ANGALIA LIVE NEWS

Saturday, December 27, 2014

Alipukiwa na bomu akishambulia polisi

Askari WP 8616 Mariam, akiwa amelazwa katika Hospitali ya Rufaa ya Mkoa Ruvuma jana, baada ya kujeruhiwa na bomu la kienyeji la kurushwa kwa mkono lililotaka kurushwa kwa askari hao waliokuwa doria wakati wa sherehe za Krismasi eneo la Kotazi, mjini Songea juzi na kumuua mtu mmoja anayedaiwa kutaka kufanya shambulio hilo. Picha na Joyce Joliga

Songea. Mtu mmoja mwanaume ambaye jina lake halikufahamika mara moja, amefariki dunia baada ya kulipukiwa na bomu wakati akijaribu kuwarushia polisi waliokuwa doria wakati wa Sikukuu ya Krismasi katika Kata ya Majengo, mjini hapa.
Baada ya bomu hilo kulipuka, lilimpasua tumbo mtu huyo na kumkata mkono wa kushoto ambao haukuonekana eneo la tukio. Pia liliwajeruhiwa polisi wawili.
Polisi mkoani Ruvuma ikishirikiana na makachero kutoka makao makuu ya jeshi hilo, imesema linawasaka watu wengine watatu ambao wanasadikiwa kujihusisha na ulipuaji mabomu.
Akizungumza na waandishi wa habari kwenye ukumbi wa mikutano wa Jeshi la Polisi Mkoa wa Ruvuma, Naibu Kamishna wa Jeshi la Polisi, Kaimu Mkurugenzi wa Upelelezi wa Makosa ya Jina nchini (DCP),  Diwani Athumani alisema kuwa tukio hilo limetokea jana saa 1.30 usiku katika Mtaa wa Kotazi uliopo kata ya Majengo Manispaa ya Songea.
Alieleza kuwa wakati polisi wakiwa katika doria kulitokea mlipuko wa kitu kinachodhaniwa kuwa ni bomu, lililotengenezwa kienyeji na kuwajeruhi askari wa wawili.
DCP Athumani aliwataja polisi waliojeruhiwa PC Mselem mwenye namba G 7903 ambaye alijeruhiwa mkono wake wa kushoto na alitibiwa na kuruhusiwa na  mwingine PC Mariam mwenye namba WP. 8616 alijeruhiwa kwenye bega la mkono wa kushoto na amelazwa katika Hospitali ya Rufaa ya  Mkoa Ruvuma (HOMSO) akiendelea kupata matibabu.
 DCP Athumani alieleza kuwa wahalifu hao watakamatwa kirahisi kwa kuwa baada ya mwenzao kulipukiwa na bomu hilo walijaribu kutorosha mwili wake ili kupoteza ushahidi, lakini walishindwa baada ya polisi wengine kufika eneo la tukio hilo mapema.
“Wahalifu hao waliuvuta mwili wa mwenzao kutoka katika eneo la tukio kwa umbali wa mita zisizopungua 80 na 90 kwa lengo la kutaka kupoteza ushahidi, lakini waliwahiwa na polisi wengine wa doria na kuuacha mwili na kutokomea kusikojulikana,” alisema DCP Athumani.
Alisema kuwa kikosi chache kimejipanga kukabiliana na ongezeko la matukio ya mabomu nchini na hususan mkoani humo, ambapo hilo ni tukio la tatu kwa mwaka huu.
Hata hivyo, amewaomba wadau mbalimbali wakiwamo viongozi wa dini, wanasiasa, wazee, makundi mbalimbali  ya kijamii pamoja na waandishi wa habari kuwa kitu kimoja katika kuwafichuwa waharifu hao ili matukio hayo yasiweze kujirudia tena hususan Mkoa wa Ruvuma.
Kwa upande wake Mkuu wa Mkoa wa Ruvuma, Said Mwambungu aliyetembelea eneo la tukio alisema kuwa waharifu hao wanaishi kwenye jamii hivyo ni vyema kuwafichua ili mkoa uendelee kuwa na amani.
“Nimeumizwa sana na vitendo hivi vya ulipuaji mabomu, naomba wananchi tuwafichue watu wanaofanya vitendo hivi kwani tunaishi nao kwenye jamii tuache kuyafumbia macho matendo haya mabaya ambayo ni hatari kwa jamii,” alisema Mwambungu.
Naye Mganga Mkuu Mfawidhi Hospitali ya Mkoa wa Ruvuma,  Dk Benedkto Ngaiza amethibitisha kupokea mwili mmoja  wa mtu ambaye amekufa na utumbo ukiwa umetoka nje. Pia majeruhi wawili ambao ni polisi na kwamba mmoja alitibiwa jana na kuruhusiwa huku mmoja akiwa amelazwa wodi ya majeruhi namba mbili  akiendelea kupatiwa matibabu na hali yake inaendelea vizuri.

MWANANCHI

No comments: