukilizungumzia jambo hili mara nyingi na hata viongozi waliopewa dhamana ya kuongoza klabu hizo ni mashahidi.
Kinachotushangaza ni kwamba kuna wakati viongozi huibuka na kuonyesha dhamira ya kuvijenga au kuvikarabati viwanja hivyo lakini kinachofanyika ni kitu kidogo au kisifanyike kitu na mambo kuendelea kama kawaida.
Yanga wana uwanja wao mitaa ya Jangwani na Twiga, Dar es Salaam, kila atakayefika katika uwanja huo atakubaliana nasi jambo moja kwamba Yanga wameutelekeza uwanja wao.
Kwa Yanga kuna wakati wanaibuka na kutoa ahadi na hata viongozi wao kutembelea eneo hilo lakini baada ya hapo hakuna linalofanyika, eneo limeendelea kuwa hivyo hivyo miaka nenda rudi.
Simba wao walikuwa hawana uwanja, baada ya kelele zetu na wadau wengine, viongozi wakaona umuhimu wa kumiliki eneo lao huko Bunju B nje kidogo ya Jiji la Dar es Salaam.Kama walivyo wenzao wa Yanga nao huibuka na kuzama katika suala zima la kuliendeleza eneo lao ili liweze kuwa na japo uwanja wa kufanyia mazoezi.
Kwa wadau wa soka bila shaka wanakumbuka ahadi ya kufanya mabadiliko katika eneo hilo baada ya siku 100 lakini leo siku zaidi ya 100 zimepita hakuna jambo kubwa lililofanyika zaidi ya kufyeka eneo hilo.
Tulikuwa wa kwanza kuwazindua viongozi na mashabiki wa Simba kuhusu kutelekezwa kwa eneo hilo pamoja na mlinzi wake kutolipwa mishahara kwa muda mrefu.
Kelele zetu katika hilo walau zilisaidia kuwaamsha viongozi, wakafanya ziara katika eneo hilo na kuja na ahadi lukuki lakini hadi sasa hakuna dalili za jambo lolote la maana kufanywa.
Kwetu hii tunaiona kuwa ni aibu iliyoje kwa klabu hizi mbili kutoona umuhimu wa kuwa na viwanja vyao vya kisasa na kuishia kukodi na kutumia viwanja visivyo na hadhi.
Kinachotushangaza zaidi ni kwamba hizi klabu kongwe ndizo zilizotakiwa kuwa mfano wa kuigwa lakini aibu iliyoje wala hazijali umuhimu wa kuwa na viwanja vyao.
CREDIT@MWANASPOTI
No comments:
Post a Comment