ANGALIA LIVE NEWS

Friday, December 26, 2014

Maaskofu: Watuhumiwa wa Escrow washitakiwe


  Wataka katiba isiharakishwe
  Wadai tume huru ya uchaguzi


Kiongozi wa Kanisa la Kiinjili la Kilutheri Tanzania (KKKT), Dk. Alex Malasusa, akihubiri wakati wa Ibada ya sikukuu ya Krismas katika Kanisa Kuu la KKKT Azania Front jijini Dar es Salaam jana.(Picha: Khalfan Said).

Viongozi wa madhehebu mbalimbali ya Kikristo nchini, wamemtaka Rais Jakaya Kikwete, kutowaonea haya viongozi wasiokuwa waadilifu wanaokwenda kinyume cha maadili katika kushughulikia mambo mbalimbali.

Kama vile fedha zilizokuwa zikihifadhiwa katika akaunti ya Tegeta Escrow, iliyokuwa Benki Kuu ya Tanzania (BoT), badala yake achukue hatua za haraka kuwawajibisha na washitakiwe bila kusubiri kelele za wananchi.

Pia wamewataka watu waliohusika kwenye vitendo vya rushwa, ikiwa ni pamoja na kupokea mabilioni ya shilingi, kwenda kanisani kutubu badala ya kuzunguka huku na kule wakikanusha.

Vilevile, wametaka upatikanaji wa Katiba mpya usiharakishwe, lakini wakasisitiza uwapo wa tume huru ya uchaguzi kabla ya kuitishwa kwa uchaguzi mkuu mwaka 2015.

Walitoa matamko hayo kwa nyakati tofauti katika salamu zao za sikukuu ya Krismas, iliyoadhimishwa duniani kote jana.

ASKOFU MALASUSA
Askofu Mkuu wa Kanisa la Kiinjili la Kilutheri Tanzania (KKKT), Dk. Alex Malasusa, aliwataka watu waliohusika kwenye vitendo vya rushwa, ikiwa ni pamoja na kupokea mabilioni ya shilingi, kwenda kanisani kutubu badala ya kuzunguka huku na kule wakikanusha, kwani Mungu hapendezwi na vitendo hivyo.

Alisema muumini wa kweli anapoona ametenda kosa huenda mbele za Mungu kutubu.

Dk. Malasusa alitoa kauli hiyo wakati akitoa ujumbe wa Sikukuu ya Krismasi katika kanisa hilo, lililopo Azania Front, jijini Dar es Salaam jana.

Aliwataka watu wote walioshiriki katika vitendo vya rushwa, vikiwamo vya kupokea mabilioni ya shilingi waache kuzunguka mitaani na kujitetea, bali waende kanisani kutubu mbele za Mungu, kwani hiyo ndiyo sifa ya muumini wa kweli.

“Wale wote, ambao wamehusishwa na rushwa, wasikae na kuzunguka kukanusha, wanachotakiwa ni kwenda kutubu kwa vitendo viovu walivyofanya,” alisema Askofu Malasusa.

Aliongeza: “Haiwezekani watu wachukue mabilioni ya shilingi mali za wananchi, huku wananchi wakiendelea kuishi katika umaskini uliokithiri.”

Hata hivyo, Dk. Malasusa hakubainisha wazi iwapo watu hao ni pamoja na waliohusika katika kashfa ya IPTL ya uchotwaji wa zaidi ya Sh. bilioni 300 katika akaunti ya Tegeta Escrow, iliyokuwa Benki Kuu ya Tanzania (BoT) au la.
Pia aliwataka Watanzania kuwa waombaji ili kuepukana na matukio ya uovu, ambayo yamekuwa yakiendelea kujitokeza.

Alisema hivi karibuni watu wameendelea kushuhudia kujitokeza kwa migogoro kati ya mihimili na mihimili kutokana na ubadhirifu na kukosekana kwa uaminifu.

Askofu Malasusa alisema kutokea kwa matukio hayo kunatokana na kuendelea kwa vitendo vya uovu na hivyo kuwataka Watanzania kumwomba Mungu, kwani vitendo hivyo ndivyo vilivyosababisha hali iliyopo sasa.
Aliwataka Watanzania kuendelea kukemea vitendo vya unyanyasaji kwa watoto.

ASKOFU KINYUNYU
Askofu wa Kanisa la Kiinjili la Kilutheri Tanzania (KKKT), Dayosisi ya Dodoma, Amon Kinyunyu, aliitaka serikali kuchukua hatua haraka za kisheria kuwawajibisha watuhumiwa wote wa vitendo vya ufisadi, wakiwamo waliohusishwa na kashfa ya akaunti hiyo, badala ya kusubiri kelele za wananchi. Askofu Kinyunyu alitoa kauli hiyo wakati akitoa salamu za Krismasi katika Kanisa Kuu la Dodoma mjini.

“Tatizo la nchi yetu imekuwa zimamoto. Inatakiwa kutekeleza na kusimamia maadili na sheria za utumishi wa umma. Isingoje mpaka wananchi kupigia kelele, wanahatarisha usalama wa nchi,” alisema Askofu Kinyunyu.

Alisema baadhi ya watuhumiwa wa kashfa ya akaunti hiyo waliovuliwa nyadhifa walizokuwa nazo serikalini, wanatakiwa kurudisha fedha walizochukua na kisha wachukuliwe hatua za kisheria ili iwe fundisho kwa viongozi wengine wa umma.

Askofu Kinyunyu alisema tatizo kubwa lililopo kwa baadhi ya viongozi, wanapoingia madarakani wanawaza kujilimbikizia mali, badala ya kukumbuka kuwahudumia wananchi.

ASKOFU MICHAEL
Askofu wa Kanisa la Anglikana, Dayosisi ya Zanzibar, Michael Henry Hafidh, alimtaka Rais Kikwete kutowaonea haya viongozi wasio waadilifu wanaokwenda kinyume cha maadili ya kazi yao na kuwataka awajibishe.

Alitoa kauli hiyo wakati akihubiri katika ibada ya kitaifa iliyofanyika katika Kanisa la Umoja la Chuo Kikuu cha Dar es Salaam.

Alisema Rais Kikwete hana haja ya kuwalinda viongozi wake wanaobainika kukiuka miiko ya uongozi kwa sababu ana mamlaka ya kuwawajibisha, hivyo anatakiwa asisite anapotakiwa kufanya hivyo.

“Unakuta eti kiongozi anaingia mikataba mibovu halafu anapokuja kuulizwa, anasema aliingia kwa bahati mbaya, hivi inawezekanaje mtu anaingia mwenyewe mikataba hiyo mibovu halafu eti anapoulizwa anasema ni bahati mbaya, hii haikubaliki,” alisema Askofu Hafidh.

Aliongeza: “Hapa hakuna bahati mbaya. Wanafanya makusudi. Watu kama hawa ni lazima wachukuliwe hatua kali. Kwa sababu waliwekwa madarakani ili kuwasaidia wananchi. Lakini wao wanalewa madaraka na kuyaumia vibaya.”

ASKOFU MLOLA
Serikali imetakiwa kufanya uchunguzi haraka ili kuhakikisha watu wote waliyohusishwa na tuhuma za wizi wa Escrow wanafikishwa Mahakamani.

Askofu wa Jimbo la Kigoma, Joseph Mlola, akizungumza jana katika ibada ya Sikukuu ya Krismasi katika Kanisa Kuu la Bikira Maria Mshindaji, lililopo mjini Kigoma, alisema hatua iliyochukuliwa na Rais Kikwete kumfukuza kazi aliyekuwa Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi, Profesa Anna Tibaijuka, ni nzuri.

Hata hivyo, alitaka na uchunguzi unaofanywa dhidi ya watuhumiwa wengine wa kashfa ya akaunti hiyo, ufanyike haraka ili hatua ziuchukuliwe, ikiwamo kufikishwa mahakamani. Alisema kumfukuza kazi waziri na kumuacha bila kufikishwa mahakamani haisaidii kuondoa matatizo, bali inayaongeza kwa sababu viongozi wengine hawajifunzi.

Pia alisema uamuzi wa kumfukuza Profesa Tibaijuka bila kurudisha fedha alizochukua na kufikishwa mahakamani kutawafanya viongozi wengine kufanya ubadhirifu wakitarajia kuachishwa tu nafasi zao za uongozi bila kuchukuliwa hatua.

ASKOFU NGALALEKUMTWA
Rais wa Baraza la Maaskofu Katoliki Tanzania (TEC), Askofu Taricisius Ngalalrkumtwa, alisema sera mbovu, uongozi usiozingatia maslahi ya wananchi walio wengi pamoja na ulafi wa baadhi ya viongozi ndiyo chanzo cha umaskini wa Watanzania kwenye nchi iliyobarikiwa kila aina ya rasilimali, yakiwamo madini, ardhi ya kutosha, misitu na mbuga za wanyama.

Alisema hayo wakati akitoa mahubiri kwenye ibada ya sherehe za Krismas, iliyofanyika katika Kanisa Kuu la Moyo Mtakatifu wa Yesu Kihesa, mjini Iringa.

Ngalalekumtwa, ambaye pia ni Askofu wa Jimbo Katoliki la Iringa, alisema anashangazwa na maneno yanayoeleza kuwa Tanzania ni nchi maskini, huku ikiwa na utitiri wa maliasili, ambazo baadhi yake hazipatikani sehemu nyingine kokote duniani.

“Nashangaa kila siku tunaambiwa nchi hii ni maskini, hivi ni kweli nyie ni maskini. Mna gesi mna ardhi ya kutosha mna mafuta mna wanyama wa kila aina kweli huu ni umaskini?” alihoji Askofu Ngalalekumtwa.

