ANGALIA LIVE NEWS

Thursday, December 4, 2014

Escrow yamganda Pinda

Sakata la uchotaji zaidi ya Sh. bilioni 300 katika akaunti ya Escrow iliyopo Benki Kuu ya Tanzania (BoT), limeendelea kushika kasi baada ya Chama cha Wananchi (CUF) kung’ang’ania kuwa Waziri Mkuu, Mizengo Pinda anapaswa kuwajibishwa.

Mwenyekiti wa CUF Taifa, Profesa Ibrahimu Lipumba, amesema Rais Jakaya Kikwete, anapashwa achukue hatua za kumwajibisha Pinda kwa kutengua uteuzi wake kabla ya kufanyika kwa uchaguzi mkuu wa 2015 ili nchi iweze kuwa na uchaguzi wenye amani na haki.

Profesa Lipumba alitoa kauli hiyo jana kwenye mkutano mkuu wa uchaguzi wa Jukwaa la Wanawake la CUF (JUKE CUF).

Alisema kama Kikwete hatachukua hatua za kumwajibisha Pinda na viongozi wengine wakiwamo mawaziri waliotajwa katika kashfa hiyo, chama hicho kwa kushirikiana na vyama vingine vinavyounda Umoja wa Katiba ya Wananchi (Ukawa), watafanya maandamano nchi nzima kushinikiza waondolewe.

Alisema ni jambo la kushangaza kuona viongozi waliotajwa katika kashfa hiyo hadi sasa wanaendeela kuwapo katika ofisi za umma bila kuwajibika hali inayotia mashaka kuwa wanaweza kufanya njama za kubadilisha nyaraka ili kupoteza ushahidi.

“Rais Kikwete kama anataka uchaguzi uwe huru na wa amani achukue maamuzi magumu kwa kuwajibisha viongozi wote waliotajwa akiwamo Waziri Mkuu kabla ya kufanyika kwa uchaguzi mkuu unaotarajia kufanyika Oktoba mwakani,” alisema.

Lipumba alisema Pinda hawezi kusimamia utekelezaji wa maazimio ya Bunge wakati mchakato mzima wa kusaini mkataba mbovu kati ya Shirika la Umeme Nchini (Tanesco) na kampuni ya IPTL uliozua mgogoro hatimaye kufunguliwa kwa akaunti ya Tegeta Escrow ambayo ilitumika kuchota mabilioni hayo ya fedha.

“Katika hali iliyopo sasa nchini, Rais Kikwete anatakiwa kuteua Waziri Mkuu mpya ambaye hana nia ya kugombea urais 2015 na hatajwi katika kashfa ya ubadhirifu wa fedha za umma,” alisema Lipumba.

Alisema serikali ya Chama Cha Mapinduzi (CCM) imepoteza sifa ndani na nje ya nchi kutokana na kuandamwa na kashfa kila mara, hivyo ni wakati sasa kwa vyama vinavyounda Ukawa kuchukua hatamu ya uongozi ili kurudisha heshima ya nchi.

Kuhusu katiba, alisema katiba pendekezi iliweka vifungu vilivyopendekezwa na wananchi vikiwataka viongozi wa umma kuwa na akaunti nje ya nchi, lakini viliondolewa ndani ya Katiba mpya iliyopendekezwa na Bunge Maalum la Katiba.


“Katiba mpya imeondoa vifungu muhimu vyote, jambo hilo halikubaliki kwani ni maridhiano, hivyo hiyo katiba iliyopendekezwa haikubaliki,” alisema Lipumba.
Aliongeza kuwa wale viongozi walioko madarakani hawana budi kufuata haki na sheria wakati wa kutekeleza majukumu yao vinginevyo hali ya uchumi wa nchi itaendelea kuporomoka.

MAPENDEKEZO YA WABUNGE
Mwishoni mwa wiki iliyopita, wabunge walitoa maazimio manane kuhusu sakata la Escrow likiwamo la kutenguliwa kwa nyadhifa za Waziri wa Nishati na Madini, Profesa Sospeter Muhongo, Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi, Profesa AnnaTibaijuka na Mwanasheria Mkuu wa Serikali (AG), Frederick Werema.

Wengine waliopendekezwa kuvuliwa yadhifa zao ni wenyeviti wa kamati za kudumu za Bunge hilo, William Ngeleja (Sheria, Katiba na Utawala), Andrew Chenge (Bajeti) na Victor Mwambalaswa (Nishati na Madini).

Pia wamo Katibu Mkuu wa Wizara ya Nishati na Madini, Eliakim Maswi na Bodi ya Wakurugenzi ya Shirika la Umeme Tanzania (Tanesco).

Viongozi wa umma na maofisa wa ngazi za juu serikalini wanapaswa kuwajibika kwa sababu wamehusishwa na vitendo vya kijinai katika sakata hilo linalohusisha kampuni ya kufua umeme ya Independent Power Tanzania (IPTL).

Kadhalika, Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (Takukuru), Jeshi la Polisi na vyombo vingine vya ulinzi na usalama, vimetakiwa kufanya uchunguzi dhidi ya wote waliotajwa kuhusika na sakata hilo na kupendekeza watakaobainika kuhusika wachukuliwe hatua.

Maazimio mengine ni kumtaka Rais kuunda Tume ya Uchunguzi ya Kijaji kuchunguza tuhuma za utovu wa maadili dhidi ya majaji kuhusishwa kwenye kashfa hiyo.

Majaji waliotakiwa kuchunguzwa ni Jaji Aloysius Mujulizi na Jaji Prof. Eudes Ruhangisa wa Mahakama Kuu ya Tanzania.

Aidha, Bunge lilitaka mamlaka husika za kifedha na za kiuchunguzi kuitaja Stanbic Bank Tanzania Ltd na benki nyingine yoyote itakayogundulika baada ya uchunguzi wa mamlaka za kiuchunguzi, kujihusisha na utakatishaji wa fedha zilizotolewa katika akaunti ya Escrow, kuwa ni taasisi zenye shaka ya utakatishaji wa fedha haramu.

Pia, Serikali iandae na kuwasilisha Muswada wa Marekebisho ya Sheria iliyounda Takukuru kwa lengo la kuanzisha taasisi mahususi itakayoshughulikia, kupambana na kudhibiti vitendo vya rushwa kubwa, ufisadi na hujuma za uchumi zinazotishia uhai wa taifa kiuchumi, kijamii na kisiasa kutokana na kushamiri kwa vitendo hivyo.

Serikali imetakiwa kutekeleza azimio la Bunge kuhusu mikataba mibovu ya kuzalisha umeme kati ya Tanesco na kampuni binafsi ya kufua umeme na hivyo kuwasilisha taarifa ya utekelezaji wa mapitio ya mikataba ya umeme kabla ya kumalizika kwa Mkutano wa Bunge la Bajeti.

Akizungumzia kuhusu uchaguzi wa JUKE CUF, Lipumba aliwataka wanachama wake kujitokeza kwa wingi kugombea nafasi mbalimbali ndani na nje ya chama hicho.

Alisema takwimu za chaguzi mbalimbali zinaonyesha kuwa wanawake ndiyo wanaoongoza kupiga kura, hivyo ni lazima apatikane kiongozi ambaye atasimamia na kuwaongoza.

“Mwanamke ni kioo cha jamii na uchungu wa mwana aujuae ni mzazi, hivyo kwa kuwa mwanamke ndiye mpigakura hamna budi kupambana ili tuitoe CCM madarakani,” alisema.

Kwa upande wake mgombea uenyekiti wa JUKE, Najma Khalifan, alijinadi akisema endapo atashinda atashirikiana na viongozi wengine hususani wanawake katika utekelezaji wa miradi ya maendeleo.

Kwa upande wake, Fatma Fereji, ambaye naye anagombea nafasi hiyo, aliwataka wanawake kujitokeza kuwania uongozi ndani na nje ya chama hicho ili wabadilishe mfumo wa uchumi wa nchi.
CHANZO: NIPASHE

2 comments:

Anonymous said...

Tusipokuwa makini waTANZANIA Raisi ajaye akitoka CCM tumekwisha nikiwa mwana CCM Miaka nenda rudi zipo njama za hali ya juu hasa nchi inamezwa!! Ukimya huu wa hata mkuu wetu hataki kuliona hilo ina maana kuna kulindana kwa hali ya juu sana na hawa wahusika wamekuwa wanatamba hakuna atakayeniweza!! Hali ni mbya sana turuhusiwe kudai haki zetu kwa maandamano na vyombo vya dola acheni wananchi wadai haki zao kwa amani!!

Anonymous said...

pinda amefanywa kama mbuzi wa kafara wako wengi tu wakuu katika serikalini wamechota pesa wanamsingizia pinda na ndo maana hawataki kujiuzulu na ndo maana mkuluu ananyamaza kimya.

wajinga watanzania watachezewa mchezo watasahau sakala hili.ngoja tusubiri story za kina wema sepetu kama kawaida yetu na makali yatuishe nchi ifilisiwe zaidi.ndo mpango mzima.