Aliongeza: “Ninachokiona hapa ni sera mbovu, ulafi, ubinafsi wa viongozi wenu ndiyo sababu ya umaskini huu.

Lakini nchi hii siyo maskini. Mnapokuwa na viongozi wachoyo wanaojilimbikizia mali kwa mabilioni, msitegemee kuna siku maisha ya watu yataboreshwa, kwani viongozi wanaojilimbikizia mali bila kujali wananchi wao ni wale waliofilisika kisiasa na ndiyo chanzo cha kukumbatia sera mbovu zisizo na tija kwa wananchi na taifa.”

“Ndugu zangu, huu ni umaskini wa mawazo na ulafi usio na maana. Hivi mtu mmoja anakusanya mabilioni ya pesa tena isivyo halali atakula lini pesa zote hizo?

Huu ni uchoyo na kutowajali wengine ndiyo maana mtu anajawa tamaa ya kuwa na vitu vingi bila kujali atazitumiaje. Wakristo tujitafakari na kuona maana ya mtoto Yesu aliyezaliwa huko Bethlehemu ili tuuone upendo wa Mungu kwa mwanaadamu.”

Askofu Mkude: Katiba isiharakishwe
Askofu wa Kanisa Katoliki Jimbo la Morogoro, Telesphor Mkude, amesema hakuna haja ya kuharakisha Katiba iliyopendekezwa itumike katika uchaguzi ujao.

Badala yake, Askofu Mkude amesema Katiba inapaswa kujadiliwa na wananchi kwa mapana na kuweka maoni yao yatakayosaidia kuiboresha ili kuwa na Katiba bora.

Aliyasema hayo wakati akitoa maoni yake baada ya kumalizika kwa ibada ya misa takatifu ya kusherehekea sikukuu ya Krismas iliyofanyika katika Kanisa Kuu la Mtakatifu Patrice la mjini hapa.

Alisema kuwa licha ya Bunge Maalum kupendekeza Katiba ili ipigiwe kura na wananchi, lakini kutokana na msuguano uliopo kuhusu katiba hiyo, ni vyema isitumike katika uchaguzi mkuu ujao ili kutoa fursa kwa wananchi kuweka maoni yao ambayo yataiboresha ikubalike na makundi yote.

Askofu Mkude alisema kuwa kwa sasa inaonekana Katiba iliyopendekezwa imewekwa katika msukumo wa kundi fulani na kutokubalika na makundi mengine, hivyo ili kuwa na Katiba bora na yenye kuunganisha taifa, ni vyema ikashirikisha upya wananchi kutoa maoni yao.

Kuhusu sakata la Tegeta Escrow, Askofu Mkude aliwasifu wabunge bila kujali itikadi za vyama kuhoji kwa pamoja uchotwaji wa fedha hizo na kwamba wameonyesha namna walivyochukizwa na hali hiyo.

Alisema kuwa sakata hilo hivi sasa limekuwa fundisho kwa viongozi wengine wanaofikiri kufanya majaribio kama hayo kuingiwa na woga wa kudokoa fedha za umma wakitambua kuwa wataumbuliwa.

Hata hivyo, Askofu Mkude alimpongeza Rais Jakaya Kikwete, kwa maamuzi yake ya kutoa ufafanuzi wa suala hilo pamoja na kuwawajibisha baadhi ya viongozi waliohusishwa katika sakata hilo.

Askofu Mameo: Wananchi ombeeni uchaguzi ujao
Kwa upande wake, Askofu wa Kanisa la Kiinjili la Kilutheri Tanzania (KKKT) Dayosisi ya Morogoro, Jacob Mameo, amewaomba waumini wa kanisa hilo kuiombea nchi isiingie katika machafuko kwenye uchaguzi mkuu wa mwakani.

Askofu Mameo aliyasema hayo wakati wa mahubiri yake katika misa ya sikukuu ya Krismasi iliyofanyika katika Kanisa Kuu la Bungo mjini hapa.

Alisema Taifa linapaswa kuombewa ili kupita salama katika uchaguzi mkuu wa Rais, wabunge na madiwani. Alisema ni jambo jema kwa Wakristo kuhakikisha siku zote wanakuwa katika maombi ili Taifa iendelee kuwa na amani na utulivu.

Na katika hatua nyingine, amewaomba viongozi waliochaguliwa katika uchaguzi wa serikali za mitaa, vitongoji na vijiji, kutenda haki kwa Watanzania na kuwajibika kwa uzalendo kwa ajili ya maendeleo ya nchi.

Askofu Kakobe: Amani imebaki kama bomu
Askofu Mkuu wa Kanisa la Full Gospel Bible Fellowship, Zacharia Kakobe, amesema amani ya Tanzania imebaki kama bomu lililotegwa mahali fulani na linasubiri kulipuka kutokana na watawala kutokubali mabadiliko.
CHANZO: NIPASHE

No comments: